Nitoe mfano, ndugu yako amefariki dunia lakini ameacha shauri mahakamani ambalo alikuwa akidai kitu fulani kama haki yake. Yaweza kuwa alifungua kesi kudai ardhi, nyumba, mirathi, mgogoro wa kimkataba, fidia au madai  mengine yoyote. Kwa hiyo, tutatazama ni jambo gani unapaswa kulifanya ili kuendeleza kudai au kupata kile alichokuwa akidai marehemu.

Isemavyo sheria

Amri ya 22 kanuni ya 1 –  12  katika Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai ndiyo inayozungumzia jambo hili. Katika kanuni hizo si tu imezungumzwa haki ya marehemu (ambaye alikuwa mlalamikaji) bali pia haki ya marehemu mlalamikiwa au mdaiwa. 

Kanuni ya 1 inasema kuwa kifo cha mlalamikaji/mdai au mlalamikiwa/mdaiwa hakiui shauri ikiwa haki ya kulalamika bado haijafa.  

Maana yake ni kuwa kuna wakati mdai anakufa lakini haki yake ya kuendelea kudai alichokuwa akidai inaendelea kuishi na kuna wakati akifa anakufa na haki yake ya kudai. Ni wakati gani akifa anakufa na haki yake ya kudai na ni wakati gani akifa haki yake inaendelea kuishi, tutaona hapa chini.

Kuendelea kuishi/kufa kwa haki ya madai

Kuendelea  kuishi kwa haki ya madai maana yake ni kuwa ndugu wa marehemu, hasa msimamizi wa mirathi, anapata haki ya kuendeleza shauri na kudai kilekile ambacho marehemu alikuwa anadai. 

Na kufa kwa haki hiyo maana yake ni kuwa hakuna ndugu yeyote kutoka upande wa marehemu, akiwemo msimamizi wa mirathi, atakayekuwa na haki ya kudai au kuendeleza shauri ili kupata kile alichokuwa akidai marehemu. 

Hali ni hiyo hiyo kwa upande wa mlalamikiwa/mdaiwa aliyefariki dunia. Kwani kuna wakati ndugu watalazimika kurithi shauri ambalo alikuwa ameshitakiwa nalo na kuna wakati hawatalazimika.

Ili kujua kama ndugu waendeleze shauri au la,  kinachoangaliwa ni aina ya  shauri alilokuwa amefungua mdai kabla hajafariki dunia.

Ikiwa alifungua shauri binafsi (personal) au lenye viini vya ubinafsi (individuality), basi shauri hilo haliwezi kuendelezwa  na ndugu wa marehemu. 

Lakini kama shauri si binafsi, basi ndugu wataliendeleza na hatimaye kupata alichokuwa akidai marehemu.  Mashauri ambayo si binafsi ni kama kudai ardhi, nyumba, mirathi, madai yatokanayo na mikataba, na madai mengine ya kudai mali.

Kwa mashauri kama haya, ndugu wa marehemu wanaruhusiwa kuyaendeleza ili kupata alichotakiwa kupata marehemu.

Kuzuia kuendeleza madai

Hapo juu tumeona ndugu wa marehemu wakiruhusiwa kuendeleza madai na sasa hapa tunaona wanapozuiwa kuendeleza madai.  Tumesema hapo juu kuwa ikiwa mlalamikaji/mdai ambaye sasa ni marehemu alifungua shauri binafsi (personal) au  lenye viini vya  ubinafsi (individuality) basi ni wakati huo ambapo ndugu wa marehemu wanakosa haki ya kuendeleza shauri kama hilo. 

Mashauri binafsi au yenye viini vya ubinafsi ni kama mashauri ya fidia, labda kudai fidia baada ya kupigwa, kutukanwa, kudhalilishwa, kufunguliwa mashitaka ya hila, kusababisha kufungwa bila sababu za msingi na mashauri mengine yanayofanana na hayo. 

Mashauri ya namna hii hufa baada ya mdai kufa. 

Hayana uhai baada ya uhai wa mdai, hivyo ndugu hawawezi kuyaendeleza.

Hata hivyo, ikiwa shauri la namna hiyo lilikuwa limesikilizwa tayari na inasubiriwa hukumu halafu ndiyo mdai akafariki dunia,  basi hukumu itatolewa na ndugu wa marehemu watatakiwa kulipwa kile alichostahili kulipwa marehemu ikiwa ameshinda.

Pia ikiwa marehemu atakufa baada ya hukumu kutolewa na kabla ya utekelezaji (execution) hapo ndugu wataendeleza ili kupata kile alichostahili kupata marehemu.

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG. 

By Jamhuri