Na Magrethy Katengu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimesema kitendo cha Wizara Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa inavinja Sheria.

Hayo yamesemwa Juni 12, 2024 na Katibu Mkuu wa Chama hicho Ado Shaibu akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na barua waliopokea jana kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa wakijulishwa kuwa TAMISEMI inaendelea na maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kwamba Juni 15, 2024 itafanya kikao cha wadau kukusanya maoni ya rasimu ya kanuni zitakazosimamia uchaguzi huo.

Hivyo amesema kwamba wamesikitishwa na hatua hiyo ya TAMISEMI kwa sababu ni kinyume na Sheria na inavunja kabisa misingi ya falsafa ya 4R ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwamba kwa mujibu wa kifungu cha 10(1)(c) cha Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi ya Mwaka 2024, Tume Huru ya Uchaguzi imepewa jukumu la kusimamia uchaguzi wa mitaa, vijiji na vitongoji.

“Msimamo wa muda mrefu wa Chama chetu ni kuwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa usimamiwe na Tume Huru ya Uchaguzi badala ya TAMISEMI ndiyo maana ACT Wazalendo tulishiriki kikamilifu kuhakikisha kuwa Bunge linapitisha kifungu cha Sheria kuwezesha jambo hilo,” amesema Shaibu na kuongeza,

“Ni jambo la kusikitisha kuwa Serikali hadi leo inasuasua kupeleka muswada Bungeni kutekeleza matakwa haya ya Sheria na badala yake inataka kuvunja Sheria kwa kuipa madaraka TAMISEMI kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa,”.

Ameongeza, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Namba 1 ya Mwaka 2024 imefuta kwa pamoja (consequencial amendment) Sheria ya Taifa ya Uchaguzi ya Mwaka 1985 na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa ya Mwaka 1979.

Hivyo, hatua yoyote inayochukuliwa na TAMISEMI hivi sasa kuhusiana na usimamizi wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni batili na ni kinyume na sheria.

Akieleza kuhusu msimamo wa ACT Wazalendo, ameeleza watakwenda kwenye kikao cha wadau kilichoitishwa Juni 15, 2024 Dodoma kuieleza TAMISEMI isimamishe mara moja michakato inayoendelea nao wa maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa sababu ni batili na unavunja sheria za nchi.

Kwamba ACT Wazalendo wamewasiliana na Asasi za Kiraia juu ya umuhimu wa kufungua kesi Mahakamani kuzuia hatua za maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa zinazoendelea kuchukuliwa na TAMISEMI.

“Tumefarijika kuwa Asasi hizo zipo kwenye hatua za mwisho kufungua kesi hiyo. ACT Wazalendo itatoa ushirikiano kwa taasisi hizo kwenye kesi hiyo,’ ameongeza Shaibu.

Pia, amebainisha kuwa kufuatia hali inayoendelea na kutokana na unyeti wa jambo lenyewe, wataandaa kikao maalum na kuvialika vyama vingine vya siasa kuweka msimamo wa pamoja juu ya kuizuia TAMISEMI kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa na pia kuteuliwa wajumbe wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi ili wachukue nafasi ya waliopo sasa kwa mujibu wa sheria, ambao ndio waliovuruga uchaguzi wa 2020.

kwamba hatua hii ya TAMISEMI kupora madaraka ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kinyume na sheria za uchaguzi, kwamba inatia doa kubwa falsafa ya 4R ya Mh. Rais Samia Suluhu na inapaswa kupingwa na wadau wote wa demokrasia nchini Tanzania