Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Jumla ya wagombea kumi wamechukua fomu za kugombea ubunge wa Jimbo la Kibaha Mjini, akiwemo mbunge aliyemaliza muda wake, Silvestry Koka, katika kipindi cha siku mbili tangu kuanza kwa zoezi hilo tarehe 28 Juni, 2025.
Kwa upande wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), jumla ya wagombea 22 wa viti maalum vya udiwani wamejitokeza hadi sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu wa CCM Wilaya ya Kibaha Mjini, Isaack Kalleiya, alisema kati ya wagombea hao wa ubunge, wanaume ni tisa na mwanamke mmoja.
“Hali ya uchukuaji fomu katika mji wa Kibaha inaendelea vizuri, Idadi kubwa ya watu kujitokeza ni ishara ya imani ya wanachama kwa chama chao, hadi sasa hakuna malalamiko yoyote,” alifafanua Kalleiya.
Aidha, Kalleiya alitoa onyo kwa wagombea wanaodhani kuwa kuchukua au kurejesha fomu ni ruhusa ya kuanza kampeni, akisisitiza kuwa kampeni zitafanyika kwa mujibu wa taratibu rasmi za chama.
Aliyekuwa Mbunge wa Kibaha Mjini, Silvestry Koka, alisema kuwa ametekeleza wajibu wake kama mwanachama wa CCM kwa kuchukua fomu ya kuwania tena nafasi hiyo baada ya kuitumikia kwa kipindi cha miaka 15 (vipindi vitatu) tangu mwaka 2010.
“Nimetimiza wajibu wangu kama mwanachama. Nimechukua fomu kutetea nafasi hii. Lakini natambua kwamba uteuzi ni kwa mujibu wa vikao vya chama kuanzia ngazi ya wilaya hadi taifa — niteuliwe au nisiteuliwe,” alisema Koka.
Aliongeza kuwa iwapo atateuliwa, ataendelea kumnadi mgombea urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na mgombea mwenza wake, sambamba na mgombea urais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi.
“Nimeikuta CCM ikiwa imara katika jimbo la Kibaha na nawajibika kuendelea kuifanya ikiwa imara nikiwa kiongozi na hata kama sitokuwa madarakani nawajibika kuiacha ikiwa imara kama nilivyoikuta imara, Kwa misingi hiyo nimejiandaa kwa yote mawili kupata ama kukosa “alibainisha Koka.
Koka alishukuru kwa kipindi cha uongozi wake mengi yamefanyika na anajivunia kuiona Kibaha Mji ya sasa sio ile ya zamani, kimaendeleo na kiuchumi na sasa imepanda hadhi kuwa Manispaa.
Baadhi ya wagombea wengine waliochukua fomu jimbo la Kibaha Mjini ni pamoja na Mussa Mansour, Godwin Ndosi ,Ibrahim Mkwiru na dkt. Charles Mwamwaja.


