Uislamu unahimiza ‘wasatwiyya’ (1)

‘Wasatwiyya’ ni neno la Kiarabu linalotokana na maneno ‘Wastwu’ na ‘Wasatwu’. Neno ‘Wastwu’lina maana ya kAatikati na neno ‘Wasatwu’ lina maana ya ubora. Kiujumla, neno ‘Wasatwiyya’ linapata maana ya wastani, usawa, katikati na ubora. 

Katika Falsafa na Usufi, ‘Wasatwiyya’ ni ule mrengo wa katikati. Katika Uislamu ‘Wasatwiyya’ ni lile jambo bora na ndilo jambo lililo sawa na jepesi kutekelezwa. Neno wastani na ubora yanakurubiana.

Uislamu unahimiza ‘Wasatwiyya’ katika kila jambo, kwa kuwa hata dini yenyewe ni dini ya ‘Wasatwiyya’; ‘dini ya wastani’; dini ya katikati. Nilifafanue hili. Uislamu ni dini ya ‘Wasatwiyya’ kwa kuwa kiitikadi unamwepekesha Mwenyezi Mungu, Mwenye haki ya kuabudiwa, Mmoja Pekee, Asiye na Mshirika. 

Itikadi hii ni iliyo katikati ya itikadi ya kukana uwepo wa Mwenyezi Mungu (Ulahidi) na ile itikadi ya kumshirikisha Mwenyezi Mungu na miungu wengine (Ushirikina). Uislamu ni Dini ya Wasatwiyya kwa kuwa kwa upande wa maadili si dini ya kimaada tu wala si dini ya  kiroho tu, bali ni dini inayokusanya pande zote mbili za kimaada na kiroho, kwa sharti la kulingana sawa na kukamilika. Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) anasema: “Bora ya mambo ni wastani.”

Umma wa Kiislamu pia umeelezwa kuwa ni umma ulio katika ‘Wasatwiyya.’ Tunasoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya Pili (Surat Al-Baqarah), Aya ya 143 kuwa: “Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe umma wa wastani ili muwe mashahidi juu ya watu, na Mtume awe ni shahidi juu yenu.”

Nitoe mifano michache ya ‘Wasatwiyya’ katika Uislamu.

Uislamu umeweka ‘Wasatwiyya’ katika sheria na mfano wa wazi kabisa ni kuweka mazingira ya kutekelezwa sheria pale inapowekwa. Kwa mfano, ulevi wa pombe haukukatazwa kwa katazo la mara moja kutokana na tabia ya ulevi kushamiri katika jamii. Hivyo palijengwa mazingira ya kuikataza kidogo kidogo; hatua kwa hatua.

Hatua ya kwanza ilikuwa kueleza faida na hasara za ulevi na kamari na kuonyesha kuwa pamoja na faida/manufaa yanayopatikana katika pombe na kamari, kwa hakika hasara ni kubwa kuliko faida. Tunasoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya Pili (Surat Al-Baqarah), Aya ya 219 kuwa: “Wanakuuliza juu ya ulevi na kamari. Sema: Katika hivyo zipo dhambi kubwa na manufaa kwa watu. Lakini dhambi zake ni kubwa zaidi kuliko manufaa yake.”

Hatua ya pili ilikuwa ni kujenga mazingira ya kupunguza kiwango cha unywaji wa pombe kwa kumzuia mtu asiswali akiwa amelewa mpaka awe anajua kila anachokisema. Ieleweke kuwa dhambi za kuacha kuswali ni kubwa sana na wakati huo huo haruhusiwi kuswali huku amelewa isipokuwa pale atakapokuwa anajua kile anachokisema. Tunasoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya Nne (Surat An-Nisaai), Aya ya 43 kuwa: “Enyi mlioamini! Msikaribie Swala, hali mmelewa, mpaka myajue mnayoyasema…”

Mpaka kufikia hapa, tayari mazingira ya ulevi wa pombe yalikuwa magumu kwa mwenye kutekeleza ibada na ndipo amri ya kuzuia pombe na kamari ilipotolewa. Tunasoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya Tano (Surat Al-Maaida), Aya ya 90 kuwa: “Enyi mlio amini! Bila ya shaka ulevi, na kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya Shetwani. Basi jiepusheni navyo ili mpate kufanikiwa.”

Pia ikaelezwa hasara ya kijamii inayopatikana kutokana na matumizi ya ulevi na kucheza kamari. Tunasoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya Tano (Surat Al-Maaida), Aya ya 91 kuwa: “Hakika Shetwani anataka kutia kati yenu uadui na chuki kwa ulevi na kamari, na akuzuieni kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kusali. Basi je, mmeacha?”

Utaona ‘Wasatwiyya’ unapoona namna Uislamu ulivyojenga mazingira wezeshi ya utekelezaji wa sheria.

Na Uislamu kupitia Qur’aan Tukufu umeonyesha pia pale jambo lililozoeleka au hitaji la kibinadamu linapozuia kwa amri ya mara moja athari yake ni sehemu kubwa ya watu kuivunja ile sheria na wakati mwingine si kwa ujeuri na kiburi bali kuhemewa na ugumu wa kuitekeleza ile sheria. Nitoe mfano.

Mwanzoni mwa Uislamu ilikuwa mtu akishafuturu baada ya kufunga (swaumu) anapewa muda maalumu kati ya magharibi na kuswali Swala ya Ishaa autumie kwa ajili ya kula, kunywa na ‘kunong’ona’ na mkewe au mumewe. 

Akiswali Ishaa au kulala kabla ya kuswali Ishaa, basi hana ruhusa ya kula, kunywa wala ‘kunong’ona’ na mkewe au mumewe hadi magharibi ya siku ya pili kwa utaratibu huohuo. Jambo hili lilileta mashaka makubwa na wapo walioteleza. Kwa kuwa Uislamu ni Dini ya ‘Wasatwiyya’, Mwenyezi Mungu aliwaonea huruma waja wake wanaoteseka na akawafanyia wepesi kwa kuondoa sheria hii ambayo utekelezaji wake ulikuwa ni mgumu na wenye shaka.

Tunasoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya Pili (Surat Al-Baqarah), Aya ya 187 kuwa: “Mmehalalishiwa usiku wa Saumu kuingiliana na wake zenu. Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao. Mwenyezi Mungu anajua kwamba mlikuwa mkizikhini nafsi zenu. Kwa hivyo amekukubalieni toba yenu na amekusameheni. Basi sasa changanyikeni nao na takeni aliyokuandikieni Mwenyezi Mungu. Na kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni Swaumu mpaka usiku. Wala msichanganyike nao, na hali mnakaa Itikafu msikitini. Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi msiikaribie. Namna hivi Mwenyezi Mungu anabainisha Ishara zake kwa watu ili wapate kumcha.”

Nilipokuwa nazingatia mazingira (scenario) hii ya ugumu wa utekelezaji wa sheria hususan inayoigusa jamii moja kwa moja nikakumbuka namna ya wanaume wengi Waislamu nchini Tanzania wanavyovunja kipengele cha talaka kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971.

Wakati kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 “Talaka ni ruhusa au amri ya mahakama ya kisheria ambayo mume au mke hupewa wakati anapomwacha mwenzake”, kwa mujibu wa Uislamu, Talaka ni “kuuvunja mkataba wa ndoa kwa neno la kutaliki au mfano wake.”

Hivyo utaona kuwa hata fasili ya neno talaka kwenye Uislamu na Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 ni tofauti. Uislamu umempa haki mwanamume kuvunja ndoa kwa kutamka neno ‘Talaka’ au mfano wake. Akifanya hivyo mke ameachika na itabaki tu kuangalia aina ya talaka kwa mujibu ya Sheria ya Kiislamu.

Kwa upande wa Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 mwanamume hana mamlaka hayo aliyopewa na Uislamu kwa mujibu wa Kifungu kifuatacho: “Chombo chenye mamlaka ya kutoa talaka ni Mahakama tu. Mahakama hiyo itatoa kwa ndoa ambayo imedumu kwa muda wa miaka miwili au zaidi. Mahakama inaweza kutoa talaka kwa ndoa ambayo haijafikisha muda huo endapo mlalamikaji atatoa sababu za msingi mahakamani.”

Unapokiangalia kipengele hiki cha Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 utaona kimekwenda kinyume kabisa na Sheria ya Ndoa ya Kiislaam ingawa Sheria yenyewe imetambua haki ya ndoa ya Kiislamu kufuata mafundisho ya dini husika.

Nihitimishe ngwe ya leo kwa kuweka wazi kuwa sehemu kubwa ya wanandoa waislamu nchini Tanzania wamekuwa wakivunja kipengele hiki cha kuwa talaka sharti itolewe na Mahakama kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971.

Utakuta wanandoa Waislamu wameoana kisha wakaachana kwa mujibu wa talaka ya Kiislamu na mwanamke huyo baada ya eda akaolewa na mwanamume mwingine ilhali Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 inamhesabu ni mke wa mume yule wa kwanza.

Kinyume chake ni kuwa kuna ndoa nyingi hivi sasa zinavunjwa mahakamani tena wakati mwingine kwa msaada wa viongozi wa dini wasio waaminifu au walioweka mbele masilahi binafsi ilhali kwa mujibu wa Sheria ya Uislamu bado ni ndoa halali. 

Kwa viongozi wa dini wa aina hii niwanasihi kutenda haki na kuepuka dhuluma za aina hiyo na warejee Qur’aan Tukufu Sura ya Pili (Surat Al-Baqarah), Aya ya 281 Mwenyezi Mungu akituonya: “Na iogopeni siku ambayo mtarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, kisha kila nafsi italipwa ilichochuma. Nao hawatadhulumiwa.”

Mifano hii ya talaka inawakilisha mifano mingi ya ndoa zilizovunjika kidini (Kiislamu) lakini zikawa hai kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 lakini wanandoa hao wakiwa kila mmoja na hamsini zake na kinyume chake.

Ni vema viongozi wa dini, wanasheria na serikali wakakaa pamoja na kuiangalia changamoto hii ambayo inawatesa wengi na kuwaingiza katika kuvunja sheria ya nchi huku wakiwa wametekeleza Sheria ya Dini.

Haya tukutane Jumanne ijayo In-Shaa-Allaah.

Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).

Simu: 0713603050/0754603050