Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Mkoa wa Pwani una nafasi ya kipekee na ya kimkakati nchini Tanzania, ukiwa lango kuu la kibiashara linalounganisha Jiji la Dar es Salaam na mikoa mingine nchini pamoja na nchi jirani.

Kabla ya Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, sehemu kubwa ya mtandao wa barabara mkoani Pwani ilikuwa ya changarawe na udongo, ikitumika zaidi kurahisisha shughuli za kiutawala, usafirishaji wa mazao na kuunganisha maeneo muhimu ya kiuchumi.

Aidha, hali hiyo iliambatana na changamoto za usafiri, hasa wakati wa mvua, ambapo baadhi ya maeneo yalikuwa na muunganiko hafifu uliokuwa ukiathiri biashara, huduma za kijamii na shughuli za maendeleo.

Baada ya Uhuru, Serikali iliendelea kuweka mikakati ya kuboresha miundombinu ya usafirishaji kwa kujenga, kukarabati na kupanua mtandao wa barabara ili kufungua maeneo ya uzalishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Kutokana na mazingira yake ya kijiografia, Mkoa wa Pwani umeendelea kuwa eneo lenye umuhimu mkubwa kiuchumi, ukiwa kitovu cha uwekezaji wa viwanda vinavyochipuka kwa kasi pamoja na ongezeko la shughuli za biashara na watu wanaohamia kutafuta fursa.

Ili kuendana na kasi hiyo ya ustawi, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Pwani, imeendelea kuwekeza katika kuboresha, kutanua na kufungua mtandao wa barabara.

Jitihada hizi zinalenga kimkakati kuondoa vikwazo vya usafirishaji, kuchochea biashara, na kuhakikisha miundombinu inarahisisha maisha ya wananchi na uendeshaji wa shughuli za kiuchumi kwa ufanisi wa hali ya juu.

BAJETI INAVYOAKISI MAENDELEO YA MIUNDOMBINU YA BARABARA

TANROADS hutekeleza miradi ya barabara kupitia bajeti ya Serikali Kuu inayotolewa na Wizara ya Ujenzi, katika mwaka wa fedha 2026/2027, Wizara hiyo iliomba bajeti ya takribani sh. trilioni 2.564 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya barabara na madaraja nchini.

Mgawanyo huo unaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha sekta ya usafirishaji kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi, ambapo Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa maeneo yanayonufaika kutokana na nafasi yake ya kimkakati kama kiungo muhimu kati ya Dar es Salaam na maeneo mengine nchini.

MTANDAO WA BARABARA NA MIRADI YA KIMKAKATI

Meneja wa wakala wa barabara TANROADS mkoani Pwani, Mhandisi Baraka Mwambage alieleza, mtandao wa barabara chini ya usimamizi wa wakala huo una jumla ya urefu wa km 1510.58, ambapo barabara kuu ni km 503.66 na barabara za mkoa km 59.717 zikiwa za kiwango cha lami.

Barabara za mkoa zina jumla ya km 1006.92 ambazo km 50.717 ni za lami na km 947.22 ni za changarawe na udongo.

Katika bajeti ya miradi ya maendeleo mkoa, mwaka 2024/2025 ilikuwa bilioni 11.063, mwaka 2025/2026 bilioni 15.5 na mwaka 2026/2027 imefikia bilioni 16.430 ambapo miradi ya matengenezo kwa mwaka 2026/2027 ni bilioni 25.879.

Miongoni mwa miradi ya kimkakati ni ujenzi wa barabara ya Tamco–Mapinga yenye urefu wa kilomita 23, ambapo sehemu ya Tamco–Pangani yenye urefu wa kilomita 8.5 ilianza kutekelezwa mwaka 2022 na inatarajiwa kukamilika Juni 2027 kwa gharama ya zaidi ya sh. bilioni 5.628.

Katika mradi huo kilomita 4.7 imekamilika kwa kiwango cha lami, huku mkandarasi M/S Kaserkandis akiendelea na kazi za ujenzi wa sehemu iliyobaki kwa ujumla, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 80.

Mradi wa Pangani–Mapinga ulianza Aprili 2024 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2027, ukiwa na thamani ya sh. bilioni 17.859. Mkandarasi Kings Builders Ltd anaendelea na utekelezaji ambao umefikia asilimia 79, ukiwa katika hatua za maandalizi ya uwekaji lami na ujenzi wa tabaka la barabara.

Kuhusu barabara ya Nyamwage–Utete yenye urefu wa kilomita 33.7, Mwambage alieleza ujenzi ulianza Julai 2023 na unagharimu Sh bilioni 43.419, mkandarasi M/S China Railway Seventh Group (CRSG) anaendelea na kazi ambapo mradi umefikia asilimia 19.

Ujenzi wa daraja la Mbambe lenye urefu wa mita 81 pamoja na barabara unganishi ya kilomita 3 kwa kiwango cha lami unaendelea, ambapo mradi huo ulianza mwaka 2023 na unagharimu zaidi ya Sh bilioni 24.164.

Mradi umefikia asilimia 49 huku mkandarasi M/S Nyanza Road Works Limited akiendelea na ujenzi wa misingi ya daraja na barabara unganishi.

Katika mradi wa barabara ya Chalinze–Utete yenye urefu wa kilomita 354.9 kupitia Bwawa la Mwalimu Nyerere upo katika hatua ya manunuzi ya mhandisi mshauri kupitia Ofisi ya Mtendaji Mkuu.

Pia upanuzi wa barabara kuu ya Morogoro eneo la Kibaha–Maili Moja–Picha ya Ndege wenye urefu wa kilomita 3.6 kwa njia sita, pamoja na mradi wa Kibaha–Chalinze Expressway awamu ya kwanza, upo katika hatua ya manunuzi ya mhandisi mshauri.

Kutokana na ongezeko la magari, uwekezaji wa viwanda na shughuli za kiuchumi, barabara kuu ya Morogoro imekuwa ikikabiliwa na msongamano mkubwa hasa nyakati za asubuhi na jioni, hivyo miradi hiyo inalenga kutoa suluhisho la muda mrefu.

Changamoto nyingine ni ucheleweshwaji wa malipo ya kandarasi na upungufu wa malighafi za ujenzi hasa changarawe katika baadhi ya maeneo ya miradi.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge alibainisha kuwa, katika utekelezaji wa ibara 40 ya ilani ya Chama Cha Mapinduzi, Serikali inaendelea kuimarisha sekta ya usafirishaji kwa kuboresha miundombinu ya barabara, madaraja na vivuko,na barabara kuu za kimkakati.

Kunenge alieleza, maendeleo ya sekta ya barabara yamefungua maeneo mapya ya biashara na kurahisisha muunganiko kati ya viwanda, bandari na masoko ya ndani na nje ya nchi.

Kutokana na hilo mkoa umeongeza idadi ya viwanda kutoka 1,631 hadi 1,722 Machi 2026 kati ya hivyo viwanda 226 ni vikubwa, 231 vya kati, 248 vidogo na 1,017 vidogo sana huku ajira zikiongezeka kutoka 14,559 mwaka 2021 hadi 22,289 mwaka 2026 sanjali na ajira zisizo za moja kwa moja zaidi ya 62,000.

Vilevile katika kipindi cha awamu ya sita jumla ya viwanda 335 vimejengwa ambapo 82 vipo katika hatua mbalimbali za ujenzi na viwanda 8 vimeanzisha uzalishaji ndani ya siku 100.

Pia Kunenge ameonyesha imani yake kwa TANROADS mkoa kuendelea kusimamia ipasavyo utekelezaji wa miradi ya barabara ili kuendana na kasi ya ukuaji wa mkoa.

Hivi karibuni Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega alielezea, Serikali imeweka kipaumbele katika kuufungua Mkoa wa Pwani kupitia barabara za Tamco–Mapinga–Bagamoyo, Bagamoyo–Makofia–Mlandizi–Mzenga na Kibaha–Kisarawe, ambazo zimepangwa kupewa fedha katika bajeti ya 2026/2027.

Kwa mujibu wa Ulega, miradi hiyo itawaondolea wananchi wa Mkuranga, Kibiti na Rufiji adha ya kupita Dar es Salaam wanaposafiri kwenda makao makuu ya Mkoa wa Pwani.

Alifafanua ,Serikali inaendelea na mkakati wa kupunguza msongamano Kibaha kupitia ujenzi wa njia nane (Kimara–Kibaha–Chalinze Expressway) ujenzi wa barabara mbadala usimamizi wa trafiki kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.

Ulega alitoa rai kwa wakandarasi kuzingatia umuhimu wa kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa wakati ili kuepusha hasara kwa serikali na mateso kwa wananchi kutokana na ubovu wa barabara huku akiwaomba wananchi kushirikiana na wakandarasi katika kukamilisha miradi.

USALAMA BARABARANI NA UDHIBITI WA MSONGAMANO


Katika kuhakikisha miundombinu ya barabara inakuwa tija kwa ajili ya vizazi vijavyo suala la usalama wa watumiaji wa barabara limepewa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Pwani (RTO), Edson Mwakihaba alisema ,upanuzi wa barabara, uwekaji wa taa za barabarani na ujenzi wa njia mbadala umesaidia kupunguza matukio ya ajali na msongamano uliokuwa ukijitokeza kutokana na ufinyu wa njia.

Mwakihaba alieleza, TANROADS imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani katika kuhakikisha uwepo wa alama sahihi za usalama, taa za kuongozea magari pamoja na maeneo salama kwa watembea kwa miguu ili kuongeza usalama kwa wananchi.

SAUTI ZA WABUNGE
Mbunge wa Kibaha Mjini, Silvestry Koka, anaridhishwa na utekelezaji wa mradi wa Njia Nane Kimara–Kibaha, lakini alisisitiza umuhimu wa mradi huo kuendelea kupita ndani zaidi ya mji wa Kibaha ili kuongeza manufaa ya kiuchumi kwa wananchi.

Alielezea kwamba, Kibaha ni lango la uchumi kati ya Dar es Salaam na mikoa ya ndani, hivyo miradi ya kimkakati inapaswa kuwa na matokeo ya moja kwa moja kwa wananchi.

Mbunge wa Bagamoyo, CPA Subira Mgalu alipongeza ,maendeleo ya miradi ya barabara huku akisisitiza kukamilishwa kwa miradi iliyoanza na kuharakishwa kwa ile iliyokwama.

Alisema barabara ya Kibaha–Mapinga na Afrika Mashariki Pangani–Makurunge ni muhimu katika kuimarisha mawasiliano ya kikanda na kufungua fursa za kiuchumi.

Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, alisisitiza umuhimu wa miradi ya barabara katika kukuza biashara, utalii na uwekezaji katika maeneo ya Chalinze.

Ridhiwani alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia TANROADS kwa kuelekeza mabilioni ya fedha katika kuongeza mtandao wa barabara Chalinze na Mkoa wa Pwani, akisema utekelezaji huo unaendelea kuchochea ukuaji wa uchumi.

SAUTI ZA WANANCHI NA WAWEKEZAJI
Mbali na viongozi, wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji wameanza kushuhudia matunda ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara.

Juma Omari, mkazi na dereva wa usafiri wa abiria Chalinze, alieleza zamani kusafirisha bidhaa kutoka maeneo ya vijijini kwenda sokoni Kibaha ilikuwa changamoto kubwa, hasa wakati wa mvua ambapo baadhi ya barabara zilifungika.

Amina Salim, mama lishe katika barabara ya mchepusho Tamco–Maili Moja–Sheli, alieleza mafanikio yaliyopatikana ni makubwa, lakini Serikali inapaswa kuendelea kutatua changamoto zilizopo.

Barabara hiyo bado inakabiliwa na changamoto ya vumbi linalosababishwa na magari makubwa kupita eneo hilo, hali inayowaathiri wafanyabiashara na wananchi kiafya.

Anataja pia changamoto za mabadiliko ya tabianchi yanayosababisha mvua kubwa kuharibu miundombinu ya barabara za vumbi kabla ya kuwekwa lami, pamoja na kuchelewa kwa fidia kwa baadhi ya wananchi wanaopisha miradi.

Mwekezaji katika eneo la Zegereni, Kibaha Mjini, George Ally, alisema ubovu wa baadhi ya barabara za vumbi, hususan barabara ya Kinglion, umekuwa ukikwamisha mipango ya uwekezaji.

Alisema malori yanayobeba vifaa vya ujenzi na saruji yamekuwa yakikwama katika maeneo yenye matope kwa muda mrefu, jambo linaloongeza gharama za uendeshaji na kuchelewesha kukamilika kwa miradi ya viwanda.

FAIDA ZA KUBORESHA BARABARA PWANI


Uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali kupitia TANROADS umeendelea kuvutia na kukuza uwekezaji wa viwanda Mkoa wa Pwani, kupunguza gharama na muda wa usafiri, kuchochea biashara na masoko ya mazao ya kilimo pamoja na kukuza sekta ya utalii.

Kufunguka kwa mtandao wa barabara kumesababisha ongezeko la thamani ya ardhi, huku maeneo mengi yaliyokuwa hayafikiki kwa urahisi sasa yakifunguka kwa shughuli za makazi, biashara na uwekezaji.

Hali hiyo imeongeza fursa za mapato kwa halmashauri kupitia kodi za majengo na ardhi.

Ni dhahiri kuwa mageuzi makubwa ya miundombinu ya barabara yanayotekelezwa na TANROADS Pwani chini ya Serikali ya Awamu ya Sita si tu yamerahisisha usafiri, bali pia yanatengeneza msingi mpya wa ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Pwani na Tanzania kwa ujumla.

Ili uwekezaji huo wa mabilioni ya fedha ulete tija iliyokusudiwa kwa miaka mingi ijayo, ni wajibu wa wananchi, wasafirishaji na wadau wote wa maendeleo kushirikiana kulinda miundombinu, kuzingatia sheria za usalama barabarani na kutumia fursa za kiuchumi zinazofunguka kwa maendeleo endelevu.