Katika sehemu iliyopita ya makala hii tuliona jinsi Gavana wa mwisho Mwingereza, Sir Richard Turnbull, alivyomsifia Mwalimu Nyerere baada ya kutembezwa sehemu mbalimbali nchini na kujionea maendeleo ambayo nchi ilikuwa imeyapata katika kipindi cha miaka kumi baada ya kupata Uhuru.

Sir Turnbull alitoa sifa hizo wakati wakiwa katika ziara mikoani, kama sehemu ya kumuonyesha jinsi nchi ilivyobadilika. Endelea…

Ilipofika siku yenyewe ya sherehe hapa Dar es Salaam palifanyika gwaride kubwa na michezo ya halaiki ambayo wale wakoloni hawakupata kuona kabla yake. Michezo ya halaiki ilifundishwa na Wakorea. 

Yule Gavana Sir Richard aliyeshuhudia bendera ya mkoloni ikiteremshwa na bendera ya Tanganyika ikipandishwa, sasa alishuhudia vimbwangwa vya wananchi huru.

Baada tu ya maonyesho yale ya kufana sana, Baba wa Taifa alitoa hotuba yenye majumlisho ya kilichofanyika nchini katika kipindi cha miaka 10 ya Uhuru wetu, kama vile pale Mwanza Rais Mugufuli alivyo tuelezea maendeleo yetu katika miaka 58 ya Uhuru wetu.   

Kwa upande wa utawla (civil service) Mwalimu alisema: “Mwezi Aprili 1960, Waafrika maofisa wafawidhi (Senior posts) walikuwa 346 tu, lakini wakati wa Uhuru Desemba 1961 Waafrika walioshika nyadhifa za juu sasa walifikia watu 1,170 kati ya nafasi 3,282 zilizokuwepo.”

Upande wa elimu, Mwalimu alisema: “Wakati wa Uhuru tulikuwa na watoto 11,832 katika shule zote za sekondari hapa Tanganyika. Tulikuwa na watoto 176 tu katika kidato cha sita. Kumbe mwaka ule 1971 (miaka 10 tu baada ya Uhuru) walikuwepo watoto 31,662 katika shule zote za sekondari mpaka kidato cha nne na walikuwepo watoto 1,488 katika kidato cha sita ukilinganisha na watoto 176 mwaka ule wa Uhuru 1961.”

Kwa upande wa elimu ya juu alibainisha: “Mwaka 1961 walikuwepo watoto 194 katika vyuo vikuu mbalimbali Afrika Mashariki, na watoto 1,312 katika vyuo vikuu ughaibuni (Ulaya, Marekani, China nk). Ilipofika mwaka 1971, miaka 10 tu baada ya Uhuru, watoto wasomi katika vyuo vikuu vya Afrika Mashariki walikuwapo 2,028, na vyuo vikuu huko ughaibuni walikuwa 1,347.”

Kwa elimu ya msingi hotuba ya Baba wa Taifa 1971 ilisema hivi: “Kumekuwa na ongezeko kubwa kwa upande wa elimu ya msingi katika muda wa miaka hii 10 ya kujitawala kwetu. Wakati mwaka 1961 zilikuwepo shule za msingi 3,100 zenye jumla ya watoto 486,000 mwaka 1971 tumekuwa na shule za msingi 4,705 zenye jumla ya watoto 848,000.”

Kwa upande wa tiba, Mwalimu alisema: “Wakati mwaka 1961 walikuwepo madaktari 12 Watanganyika, mwaka 1970 walifikia idadi ya madaktari 123. Kumekuwa na ongezeko kubwa la wahudumu wa cheo cha Medical Assistants na Rural Medical Aids. Mwaka 1961 vilikuwepo vyuo vya kufunza hao wahudumu vikitupatia watu 74 kwa mwaka sasa mwaka 1971 vyuo namna ile viliongezeka na kufikia tisa vyenye uwezo wa kutoa wahudumu 270. Shule za manesi zilikuwa 14 zikifunza manesi 235 hivi, hapa Tanganyika mwaka 1961 lakini mwaka 1971 tulikuwa na shule 22 zenye kufunza manesi 422.”

Kwa upande wa barabara Baba wa Taifa alisema: “Kwa mwaka ule wa 1961 tulikuwa na barabara za lami (bituminized major roads) zenye urefu wa maili 660 tu katika nchi nzima na barabara za changarawe (engineered gravel major roads) zenye urefu wa maili 310 tu, barabara nyingine zote katika nchi hii zilikuwa za udongo zenye urefu wa maili 8,026.”

Sasa miaka 10 tu ya Uhuru wetu. Mwalimu aliwaelezea wakoloni wale kuwa tunazo barabara za lami zenye urefu wa maili 1,550 na barabara za changarawe zenye urefu wa maili 595 wakati barabara za udongo ni zenye urefu wa maili 8,405, hivyo kufanya jumla ya maboresho ya miundobinu ya barabara nchini kufikia urefu wa maili 105,500.

Mwaka jana kule Mwanza Rais Magufuli alikwenda mbali zaidi ya Mwalimu. Wakati mwaka 1961 Mwalimu baada ya kulihutubia taifa hakuwakaribisha wakoloni wale angalau wawaamkie wananchi. Lakini kule Mwanza, Rais Magufuli aliwakaribisha viongozi waliomtangulia wote watoe neno mbele ya umati ule. Zaidi ya hilo aliwakaribisha pia na viongozi wakuu wa vyama vya upinzani kuwaamkia wananchi wale. Kila kiongozi aliyepata fursa ile alikuwa na la kutamka. 

Hapo ndipo ninajiuliza, Watanzania wale wanaosema sema “hakuna lolote lililofanyika tangu tupate Uhuru”, maneno yao haya ni kweli hawayaoni haya maendeleo au tu hawataki kuyaona?

Kwanini wanakuwa kama yule Mtume Tomaso, kutokutaka kuamini mpaka pale wanapodhihirishiwa? Je, hizi ndege zetu nane za ATCL hawazioni? Hii reli ya kisasa SGR hawaioni? Umeme wa REA vijijini nao hawauoni? Hizi hospitali mpya hawazioni wala mabarabara ya lami hawayaoni? Huo tuite ni upofu wa kujitakia. 

Serikali imeweka wazi miradi yote na kutaja gharama za kila mradi na kusema unalipiwa kwa fedha zetu wenyewe kutokana na kodi zinazolipwa. Rais anatueleza Watanzania kuwa tutembee vifua mbele, maana sisi si maskini. Nchi yetu hii ni tajiri sana.

Kitu kimoja muhimu sana na cha kukumbukwa daima alichokifanya Mwalimu mara tu baada ya Uhuru ni kulinda hadhi ya utu wa Mtanganyika mweusi. Hili alilisema wazi namna hii: “The most immediate task after independence, however, was the assertion of the dignity of all Tanganyika citizens.” (Kati ya majukumu makubwa ya kwanza baada ya Uhuru ni kusisitiza hadhi na utu wa Watanganyika wote). 

Jukumu kubwa la kwanza kuonyesha kuwa hakuwa anatania katika hili, aliwatimua Wazungu watano hivi siku chache tu baada ya Uhuru, pale Wazungu wale kwa mazoea yao walipowadhalilisha Waafrika baada tu ya Uhuru. 

Kule kuwafukuza kutoka hapa nchini kuliwafanya Wazungu watambue kuwa Uhuru wa Tanganyika haukuwa wa bendera tu, bali ulikuwa umewapatia wazawa haki ya kuwa kama binadamu wengine wote (tazama; Nyerere Uhuru Na Maendeleo uk. 269 ibara ile ya 2). Kwa uamuzi ule Mwalimu atakumbukwa sana kama muumini wa usawa wa binadamu wote duniani.

Basi kwa mwendo huu wa Serikali ya Awamu ya Tano, kujenga taifa la uchumi wa kati na kuelekea kwenye kujitegemea “per se”, hadhi ya Mtanzania itapaa zaidi. Tutaheshimika na tutathaminiwa kama moja ya mataifa mashuhuri Afrika na ulimwenguni kote.

Hapo basi, tunapaswa kutembea vifua mbele. Sisi si maskini. Ombaomba ni kudhalilisha utaifa tu. Msingi aliojenga Mwalimu, Rais Magufuli anaendelea kuuimarisha zaidi. Tusitazame nyuma tusije tukageuka mawe. 

Mungu ibariki Tanzania.

Mbenna ni Brigedia Jenerali mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

82 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!