Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Kassim Majaliwa Majaliwa amevutiwa na utendaji na mafanikio iliyopata Shirika la Maendeleo la Taifa (STAMICO) kwa kipindi kifupi.

Pongezi hizo alizotoa leo tarehe 24 Juni,2025 jijini Dodoma katika hotuba yake wakati wa uzinduzi wa mitambo ya uchorongaji kwa wachimbaji wadogo na vitendea kazi vya STAMICO

“Nimpongeze sana Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO,Dkt. Venance Mwasse na watendaji wote kwa mageuzi makubwa katika kipindi kifupi”,amesema.

Ameongeza kuwa mageuzi yaliyofanywa na STAMICO yametokana na uongozi madhubuti na kuongeza kuwa Shirika limekuwa la mfano wa kuigwa.

Akitoa maelezo mafupi katika hafla hiyo,Dkt Mwasse ameyataja kati ya mambo makubwa yaliyofanyika kwenye kipindi husika kuwa ni pamoja na ufufuaji wa mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira ambao serikali ilikuwa inatumia gharama kubwa kuulinda ambapo kwa sasa umekuwa ni chanzo kikubwa cha fedha za kigeni tangu ulipopofufuliwa.

Dkt. Mwasse amesema pamoja na mageuzi hayo katika mgodi wa Kiwira, STAMICO pia inaendesha mradi wa kimageuzi wa Rafiki Briqquete ambao ni mradi wa kuzalisha nishati safi ya kupikia ambao nao umekuwa tegemeo kwa taasisi mbalimbali ambazo zinanunua nishati hiyo huo ikiwemo Jeshi la Magereza.

Ameongeza kuwa katika kuhakikisha nishati safi hiyo inasambazwa zaidi, wameingia makubaliano na vikundi mbalimbali vya wanawake kwenye jamii ikiwemo Wanawake na Samia ili wawe mawakala wa nishati hiyo.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwasse amesema kutokana na uendelezaji wenye ufanisi uliofanywa na serikali, STAMICO imepata mafanikio makubwa ikiwemo kuongeza uwezo wa ukusanyaji mapato kutoka shilingi bilioni 1.35 mwaka 2018/19 hadi shilingi bilioni 85.3 mwaka 2023/24.

Ameongeza kuwa uwezeshaji huo umeifanya STAMICO kupunguza utegemezi wa fedha kutoka serikalini kutoka asilimia 89 na kwa sasa shirika linajilipa mishahara na kugharamia shughuli zake za uendeshaji.

“Kwa sasa Shirika linajitegemea fedha za matumizi mengineyo (OC) ya shilingi bilioni 1.1 tangu mwaka 2023/24 na linajitegemea kwa kujilipa mishahara ambapo limeokoa shilingi bilioni 6.4 kwa mwaka, kuanzia mwaka 2024/25” amesema.