Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Kagera, ambapo zaidi ya Shilingi trilioni 1.131 zimetolewa kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi Aprili 2025.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Hajjat Fatma Mwassa, amesema fedha hizo zimetumika katika sekta muhimu kama afya, elimu, maji, barabara, nishati, kilimo, biashara na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, hali iliyosababisha mageuzi makubwa ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Kagera.

Akizungumza leo Julai 1, 2025 jijini Dodoma, Mkuu huyo wa Mkoa amesema Kagera ina wilaya 7, halmashauri 8, kata 192, vijiji 662 na vitongoji 3,728, huku ikiwa na idadi ya watu wapatao 2,989,299 kwa mujibu wa Sensa ya 2022, hivyo kushika nafasi ya sita kitaifa kwa idadi ya watu. Aidha, zaidi ya asilimia 80 ya wakazi wa Mkoa hutegemea kilimo kama chanzo kikuu cha kipato na chakula.

Kwa upande wa sekta ya afya, zaidi ya Shilingi bilioni 146.3 zimetumika kujenga na kuboresha huduma za afya ambapo hospitali zimeongezeka kutoka 3 hadi 11, vituo vya afya kutoka 29 hadi 42, na zahanati kutoka 217 hadi 283. Aidha, huduma za kibingwa na vifaa tiba vya kisasa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa vimesababisha ongezeko la asilimia 273 ya wagonjwa waliotibiwa ndani ya Mkoa.

Katika sekta ya elimu, amesema zaidi ya Shilingi bilioni 128.05 zimetumika kuongeza shule mpya 116 za msingi na awali, sekondari 68, na vyuo vya VETA kutoka 4 hadi 9. Pia vyumba vya madarasa 4,709, maabara 167, na mabweni 121 yamejengwa. Ufaulu wa sekondari umeimarika kutoka asilimia 91 hadi 94.57.

Huduma ya maji nayo imeboreshwa kwa kiwango kikubwa ambapo upatikanaji umefikia asilimia 93 mijini na asilimia 83 vijijini, baada ya utekelezaji wa miradi 41 ya maji yenye thamani ya Shilingi bilioni 164.7. Miradi mikubwa ni pamoja na ule wa Kyaka–Bunazi, Kemondo na Kayanga–Omurushaka.

Katika miundombinu, Serikali imetoa Shilingi bilioni 117.9 kwa ajili ya barabara na madaraja, ikiwa ni pamoja na Daraja la Kitengule na barabara ya Bugene–Kasulo–Kumunazi. Barabara za mijini zimeongezeka hadi kilomita 40.87 huku idadi ya madaraja ikifikia 468.

Kwa upande wa nishati, Mwassa amesema vijiji vyote 662 vimeunganishwa na umeme, sawa na asilimia 100, huku vitongoji vilivyounganishwa vikiwa 1,763 kati ya 3,665. Hali hiyo imechochewa na kuunganishwa kwa Mkoa na Gridi ya Taifa badala ya kutegemea umeme kutoka Uganda.

Sekta ya kilimo pia imeimarika ambapo Serikali imepunguza tozo za zao la kahawa kutoka 17 hadi 5, hali iliyopelekea kupanda kwa bei ya kahawa kutoka Shilingi 1,200 hadi 4,200 kwa kilo, na uzalishaji kufikia tani 54,203.

Ameeleza kuwa katika uwezeshaji wananchi kiuchumi, mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu imeongezeka kutoka Shilingi bilioni 3.2 hadi bilioni 9.4, huku kaya zinazofaidika na mpango wa TASAF zikifikia 380,035. Mkoa pia umeanzisha mashamba ya vijana (block farms) na kongani maalum kwa ajili ya kilimo.

Idadi ya biashara rasmi imeongezeka kwa asilimia 55, huku wawekezaji waliosajiliwa kupitia TIC wakifikia 275 waliowekeza miradi yenye thamani ya Shilingi bilioni 267.1 na kutoa ajira zaidi ya 11,000.

Kwa upande wa mapato ya ndani, halmashauri za Mkoa zimekusanya jumla ya Shilingi bilioni 175.8 katika kipindi cha miaka mitano, kutoka bilioni 23.6 mwaka 2020/21 hadi bilioni 47.2 mwaka 2024/25.

Pia Mkoa umetekeleza miradi 28 ya kimkakati kupitia mapato ya ndani ya halmashauri yenye thamani ya Shilingi bilioni 25.93, ikijumuisha ujenzi wa masoko ya kisasa, shule za michepuo ya Kiingereza, stendi mpya za mabasi na barabara za lami ndani ya Manispaa ya Bukoba.

Amesema, “Mafanikio haya yanadhihirisha dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi wote bila kubagua. Tutaendelea kusimamia kwa weledi utekelezaji wa miradi yote kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” amesema.