Uhispania imeshinda Kombe la Dunia 2026 kwa kuwabamiza mabingwa watetezi timu ya soka ya Argentina bao 1-0.

Mshambuliaji Ferran Torres ndiye ameifungia Uhispania bao la pekee lililowapa ushindi na kunyakua Kombe la Dunia kwa mara ya pili katika historia.

Mchezo wa fainali uliopigwa kwenye dimba la MetLife huko New Jersey ulikwenda hadi dakika za nyongeza baada ya miamba hiyo miwili kushindwa kutikisa nyavu za mwingine ndani ya dakika 90.

Bao la ushindi la Uhispania lilipatikana dakika ya 106 ya mchezo pale mshambuliaji Nico Williams alimpompigia pasi maridadi Torres aliyemalizia vyema kwa kuutia mpira wavuni.

Uhispania ilikuwa nusura iondoke na ushindi wa mabao mawili kwenye mchezo huo, lakini bao la awali la Williams lilikatiliwa na mwamuzi aliyepuliza firimbi alipoona rafu imechezwa.

Uhispania ambao pia ni mabingwa wa michuano ya mataifa ya Ulaya 2024, walionesha kandanda safi dakika zote tisini kwa kuwanyima Argentina ya Lionel Messi nafasi ya kufurukuta.

Timu hiyo ya kinda mwenye nyota kali Lamine Yamal ilipambana kwa muda mrefu kutikisa nyavu za Argentina bila mafanikio ambayo ilijikuta na wachezaji 10 pekee wakati wa kipindi cha pili.

Messi na wenzake washindwa kutamba mbele ya kikosi cha kinda Lamine Yamal

Mambo yaliwaendea kombo Argentina pale kiungo wao mchezeshaji Enzo Fernandez alipotolewa nje kwa kuoneshwa kadi ya pili ya njano baada ya kumfanyia madhambi Pau Cubarsi wa Uhispania.

Kichapo hicho kwa Argentina ni mzigo mzito kwa Lionel Messi ambayo yumkini hilo litakuwa kombe lake la mwisho la dunia.

Kulikuwa na matumaini kwa Argentina kunyakua kombe la mwaka huu ambalo lingempa heshima kubwa na mkono wa heri Messi mwenye umri wa miaka 39 ambaye ameonesha kandanda lisilo la kawaida katika miaka yake yote ya kucheza soka.

Ushindi kwa Argentina ungeipa pia timu hiyo sifa kubwa ya kutetea taji hilo kama walivyofanya miaka minne iliyopita nchini Qatar.

Hata hivyo inaonesha kikosi cha kocha Luis de la Fuente kilidhamiria kuwapokonya tonge mdomoni na kurejea nyumbani wakiwa na Kombe la Dunia kama walivyofanya mwaka 2010 nchini Afrika ya Kusini.

Mbali ya ushindi huo kikosi cha Fuente kinaacha nyuma rikodi ya kuwa kuruhusu goli moja pekee katika michuano hiyo ya Kombe la Dunia 2026.