Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Wakandarasi wazawa nchini sasa wanapata unafuu mkubwa wa mtaji kupitia mpango mpya wa hatifungani maalum ya miundombinu iliyoanzishwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kushirikiana na Benki ya CRDB, kwa lengo la kuharakisha utekelezaji wa miradi ya barabara na kuwawezesha wazawa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

Hatifungani hiyo, inayojulikana kwa jina la Samia Infrastructure Bond, ilizinduliwa rasmi Novemba 29, 2024 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, ikiwa ya kwanza nchini kwa sekta ya miundombinu. Lengo kuu la mpango huo ni kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya barabara vijijini na mijini kwa kushirikisha wakandarasi wa ndani.

Akizungumza na vyombo vya habari, Mhasibu Mkuu wa TARURA, CPA Jacob Nyaulingo, amesema kuwa mpango huo ni matokeo ya wazo la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa, aliyetilia mkazo umuhimu wa kuwa na chanzo mbadala cha fedha kwa ajili ya miundombinu.

“Awali tulitarajia kukusanya shilingi bilioni 150 kupitia hatifungani hiyo, lakini kutokana na mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi na taasisi mbalimbali, kiasi kilichokusanywa kilifikia shilingi bilioni 323, sawa na asilimia 215.4 ya lengo la awali,” alisema Nyaulingo.

Kwa mujibu wake, fedha hizo zimeelekezwa moja kwa moja kwenye miradi ya barabara inayosimamiwa na TARURA ili kuhakikisha utekelezaji wake unakwenda kwa kasi na kwa viwango vinavyokubalika. Amesema ili kuondoa urasimu katika upatikanaji wa fedha kwa wakandarasi, mfumo maalum wa kidijitali ujulikanao kama Samia Infrastructure Portal umeanzishwa.

“Portal hii ni jukwaa la kidijitali linalowawezesha wakandarasi kuwasilisha maombi ya mikopo moja kwa moja mtandaoni. Hakuna tena haja ya wakandarasi kusafiri hadi ofisi za TARURA au benki, kwani maombi yao yanachakatwa kwa njia ya kielektroniki,” alifafanua.

Amesema mfumo huo unaongeza uwazi na ufanisi katika upatikanaji wa mikopo, ambapo baada ya uhakiki wa TARURA ngazi ya mkoa, maombi hayo hupelekwa moja kwa moja kwa CRDB kwa hatua za mwisho za kifedha.

Aidha, ameeleza kuwa kupitia mfumo huo, wakandarasi wanaweza kupata bidhaa mbalimbali za kifedha kama vile Bid Guarantee, Performance Guarantee, Advance Payment Guarantee, Retention Guarantee, Certificate Discounting na huduma mpya ya Bridge Financing inayowezesha upatikanaji wa mtaji wa haraka kabla ya malipo ya mkataba.

Katika hatua nyingine, CRDB imeamua kutoa mikopo hiyo bila ya dhamana kwa wakandarasi wanaolipa kwa wakati, huku ikitoza riba ya chini ya asilimia 15 kwa mwaka, hatua iliyotajwa kuwa suluhisho kwa changamoto za muda mrefu zinazowakabili wakandarasi wazawa.

“Tunatoa rai kwa wakandarasi wote nchini kutumia fursa hii. Kupitia Samia Infrastructure Bond, sekta ya ujenzi wa barabara inafunguliwa zaidi kwa wazawa na kukuza ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya miundombinu,” alisisitiza CPA Nyaulingo.

Amesema mpango huo unadhihirisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya Taifa, kuharakisha ujenzi wa barabara na kuongeza ajira kwa Watanzania kupitia miradi ya kimkakati.