DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Msanii, mtunzi na mwongoza filamu, Leah Mwendamseke, maarufu kama Lamata, amesema uhalisia uliomo ndani ya tamthilia yake ya ‘Jua Kali’ ndiyo sababu ya kugusa mioyo ya watazamaji wengi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Lamata amesema asilimia kubwa ya stori hiyo ni maisha halisi ya kila siku ya jamii, hasa ya Kitanzania.

“Jua Kali ni moja ya kazi nilizozifanyia utafiti wa kina na kwa muda mrefu ndiyo maana inaelezea maisha ya kawaida kama umaskini, ndoa, ugumu wa maisha, vita ndani ya familia, mapenzi, uhusiano, ni vitu kama hivyo vinavyotugusa,” anasema Lamata.

Anasema ni utafiti huo ndio uliompa wazo la kutunga tamthiliya ya Jua Kali.

Akizungumzia changamoto anazokumbana nazo kama mwongoza filamu hasa kuwaelekeza wasanii nini cha kufanya waweze kufikisha ujumbe mahususi kwa jamii, anasema:

“Ni nyingi sana, hasa pale unapoangalia namna ya kuifanya stori iuvae uhusika halisi unalazimika kutumia muda mrefu. Na ukiangalia wahusika wenyewe ni wasanii wakubwa, lazima upate changamoto.

“Mimi ninapokuwa kazini huwa sipendi mchezo wala masihara hata kidogo. Ni lazima kutumia akili sana ili kazi iwe nzuri na kuigusa jamii.

“Huwa nina hakikisha ninatafuta watu watakaocheza uhalisia kama inavyotakiwa. Huwa ninakuwa makini na mkali sana kuhakikisha mtu anavaa uhusika vizuri hata kama ni kwa kumfundisha.

“Siwezi kupitisha kipengele kama bado sijaridhishwa nacho. Nikiridhishwa na kazi ndipo napitisha ili kuhakikisha kazi inakuwa nzuri na yenye kupendwa na watu,” anasema.

Kuhusu mmoja wa wahusika katika tamthiliya hiyo anayefahamika kama Tuma, Lamara anasema:

“Historia ya Tuma ni ya kweli ya maisha yake ndiyo maana ameweza kuuvaa uhusika vizuri sana. Kwa asilimia 70 ni maisha yake na asilimia 30 ni uandishi (ubunifu). Hii ndiyo maana amefanikiwa kuuvaa uhusika kwa kama asilimia 90 hivi.”

Lamata,

By Jamhuri