Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Singida             

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Singida imemuhukumu mkazi wa Kijiji cha Unyianga, katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida, Omari Hamisi (23) adhabu ya kutumikia kifungo cha maisha jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumbaka motto mdogo wa kike mwenye umri wa miaka 2 na nusu.

Mwendesha Mashtaka, wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya taifa ya mashtaka Mkoa wa Singida, Foibe Malecela alidai kwamba Julai, 14, 2024 akiwa katika Kijiji cha Ighuka, Wilaya ya Ikungi, Mkoani Singida, Omari Hamisi alimbaka mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 2 na nusu huku akijua kuwa kwa kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Aidha katika shauri hilo la jinai lililofunguliwa katika Mahakama hiyo Julai 25, 2024 na kusajiliwa kwa namba 20850/2024 lilikuwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Allu Nzowa na aliposomewa shitaka hilo mshitakiwa alikana na ndipo upande wa mashtaka ulipeleka mashahidi watano ambao walitoa ushahidi bila kuacha shaka yeyote kuwa mshitakiwa huyo ndiye aliyetenda kosa hilo.

Hata hivyo Foibe alidai kwamba mshitakiwa Omari Hamisi alijitetea mwenyewe huku akiungwa mkono na ushahidi wa mtu mmoja aliyempeleka katika Mahakama hiyo.

Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka huyo baada ya Mahakama kusikiliza pande zote mbili ilimtia hatiani kwa kosa hilo la kubaka na hivyo ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama ya mshitakiwa, Mahakama hiyo ilimuhukumu adhabu ya kifungo cha maisha jela.