Na Joe Beda Rupia

Luteni Jenerali Tumainiel Kiwelu ni mmoja wa viongozi watakaokumbukwa daima katika Mkoa wa Rukwa, hasa mjini Sumbawanga. Ndiyo, Jenerali Kiwelu. Hakika ameacha alama zisizofutika.

Ninashindwa nianzie wapi katika kumuelezea mwamba huyo wa Vita ya Kagera. Anyway, ngoja nianzie popote.

Kiwelu, mwanajeshi haswa, mwamba, jeuri lakini makini kweli kweli aliyeongoza Operesheni Chakaza (awamu ya awali), yaani kuyaondoa majeshi ya uvamizi ya Idi Amini katika ardhi ya Tanzania wakati wa Vita ya Kagera, aliteuliwa na Baba wa Taifa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa mwaka 1984 wakati huo akiwa na cheo cha Meja Jenerali.

Wakati wa Vita ya Kagera alikuwa Brigedia.

Naam, nikiri kwamba wakati huo nilikuwa bado nipo shule ya msingi; yaani mtoto mdogo, lakini sifa za watu kama akina Kiwelu, Mayunga, Musuguli, John Warden, Kitete, Kimario tulishazisikia sana na mimi nilikuwa shabiki mkubwa wa hawa jamaa; mashujaa wa Tanzania wanaopaswa kuingia kwenye vitabu vya historia.

Jenerali Kiwelu alihamishiwa Rukwa akitokea Tanga. Akatua Sumbawanga kwa kishindo. Wanaomfahamu wanasema hakuwa mzungumzaji sana. Lakini alitisha. Naam, aliitikisa Sumbawanga na vishindo vyake vilitufikia hata sisi watoto wa shule za msingi wilayani Mpanda.

Wafanyakazi wazembe ndio walioipata freshi, kwa kuwa Kiwelu alikuwa akienda kwenye ofisi zao asubuhi kabisa muda wa kufungua ofisi, asipomkuta bosi au mkuu wa idara, anaondoka na kiti chake!

Kasheshe ni kukifuata kiti hicho ofisini kwa Kiwelu. Nasikia kuna watu waliamua kuchonga viti vingine badala ya kwenda kuchukua kiti kilichobebwa na mkuu wa mkoa.

Wakati hayo yakiendelea na nidhamu kazini ikirejeshwa kwa kasi ya ajabu, Jenerali Kiwelu akatembelea Mpanda kwa ziara ya kikazi. Ni hapo ndipo nilipomuona kwa mara ya kwanza.

Ziara hiyo iliingia dosari wakati akiwa Inyonga. Taarifa zikaenea kwamba Polisi Jeshi (MP) kutoka Makao Makuu wamemchukua Kiwelu na kumpeleka Dar es Salaam baada ya kutajwa kwenye kesi ya uhaini!

Simanzi na hofu ikaugubika Mkoa wa Rukwa. Kwamba kiongozi wao sasa anahusishwa na uhaini na huenda asirejee tena kuendelea kulisukuma gurudumu la maendeleo la mkoa huu ambao wakati huo ulikuwa nyuma sana.

Wadadisi wa mambo tukaendelea kufuatilia nini kitakachompata Kiwelu. Kama wiki mbili hivi baadaye, akarejea Inyonga kuendelea na ziara yake. Tukapumua. Kwamba mwamba wetu ameruka kihunzi cha kuhusishwa na uhaini. Hatari sana. Mashabiki wake tukafurahi.

Tukaambiwa hata mahakamani hakufikishwa, ila aliandika maelezo tu.

Jenerali Kiwelu alihamishiwa Rukwa wakati tayari mkoa huu umetajwa kuwa mwenyeji wa sherehe za Sikukuu ya Wakulima, maarufu kama Sabasaba za mwaka 1985. Wakati huo Sabasaba ni sabasaba kweli! Inazunguka mkoa mmoja hadi mwingine.

Kuwa mwenyeji wa sherehe kubwa kama hizo ambazo mgeni rasmi huwa ni mzee mzima mwenyewe, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kulihitaji maandalizi ya kutosha. Si mchezo.

Jenerali Kiwelu anafika Sumbawanga, anataka kujua kinachoendelea katika maandalizi ya Sabasaba. Hakuna. Wenyeji wake wakamuonyesha eneo wanalotaka kujenga uwanja kwa ajili ya sababasa.

Eneo la wazi. Limezagaa mapipa ya lami. Kati ya uwanja wa maonyesho na Mazwi. Mbele ya Idara ya Maji na Ujenzi. Hata msingi haujachimbwa! Kiwelu akashangaa.

Mara moja akaamuru eneo liandaliwe na ujenzi uanze, tena ufanywe kwa haraka ndani ya miezi tisa ukamilike na uwanja huo utumike kwa ajili ya sherehe za Sabasaba.

Watu wakadhani masihara. Jenerali akaingia kazini. Mchakamchaka ulioanza hakuna atakayeusahau. Kila mtu, awe ni mkulima, mfanyakazi au mfanyabiashara kabla ya kwenda kwenye shughuli zake, alitakiwa kwenda eneo la tukio na kusogeza walau tofali moja kwa fundi.

Magari yote makubwa kabla ya kuanza kazi za kila siku, kwanza yalitakiwa kupiga tripu moja ya mchanga au mawe pale ‘site’. Vibarua wakachukuliwa kutoka maeneo mbalimbali ikiwamo makazi ya wakimbizi ya Katumba wilayani Mpanda.

Amini usiamini, Julai 7, 1985, Mwalimu Nyerere anafika Sumbawanga kwa ajili ya Sabasaba, tayari uwanja umekamilika na kupewa jina la ‘Julius Kambarage Nyerere Stadium’! Mwenyewe akashangaa.

Katika hotuba yake ambayo bado ninaikumbuka hadi leo, alimsifia sana mkuu wa mkoa kwa kukamilisha ujenzi wa uwanja ndani ya miezi tisa tu. Akasema hajawahi kufika katika mkoa wowote kwa ajili ya Sabasaba na kukuta uwanja umekamilika kabisa, ila Sumbawanga!

Likafuata tukio jingine la kusisimua kwa siku hiyo. Mwalimu akasema yeye hastahili kupewa heshima hiyo; jina lake kutumika katika uwanja mkubwa na mzuri kama huo.

Akasema: “Kuna watu wanastahili heshima hii, si mimi! Nadhani uwanja huu unastahili kuitwa Nelson Mandela Stadium.”

Wananchi wakaibuka kwa makofi na vifijo. Wakati huo Mandela bado yupo jela na Nyerere anaendesha kampeni ya kimataifa kumtoa gerezani.

Jenerali Kiwelu akiwa pembeni mwa jukwaa kubwa, ndani ya kombati za jeshi, akasimama, akapiga saluti kwa Amiri Jeshi Mkuu, akawaita wasaidizi wake. Akateta nao. Akatoa maelekezo.

Mara moja wasaidizi hao wakatoka nje ya uwanja na kuanza utekelezaji wa maelekezo ya Jenerali. Wakawachukua mafundi wapaka rangi na kufuta jina la ‘Julius Nyerere Stadium’; badala yake wakaandika ‘Nelson Mandela Stadium’.

Kitendo cha haraka hata kabla Rais Nyerere hajatoka uwanjani kimekamilika!

Uwanja wa Nelson Mandela. Kwa mwaka 1985 ulikuwa miongoni mwa viwanja vya kisasa kabisa, ukiuacha kwa mbali sana Uwanja wa Taifa (siku hizi Uwanja wa Uhuru) wa Dar es Salaam. Ni Uwanja wa CCM Kirumba tu ndio ungeweza kufananishwa na Uwanja wa Mandela uliojengwa na Jenerali Tumainiel Kiwelu.

Hiyo ndiyo ilikuwa Sabasaba ya mwisho ya Mwalimu Nyerere kama Rais wa Kwanza wa Tanzania, kwani Oktoba 1985, mzee Ali Hassan Mwinyi akawa Rais.

Uwanja wa Mandela unaotumika kwa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ni alama ya kudumu iliyoachwa na Kiwelu wala hakuna ubishi katika hilo.

Alama nyingine ni jengo la kisasa kubwa la ghorofa tatu la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa (mkoani).

Kiwelu alisimamia ujenzi wake kwa lengo la kuwa na ofisi yenye hadhi zaidi kuliko aliyoikuta pale maeneo ya Posta, Sumbawanga. Akaelekeza kuwa msitu wa asili uliokuwapo eneo la ujenzi usiguswe.

Kwa hakika hadi leo jengo hilo pamoja na msitu ule wa asili viko vilevile na mandhari yake ni ya kuvutia. Kazi ya Kiwelu hiyo.

Jenerali Kiwelu alitamani sana kuubadili mji wa Sumbawanga. Kuna wakati aliagiza kuwa watu wote wenye nyumba pembezoni mwa barabara kuu ya kutoka Chanji kwenda Sumbawanga Wenyeji hadi Mpanda, ama wajenge nyumba nzuri za ghorofa au wauze maeneo hayo.

Kwamba barabara hiyo ni sura ya mji, lazima kuwe na majengo ya kupendeza! Hakika angedumu Rukwa kwa miaka mitano, Sumbawanga ingebadilika.

Mwaka 1987, wakati nikiwa tayari sekondari, nilikuwapo Uwanja wa Mandela kwenye sherehe za kumuaga Kiwelu (sijawahi kuona mkuu wa mkoa akiagwa namna ile hadi leo) aliyeteuliwa kuwa Mnadhimu Mkuu wa JWTZ na kupandishwa cheo kuwa Luteni Jenerali.

Zilikuwa ni sherehe za huzuni, kwa kuwa wakati huo wananchi walikuwa wanampenda sana, na tayari walikwisha kuzizoea kashikashi zake. Walikuwa wanakwenda naye sambamba bila hofu ya ‘ujeshijeshi’ wake.

Katika sherehe hizo zilizojaa vichekesho, Jenerali Kiwelu alikuwa mtulivu wala hacheki! Uzalendo ulimshinda pale mtoto mmoja wa shule ya vidudu (siku hizi wanaita chekechea) ya masista alipoigiza sauti yake akitoa amri. Hakika Kiwelu alicheka sana hadi akafuta machozi!

Katika hotuba yake ya kuaga akasema mpango uliokuwa akilini mwake ni kujenga uwanja wa kisasa wa ndege Barabara ya Matai.

“Ninataka nikija tena kutembelea Sumbawanga, ndege yangu itue kwenye uwanja huo,” alisema Kiwelu. Ndoto hiyo haijakamilika hadi leo na lau angeendelea kuwapo mkoani Rukwa, uwanja huo ungejengwa wala sina shaka.

Kwa kuonyesha namna gani Kiwelu alikubalika, kuna mtaa mmoja mjini Sumbawanga wenye jina lake; Kiwelu Street! Aaah, ni huzuni sana kwamba hakuwahi kurejea Sumbawanga hadi mauti yanamkuta.

Pumzika kwa amani Jenerali Tumainiel Nderangusho Kiwelu. Rukwa itakukumbuka daima.

0746 336 491

Mwalimu Nyerere akiwa na majenerali Abdallah Twalipo na Tumainiel Kiwelu wakati wa vita ya Kagera

By Jamhuri