Afrika inahitaji mabingwa wa kusaka umoja

Mwaka 1994 akiwa mgeni rasmi kwenye sherehe iliyofanyika Arusha ya kuvunja Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), Mwalimu Julius Nyerere alitoa ujumbe ambao unafaa kurudiwa.

Alisema waasisi wa OAU waliokutana jijini Cairo; Mei 1964 walijipangia kutekeleza majukumu mawili: kwanza, kukomboa bara lote la Afrika kutoka kwenye tawala za kikoloni na za kibaguzi, na pili kujenga umoja wa Afrika.

Tukio la Rais Nelson Mandela kuhudhuria kikao cha marais wa nchi wanachama wa OAU jijini Tunis mwaka 1994, akiongoza ujumbe wa Afrika Kusini baada ya kwisha kwa utawala wa kibaguzi, lilihitimisha kazi ya kuikomboa Afrika.

Itakuwa sahihi kusema kuwa hakuna wakati mwingine katika historia ya nchi huru za Afrika ambapo nchi za Afrika, zikishirikiana na washirika wengine, zimeungana pamoja na kwa ushirikiano mkubwa kufanikisha suala kubwa na muhimu kama la ukombozi.

Tanzania ilipata heshima kubwa ya kuwa makao Kamati ya Ukombozi na viongozi wengi wa nchi zilizoshiriki kwenye mapambano ya kuzikomboa nchi zao waliishi Tanzania wakati wakiendesha mapambano hayo.

Haikuwa kazi ndogo na nchi nyingi, hasa zile zilizokuwa jirani na makoloni na nchi zilizotawaliwa kibaguzi, ziliathiriwa na hujuma mbalimbali za kiuchumi, na uharibifu mkubwa wa miundombinu.

Lakini pamoja na ugumu huo, kazi hii ilifanikiwa kwa sababu ya mikakati madhubuti iliyowekwa kukamilisha kazi hiyo, mikakati iliyotambua umuhimu wa kuwepo ile kamati mahsusi ya kuratibu mapambano yale.

Ukombozi na kujenga umoja ni majukumu mawili yaliyohusiana kwa karibu sana. La kwanza lilifuata la pili. Kusudio lilikuwa kuikomboa Afrika iwe huru, halafu kuziunganisha nchi zote chini ya serikali moja.

Hata hivyo uhuru, suala lililoonekana gumu kufanikisha, likawa ni rahisi kuliko kujenga umoja. Kwa baadhi ya nchi za Afrika, uhuru ulikuwa kama kuwekewa kidhibiti mwendo. Inawezekana kuwa, kwa baadhi ya viongozi wetu, uhuru ulionekana kama hitimisho la mapambano. Ukweli ni kuwa uhuru wa bendera ndiyo ulikuwa mwanzo wa mapambano mengine makali zaidi ya kuhakikisha kuwa rasilimali za bara la Afrika zinatumika kikamilifu kuwaletea Waafrika manufaa.

Uhuru wa bendera ulifunga uwanja mmoja tu wa mapambano, lakini ukafungua mwingine. Mwisho wa ukoloni ulikuwa mwanzo wa kupeperusha bendera za mataifa yetu, lakini haukukata mifumo ya uchumi wa kikoloni iliyokuwa mrefeji wa kupeleka malighafi kaskazini na kuturudishia bidhaa zilizochakatwa kusini.

Watawala wa jana walitumia kila mbinu kulinda mifumo iliyowapa udhibiti mkubwa wa rasilimali za Afrika ili ziendelee kuwanufaisha wao na kundi dogo la vikaragosi wao.

Kwamba kujenga umoja ndiyo kungekuwa moja ya kinga za uhakika za kuinua bara la Afrika kuwa mshirika sawa na mabara mengine, mwenye nguvu za kisiasa, kuichumi, na kijamii haikujidhihirisha wazi kwenye mipango ya pamoja ya nchi za Afrika. Lakini baadhi ya viongozi wa Afrika – kama Kwame Nkrumah na Mwalimu Nyerere – waliliona hilo na kulihimiza.

Katika hotuba yake ya Arusha, Mwalimu Nyerere alisema OAU ilifanya kosa kutokuunda kamati ya umoja ambayo ingesimamia kwa umakini zaidi ajenda ya umoja, kama ambavyo iliunda Kamati ya Ukombozi. Moja ya sababu ni kuwa nchi waasisi ziligawanyika kwenye makundi mawili yenye mitazamo tofauti ya njia ya kufuata kujenga umoja. Misimamo hiyo tofauti iliathiri jitihada za haraka za kujenga umoja.

Waliyoogopa umoja wa Afrika waliogopa pia kukatiwa mirija yao ya kuendelea kunufaika na rasilimali za bara la Afrika. Hawa walitumia kila mbinu kudhoofisha jitihada zozote za nchi za Afrika kuungana. Na hiyo kazi hawajaimaliza.

Tunakaribia kusherehekea miaka 70 ya nchi nyingi za Afrika kupata uhuru tukiona kuwa kasi ya kujenga umoja haijabadilika sana tangu Mwalimu Nyerere ahutubie Arusha.

Kama tumefanikiwa kulikomboa bara la Afrika, lakini bado tunasuasua kujenga umoja, tunahatarisha uwezekano wowote wa kuimarisha maendeleo ya kiuchumi ya bara la Afrika. Kwa kifupi tunaruhusu kuendelea kuwapo mazingira ya kunufaisha wengine bila sisi kunufaika.

Kwenye mdahalo uliyoandaliwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) mshirika kutoka Zimbabwe ambaye ni Katibu Mkuu mwanzilishi wa SADC, Dk. Simba Makoni, alisema kuwa kila suala linalohitaji mafanikio linahitaji kuongozwa na bingwa. Timu ya Genk ina wachezaji wengi, lakini inamhitaji Mbwana Samatta kuleta ushindi.

Makoni anasema akiwa Katibu Mkuu wa SADC alikuwa na uhakika kuwa uamuzi wowote ulioungwa mkono na Mwalimu Nyerere, Rais Samora Machel wa Msumbiji, na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ungetekelezwa kwa mafanikio makubwa. Alisisitiza kuwa viongozi wengine walikuwa muhimu pia, lakini ni kupitia hawa “mabingwa” ndiyo kulikuwa na uhakika wa kutekeleza uamuzi muhimu.

Nchi za Afrika zina uzoefu mkubwa wa kupambana na ukoloni na ubaguzi. Uzoefu ule unaweza kuhamishiwa kwenye jitihada za kujenga umoja kwa madhumuni ya hatimaye kuunganisha jitihada za pamoja za kujenga masoko, uchumi, mawasiliano, miundombinu, na viwanda.

Tukitumia wazo la Dk. Makoni la kutumia mabingwa, wakajielekeza kujenga umoja na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, inawezekana tukaiona Afrika inapiga hatua kubwa mbele.