Na Albano Midelo, JamhuriMedia, Ruvuma

UBORA wa mji hupimwa kwa majengo yake yaliopangwa vizuri, barabara zake au idadi ya watu wake. Lakini mji wa Songea unaonekana kupimwa kwa jambo jingine lisilopewa uzito na wengi jinsi inavyoshughulikia taka zake.

Kila chupa ya plastiki inayotupwa ovyo, kila mfuko unaoziba mfereji na kila dampo lisilosimamiwa vizuri ni jambo linaloweza kuamua afya ya maelfu ya wananchi, hadhi ya mji na hata mustakabali wa uchumi wake.

Wakati baadhi ya watu wakiona taka kama kitu kisicho na thamani, wataalamu wa mazingira wanaona rasilimali inayoweza kuzalisha ajira, mbolea, nishati na mapato. Ndiyo maana vita dhidi ya uchafu katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma si kampeni ya usafi pekee, bali ni mapambano ya kulinda afya, mazingira na uchumi wa kizazi cha sasa na kijacho.

Katika mitaa yenye shughuli nyingi za biashara, masoko yanayopokea maelfu ya wananchi kila siku na makazi yanayozidi kupanuka kutokana na ongezeko la watu, uzalishaji wa taka unaongezeka kwa kasi ambayo inahitaji mipango madhubuti ya usimamizi.

Manispaa ya Songea, ambayo ni kitovu cha biashara na huduma katika Mkoa wa Ruvuma, imeingia katika kipindi kipya cha kuimarisha usafi wa mazingira huku ikikabiliana na changamoto zinazotokana na ukuaji wa haraka wa mji.

Licha ya mafanikio yaliyopatikana katika ukusanyaji wa taka na utoaji wa elimu kwa wananchi, bado baadhi ya wakazi wameendelea kutupa taka ovyo kwenye mifereji ya maji, maeneo ya wazi na kandokando ya barabara. Kitendo hicho kimekuwa kikitishia afya ya jamii, kuongeza hatari ya mafuriko wakati wa mvua na kuchangia kuzaliana kwa wadudu wanaosababisha magonjwa.

Uchunguzi uliofanyika katika baadhi ya kata za Manispaa ya Songea umebaini kuwa makopo ya plastiki, chupa za maji, mifuko ya plastiki na taka nyingine ngumu bado hutupwa ovyo katika maeneo mbalimbali ya mji licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na halmashauri kuimarisha usimamizi wa taka.

Muonekano wa baadhi ya majengo ya mji wa Songea mkoani Ruvuma

SOKO LA BOMBAMBILI; KITOVU CHA BIASHARA CHANZO KIKUBWA CHA TAKA

Moja ya maeneo yanayozalisha taka nyingi zaidi ni Soko la Bombambili, ambalo kila siku hupokea wafanyabiashara na wanunuzi kutoka Songea na maeneo ya jirani.

Mfanyabiashara wa soko hilo, Saidi Katoto, anasema ongezeko la biashara ya matunda, mboga na bidhaa mbalimbali limeongeza kiasi cha taka kinachozalishwa kila siku.

“Soko letu linazalisha taka nyingi kwa sababu bidhaa zinazouzwa ni nyingi. Changamoto kubwa hujitokeza wakati wa masika ambapo maji yanachanganyika na taka na kuingia mpaka kwenye nyumba za jirani. Hata hivyo, hali imeanza kuboreka baada ya Manispaa kuweka utaratibu wa kuhifadhi taka sehemu maalumu kabla ya gari la taka kufika.”

Anasema wakati wa kiangazi changamoto hupungua, lakini kipindi cha masika mvua kubwa huonyesha hivyo kuna umuhimu wa kuboresha miundombinu ya mifereji na barabara ndani ya soko.

Hata hivyo amesema, magari yanajitahidi kukusanya taka tofauti na siku za nyuma, jambo ambalo limepunguza mlundikano wa uchafu sokoni.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti wa Taka na Usafi wa Mazingira wa Manispaa ya Songea

SERIKAI YAONGEZA KASI KUSIMAMIA USAFI

Akizungumza kuhusu hali ya usafi wa mazingira katika Mkoa wa Ruvuma, Mkuu wa Mkoa, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, amesema usafi wa mazingira hauishii kufagia maeneo ya wazi bali unahusisha upangaji bora wa makazi na matumizi sahihi ya ardhi.

Anasema bado yapo maeneo ambayo nyumba zimezungukwa na nyasi ndefu, taka na miundombinu isiyopangwa vizuri.

“Kama nyumba zimejengwa bila kuzingatia mipango miji, hata magari ya zimamoto yatashindwa kupita inapotokea dharura. Hivyo usafi wa mazingira unapaswa kwenda sambamba na upangaji bora wa miji.”
Kauli hiyo inaonesha kuwa changamoto za mazingira haziwezi kutenganishwa na mipango ya maendeleo ya miji.

Tani 90 za taka kila siku: Je, Songea inaweza Kumudu?

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti wa Taka na Usafi wa Mazingira wa Manispaa ya Songea, Amani Mmasi, anasema kasi ya ukuaji wa mji wa Songea imeongeza kiwango kikubwa uzalishaji wa taka.

Kulingana na Afisa huyo, Manispaa hiyo huzalisha wastani wa tani 90 za taka kila siku, huku uwezo wa sasa wa ukusanyaji ukiwa takribani tani 75 kwa siku, na tani zilizobaki hukusanywa siku inayofuata.

Anasema taka hizo husafirishwa hadi katika dampo la Subira lenye ukubwa wa takribani hekari 98, lililopo umbali wa kilomita 12 kutoka katikati ya mji.

Kwa sasa Manispaa inatumia magari mawili ya kubeba taka yenye uwezo wa tani 10 kila moja pamoja na mashine maalumu ya kukusanya na kushindilia taka.

Hata hivyo, amesema mpango wa kununua magari manne mapya ya kisasa uko katika hatua za mwisho ili kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa taka na kupunguza ucheleweshaji unaoweza kujitokeza.

KUTOKA DAMPO HADI KIWANDA CHA FURSA

Kinachovutia zaidi katika mkakati mpya wa Manispaa ya Songea siyo ukusanyaji wa taka pekee, bali ni mpango wa kuzigeuza taka kuwa rasilimali.

Kwa mujibu wa Amani Mmasi, Manispaa imeanza maandalizi ya kuanzisha mfumo wa kuchakata taka ambapo taka zinazooza zitatumika kutengeneza mbolea ya asili (compost manure), huku taka zisizooza kama plastiki na chupa zikielekezwa kwenye shughuli za urejelezaji (recycling).

Anasema kutokana na wilaya ya Songea kuwa miongoni mwa maeneo yenye shughuli kubwa za kilimo, mahitaji ya mbolea yanaendelea kuongezeka kila mwaka.

“Tunataka taka ziwe chanzo cha ajira na kipato. Badala ya kuziona kama uchafu pekee, tunaziona kama malighafi ya kuzalisha mbolea na bidhaa nyingine.”

Mpango huo pia unatarajiwa kuhusisha vikundi vya vijana na wanawake vitakavyoshiriki katika uchakataji wa taka na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali.

SHERIA ZINAVYOIMARISHA NIDHAMU YA USAFI

Katika kuhakikisha taka hazitupiwi hovyo, Manispaa ya Songea inatekeleza Sheria Ndogo za Usafi wa Mazingira za mwaka 2025, ambazo zinawataka wananchi kuhifadhi taka katika vyombo maalumu na kuzikabidhi kwa magari ya ukusanyaji taka.

Sheria hizo pia zinaweka adhabu kwa yeyote atakayebainika kutupa taka ovyo kwenye maeneo ya umma.
Kwa mujibu wa Mmasi, elimu inaendelea kutolewa kupitia mikutano ya hadhara, vyombo vya habari na kampeni za usafi zinazofanyika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi katika kata zote.

“Mabadiliko yapo, lakini elimu iongezwe”

Mkazi wa Bombambili, Ediga Mtanga, anasema miaka michache iliyopita taka nyingi zilikuwa zikitupwa ovyo, lakini hali imeanza kubadilika kutokana na elimu inayotolewa na Manispaa pamoja na vikundi vya kujitolea.

Anasema yeye pamoja na wenzake wameamua kukusanya chupa za plastiki na makopo yaliyotupwa ovyo na kuyauza kwa watu wanaoyahitaji.

“Tunaona taka kama fursa ya kipato. Lakini bado kuna watu wengi wanaotupa makopo na chupa ovyo. Elimu iendelee kutolewa ili kila mtu ajue kuwa mazingira safi ni jukumu la wote.”

Kwa upande wake, Angel Nyirenda, mwanafunzi anayejitolea kupitia Taasisi ya Saint Teresa Orphan Foundation (STOF), anasema programu ya kuokota taka imeanza kuleta matokeo chanya.

“Mwaka jana tukisimamiwa na STOF tulipoanza tuliokota mamia ya maroba ya taka. Sasa kiasi chake kimeanza kupungua katika baadhi ya maeneo. Hii inaonesha wananchi wanaanza kubadilika, lakini bado tunahitaji elimu endelevu kwa sababu baadhi ya watu bado hutupa taka bila kujali madhara yake.”

Fuatilia katika Sehemu ya Pili ya Makala hii: Uchambuzi wa Tanzania, kulinganisha Songea na Njombe pamoja na Moshi, na uzoefu wa nchi nyingine za Afrika na dunia katika usimamizi wa taka na usafi wa mazingira.

Baadhi ya taka ngumu ambazo zinatupwa hovyo katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye mifereji ya maji hali ambayo inasababisha mitaro kuziba wakati wa mvua za masika