Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia Dodoma
Katika kuenzi afya ya mtumishi wa umma kama msingi wa ufanisi wa taasisi za Serikali, Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Taasisi zake imeandaa bonanza la michezo lililowakutanisha viongozi na watumishi wake kwa lengo la kuhamasisha utamaduni wa mazoezi, kuimarisha mshikamano na kuongeza ari ya utendaji.
Akizungumza kwenye bonanza hilo mapema leo Jijini Dodoma June 28,2025 Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesisitiza kuwa Sekta ya madini haiwezi kufanikisha mipango yake pasipo kujenga msingi imara wa afya na maelewano miongoni mwa watumishi.

“Kuwa na afya njema ni mtaji wa kwanza wa utumishi,mabadiliko tunayoyalenga katika sekta yetu hayawezi kufikiwa kama tutapuuzia afya, mshikamano, na maadili ya kazi,hili bonanza ni ishara ya namna tunavyojipanga kuwa timu moja yenye ufanisi,” amesema Mavunde.
Katika hotuba yake, Waziri huyo pia ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira bora ya kisera na kiutendaji yaliyochochea maendeleo makubwa ndani ya sekta ya madini.
Aidha, ameipongeza menejimenti ya wizara ikiongozwa na Katibu Mkuu, kwa usimamizi madhubuti unaolenga kuwatengenezea watumishi mazingira ya kazi yaliyo salama, rafiki na yanayochochea ubunifu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Yahya Ismail Samamba ameeleza kuwa bonanza hilo si tukio la kawaida bali ni utekelezaji wa sera ya maendeleo ya rasilimali watu kwa njia ya afya, ustawi na mshikamano kazini.
“Tumejifunza kwamba afya bora inakwenda sambamba na tija kazini, Michezo kama hii hutoa nafasi ya kutathmini sio tu hali ya miili yetu, bali pia mahusiano na hali ya mazingira ya kazi tunayoshiriki kila siku,” amesema Katibu Mkuu.
Ameongeza kuwa mabonanza hayo yamekuwa sehemu ya kalenda ya wizara, na kwamba michezo si burudani pekee bali ni fursa ya kujifunza, kuunganishwa na kujipanga upya kwa mafanikio makubwa zaidi.
Naye Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, ametumia nafasi hiyo kumpa heshima Waziri kwa kuwa kiongozi anayeamini katika ushirikiano, uthubutu na ufuatiliaji wa karibu sifa ambazo, amesema, zimepelekea mafanikio yanayoonekana katika sekta hiyo.

Ametaja Maono ya Bonanza hilo kuwa ni Kuimarisha afya na kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza,kuweka msingi wa ushirikiano na mshikamano kazini,Kukuza ari ya utumishi, uwajibikaji na kuhimiza morali ya kazi na kutekeleza kwa vitendo miongozo ya Serikali kuhusu afya kazini ikiwa ni pamoja na kujenga taswira chanya ya sekta ya madini kama chombo cha maendeleo ya kweli.


