Ni wazi kuwa siku za kundi la waasi la Allied Democratic Forces (ADF) linaloshutumiwa kwa kuwaua wanajeshi 14 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), sasa zinahesabika.

Kundi hilo lipo DRC na Uganda, na limekuwa likiendesha mauaji kwa wananchi na kwa askari wa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa nchini DRC.

Habari kutoka ndani ya JWTZ zinasema kuwa makamanda na wapiganaji wameingiwa hasira baada ya wenzao kuuawa, na sasa wamenuia kuisambaratisha ADF kama walivyolifanya kundi la March 23 (M23).

Kutokana na mauaji hayo ya wiki iliyopita, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, na majenerali watatu wa ngazi za juu katika JWTZ tayari wamewasili DRC kujionea hali ilivyo na kupanga mikakati ya kujibu mapigo dhidi ya waasi hao haraka iwezekanavyo.

Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo, katika mahojiano maalumu na JAMHURI, amesema Jeshi liko imara wakati wote na kwamba litaongeza nguvu zaidi nchini DRC. Amewataka waasi sasa wafikirie kufanya kazi nyingine.

“Kwanza nikushukuru kwa kunitafuta na nikiri kwamba nimefarijika sana kupata hata mawazo ya watu mbalimbali kupitia kwenu, lakini masuala ya kimapigano yana mambo mengi, mazingira yenyewe ya kimapigano na watu mnaopambana nayo yanahitaji mkakati wa kipekee.

“Mnaposhambuliwa na mkajaribu kutathimi mashambulizi yenyewe yanawapa mwelekeo wa kujipanga vizuri zaidi na kupoteza vijana wetu tunasikitika sana kwamba imetokea hivyo na hayakuwa matarajio yetu na si matakwa yetu. Hawa vijana wamefunzwa vizuri na walikuwa na umahiri wa kupigana.

“Kila mapambano yanapojitokeza huwa mara nyingine mazingira ndiyo huamua hali inayojitokeza, tuko katika hali ya kuchunguza zaidi ni namna gani mashambulizi hayo yalitokea na tutajipanga vzuri zaidi kwamba mashambulizi ya namna hiyo hayatokei tena.

“Ninajua kwamba wale waliopata majeraha sasa hawawezi kupigana tena, wanaendelea kutibiwa nchini DRC pamoja na maeneo mengine kwa mujibu wa taratibu za Umoja wa Mataifa.”

JAMHURI limemuuliza kama vifo vilivyosababishwa na waasi hao vinaweza kuwa sababu ya Tanzania kuondoa wanajeshi wake DRC. Katika majibu yake, Jenerali Mabeyo amesema: “Kujitoa kwa sababu gani? Hatuwezi kujitoa, tunachofanya ni kujipanga vizuri zaidi kuwakabili. Kujitoa haina maana.”

Akizungumza kuhusu namna ya kujipanga kivita zaidi, Jenerali Mabeyo amesema tayari makamanda wake watatu, Mkuu wa Jeshi la Nchi Kavu, Meja Jenerali Sharif Sheikh Othman, Mkuu wa Operesheni na Utendaji Kivita, Brigedia Jenerali Alfred Kapinga, Mkuu wa Usalama na Utambuzi, Brigedia Jenerali Nicodem Mwangela, na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Mwinyi wameenda DRC.

“Waziri amekwenda kuwapa pole wapiganaji, lakini makamanda wako kule kwenda kufanya tathmini na ninaamini kwamba yatakayoletwa yatatusaidia kujipanga vizuri zaidi,” amesema.

Jenerali Mabeyo amesema JWTZ itaongeza nguvu zaidi nchini DRC kwa mujibu wa taratibu za Umoja wa Mataifa.

Baada ya kuuawa wapiganaji wa JWTZ kumekuwepo na maombi kadhaa ya Tanzania kurudishiwa ukuu wa Kamandi ya Monusco, ambayo mwaka 2013 ilikuwa chini ya Luteni Jenerali James Mwakibolwa, ambaye sasa ni Mnadhimu wa JWTZ, katika kipindi chake aliwashikisha adabu waasi wa M23. Wakati huo alikuwa na cheo cha Brigedia Jenerali.

Akijibu hoja hiyo Jenerali Mabeyo ameliambia JAMHURI; “Nashukuru, nimesikia…tutayafanyia kazi.”

Amiri Jeshi Mkuu Rais John Magufuli amesema amepokea kwa mshituko na masikitiko makubwa taarifa za kuuawa kwa askari 14 wa JWTZ waliopo katika operesheni ya ulinzi wa amani DRC. Wanajeshi 44 wamejeruhiwa na wengine wawili hadi mwishoni mwa wiki walikuwa hawajulikani waliko.

Kutokana na vifo hivyo, Rais Magufuli ametuma salama za rambirambi kwa Dk. Mwinyi, Jenerali Mabeyo, maafisa na askari wa JWTZ, familia za marehemu na Watanzania wote kwa kuwapoteza mashujaa waliokuwa wakitekeleza wajibu wao.

“Nimeshitushwa na kusikitishwa sana na vifo vya vijana wetu, askari shupavu na mashujaa waliopoteza maisha wakiwa katika majukumu ya kulinda amani kwa majirani zetu DRC,” amesema Rais.

Awali, Umoja wa Mataifa ulithibitisha taarifa za kuuawa kwa wanajeshi 14 wa muungano huo baada ya kambi yao kuvamiwa mashariki mwa DRC. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alishutumu vikali shambulio hilo na kusema ni sawa na uhalifu wa kivita.

Guterres ameitaka DRC kufanya uchunguzi kuhusu shambulio hilo na kusema waliohusika wanapaswa kuwajibishwa. Wanajeshi zaidi wametumwa eneo hilo na kamanda wa kikosi cha kulinda amani anaelekeza shughuli ya kuwaondoa majeruhi.

Guterres amesema shambulio hilo ndilo mbaya zaidi kuwahi kutekelezwa dhidi ya walinda amani wa UN katika historia yake miaka ya karibuni.

“Ningependa kueleza kusikitishwa kwangu na shambulio hilo lililotekelezwa dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, tunafahamu pia kwamba wanajeshi watano wa jeshi la DRC waliuawa.

Gazeti la JAMHURI limezungumza na Waziri wa Ulinzi, Dk. Mwinyi, lakini amesema hawezi kuzungumzia chochote kuhusu mauaji ya askari hao, badala yake akasema JWTZ watatoa tamko.

“Naomba usubiri tamko kutoka JWTZ maana tumeelewana kuwa tutatoa tamko moja ambalo litakuwa kwa maandishi, hicho unachouliza na unachotaka kufahamu majibu yake yote utayapata huko, kwangu itakuwa vigumu,” amesema Dk. Mwinyi.

Oktoba, mwaka huu askari wapiganaji wawili wa JWTZ, Koplo Maselino Fubusi na Praiveti Venance Chimboni waliuawa nchini DRC. Askari hao walikuwa kwenye operesheni ya ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa. Askari walijeruhiwa katika shambulio lililofanywa na kundi la wapiganaji la ADF.

Taarifa ya Kurugenzi ya Habari na Uhusiano ya JWTZ ilisema askari hao walishambuliwa kwa kupigwa risasi na kundi la waasi Oktoba 9, wakiwa umbali wa kilomita 24 mashariki mwa mji wa Beni.

Guterres alilaani mauaji hayo yaliyofanywa na wapiganaji wa ADF wenye asili ya Uganda.

Please follow and like us:
Pin Share