Wako watu ni wazazi na wamezaa lakini wameyimwa watoto. Zipo sababu nyingi katika jambo hili. Matukio ya namna hii hayawatokei sana wanawake bali wanaume. Ni rahisi na kawaida mno mwanamume kuambiwa na mzazi mwenzake  kuwa huyu  mtoto si wako hata  kama  anajua kabisa huyo mwanamume ndiye mzazi halisi.

Upo usemi wao kuwa mwanamke ndiye anayejua baba wa mtoto. Sitaki kueleza ukweli au upotoshajii wa usemi huu, bali nawaza iwapo ni sawa kutumia usemi huu  kupora haki ya uzazi  wa mtu ambaye unajua kabisa ndiye mzazi halisi.

Na kwa bahati mbaya wanaokutwa na kadhia hii wamekuwa hawajui ni hatua zipi wachukue. Wapo wanaoamua kufanya vurugu, wapo wanaojiua, wapo wanaoamua kumuachia Mola, na wengine hukimbilia ofisi za serikali za mitaa kuchukua hatua za ziada.

Ukweli ni kuwa hatua hizo haziwezi kukusaidia. Basi sasa yafaa  ujue kuwa sheria imetambua jambo hili na imeweka taratibu nzuri za kufuata ili kuondoa ujeuri wa aina hii.

Sheria Namba 21, Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 imeeleza nini ufanye kama tutakavyoona hapa. Lakini kabla ya hilo hebu kwa kutaja tu tuone sababu kadhaa zinazofanya wazazi hasa wa kike kuwanyima wazazi wenzao haki ya kutambulika kama wazazi wenzao.

Sababu ya kwanza, ukosefu wa kipato. Mtu anajua kabisa fulani ndiye mzazi wa fulani lakini kwa sababu ya uchumi mdogo, basi anakataa kumtambua mzazi huyo halisi na kumtambua asiye halisi.

Pili, tofauti za kidini. Mtu anasema mtoto wangu hawezi kutambulika kwa baba fulani kwa sababu ya dini tofauti. Anasema bora akae bila baba au anamtafutia baba mwingine.

Tatu, kukomoa. Mtu anamnyima mtoto mzazi halisi kisa waligombana, hivyo ni nafasi kwake sasa kumkomoa. Nne, familia mbili kutoelewana. Mtu anasema mtoto wangu hawezi kuzaliwa katika familia au ukoo wa kina fulani.

Tano, ubaguzi wa rangi. Ndugu wanamshawishi mwanamke amkatae baba wa mtoto kwa kuwa wao ni Wahindi, Waarabu na baba ni Mwafrika, Mzungu au kinyume chake.

Hatua za kuchukua

Sehemu ya 5, Kifungu cha 34( 1 )(b) cha Sheria ya Mtoto ya 2009 kinasema kuwa mtu yeyote anayeamini kuwa ni mzazi wa mtoto fulani anaweza kuiomba mahakama itoe amri ya kumtambua rasmi kama mzazi.

Haraka hapa utaona kuwa kitu kizuri na cha kisheria ni kwenda mahakamani na kuiomba mahakama ikutangaze kama mzazi halali wa mtoto. Itakuwa ni njia sahihi kabisa na isiyo na usumbufu.

Kifungu cha 3 ( a ) cha sheria hiyo kinazitaja mahakama zinazoshughulikia suala hilo kuwa ni Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama Kuu. Hata hivyo unashauriwa kuitumia Mahakama ya Mwanzo iliyo katika eneo lako au Mahakama ya Wilaya iliyo ndani ya wilaya yako. Mahakama ni sehemu salama kabisa wala hauna  haja ya kuhofu.

Maombi haya yanaweza kuombwa na baba ikiwa mama amedai kutomtambua  kama mzazi halali au mama ikiwa baba amemkataa mtoto.

Kifungu cha 35 cha Sheria ya Mtoto kinaeleza kwamba unatakiwa kujiandaa na haya; kuthibitisha ndoa. Kama hakuna ndoa kutafanyika kipimo cha DNA kama ushahidi, jambo jingine ni ushahidi kuwa baba alifanya taratibu za kiukoo/kimila kumtambulisha mtoto.

Jambo jingine ni jina la ubini au la baba ambalo mtoto amesajiliwa au kuandikishwa nalo. Huu ni ushahidi, lakini pia nani jamii inamtambua kama mzazi wa mtoto, nao ni ushahidi pia.

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, kampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.

By Jamhuri