Acha kubeba mzigo wa wivu (1)

Wivu  ni  kansa  ya  akili’’.  – B.C. Forbes 

Acha  wivu.  Wivu  hautajirishi.  Wivu  hauna  tuzo  ya aina  yoyote. Wivu  ni  kubeba  msalaba  mzito  usiokuhusu.  Mwandishi  B.C. Forbes  anasema: “Wivu  ni  kansa  ya  akili.”  Kama unataka  kufanikiwa katika maisha, acha wivu. 

Kama unataka kuishi maisha yenye amani, acha wivu.  Kama unataka kubarikiwa, acha wivu.  Mwenye wivu hana alama usoni.  Alama yake imo moyoni. Akiona mwenzake amefanikiwa anaumia sana. Anataka afanikiwe yeye peke yake. Anataka abarikiwe yeye peke yake. Anataka ale keki ya Mungu yeye peke yake. Anataka abaki kileleni yeye peke yake. Anataka apongezwe yeye peke yake.

Hauwezi kufanikiwa kwa kuwaombea wengine wasifanikiwe. Unafanikiwa kwa kuwaombea wengine wafanikiwe. Sala yako iwe: “Mungu naomba fulani afanikiwe,” siyo “Mungu naomba fulani asifanikiwe.”

Yafurahie mafanikio ya mwenzako kwa moyo wa shangwe na vigelegele. Mafanikio ya mwenzako ni mafanikio yako. Yafurahie. 

Mwenzako akifanikiwa mpongeze.  Ikiwezekana mnunulie zawadi ya kumpongeza.  Mtie moyo aendelee kufanya vizuri zaidi.  Mwambie: “Songa mbele.” Mwambie: “Mungu ana mpango mzuri na maisha yako. Usikate tamaa.”  Mtamkie Baraka. Fufua uwezo wa kuwapenda wenzako. 

Macho yako yafundishe kuona mazuri ya wenzako. Bubujikwa machozi ya furaha pale unaposikia habari njema za mwenzako. Tumeumbwa kuyafurahia mema/mazuri ya wenzetu na si kufurahia maanguko yao. Kama una tabia ya kufurahia maanguko ya wenzako, acha. Acha kuchekelea madhaifu ya mwenzako. Ahidi kuacha wivu  usio na tija kuanzia leo. Mungu anapokupa nafasi ya kuyajua madhaifu ya mtu mwingine kwa undani,  ni kwa  sababu  amekuamini.

Wainue wengine  juu nawe utainuliwa na uliowainua. Mwandishi wa Marekani, Zig  Ziglar anasema: “Utapata chochote unachotaka kwa kuwasaidia wengine kupata wanachohitaji.”

Umoja ni nguvu na  utengano ni udhaifu.  Kidole  kimoja hakivunji chawa.  Mwanasayansi Isaac Newton anasema: “Kama nimeona mbali zaidi ni kwa kusimama kwenye mabega ya watu wakubwa.” Ukitaka  kwenda  kwa kasi tembea peke yako.  Ukitaka  kufika mbali tembea  na watu wengine.

Mwandishi mmoja mwenye hekima  aliwahi kuandika: “Ukitaka furaha ya saa moja – lala. Ukitaka furaha ya siku moja – nenda kavue samaki.  Ukitaka furaha  ya  mwezi mmoja – oa au  olewa.  Ukitaka furaha  ya mwaka  mmoja – shinda bahati  nasibu. Ukitaka furaha ya maisha  yako yote – jitoe kwa  ajili ya wengine.” 

Kujitoa kwa ajili ya wengine ni kuwapenda. Ni kuwasaidia. Ni kuwasikiliza.  Ni kuwatetea. Ni  kuacha  kuwaonea  wivu.

Maisha unayoishi yanaitambulisha sura ya nani? Mwanafalsafa  Tolmons alipata kuandika hivi: “Katika maisha unaweza kuonyesha sura ya Mungu au sura ya shetani.”  Kazini kwako  unaweza kuonyesha sura ya shetani au sura Mungu.  Kwenye familia yako unaweza kuonyesha sura ya shetani au sura  ya  Mungu.  Kwa majirani zako unaweza kuonyesha sura ya shetani au sura ya Mungu.  Inategemea  maisha yako  unayoishi yanawakilishwa  na  matendo ya aina gani, kama ni matendo yasiyofaa, basi ni dhahiri kwamba unawakilisha sura ya shetani.

Tupembue tuone. Wivu ni sura ya shetani.  Umbeya  ni  sura  ya shetani.  Uongo  ni  sura ya shetani.  Uchoyo ni sura  ya  shetani.  Ufisadi ni sura ya shetani.  Rushwa ni sura ya shetani.  Uchu  wa madaraka ni sura ya shetani.  Sura  ya  Mungu ni sura ya uadilifu na uaminifu.  Sura ya Mungu  ni  sura ya upendo. Sura ya Mungu ni sura ya  amani.  Sura ya Mungu ni sura ya mshikamano.  Sura ya Mungu ni sura ya  unyenyekevu na huruma.

Ishi  na  watu  vizuri.  Ishi na  majirani  zako vizuri. Kumbuka: Unaishi na watu. Kuzaliwa kwako kumefanywa  na  watu.  Jina lako unalotumia  umepewa na watu.  Umepata elimu  kutoka kwa watu.  Kipato chako unachopata  kinatoka  kwa  watu.  Heshima uliyonayo  inatoka kwa watu.  Ulipozaliwa  uliogeshwa na watu. Wa mwisho kukuogesha watakuwa  watu. Mazishi  yako yatasimamiwa na watu. Utapelekwa makaburini na watu. Kila unachomiliki  kitarithiwa na watu. Ishi na watu vizuri.

Maisha  ni kama sarafu iliyotupwa angani.  Huwezi  kutabiri  itadondokea upande gani.  Mtu  unayemdhihaki leo na kumwona  kama  takataka,  inawezekana ndiye atakayeamua  hatima ya  maisha yako kesho. Mwanzoni  mwa mwaka 1980  meneja  wa hoteli  moja  ya kitalii huko  Hanzghou nchini China alimnyima kazi bilionea  Jack  Ma (kwa wakati huo  Jack Ma alikuwa hana utajiri wa aina  yoyote).  Baadaye Jack Ma alianzisha Kampuni ya Alibaba na kumwajiri mtu yule aliyemnyima kazi.  Maisha ni mzunguko. Ishi katika mzunguko wa kumheshimu kila mtu.