Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), kimepata mafanikio makubwa baada ya Rais Samia Sulubu Hassan kuifungua nchi.

Hayo yamebainishw leo Septemba 14, 2023 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa vituo vya AICC na JNICC, Ephraim Mafuru wakati akizungumza na wahariri na waandishi wa habari ikiwa ni mwendelezo wa vikao kazi baina ya taasisi na mashirika ya umma chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

“Juhudi za Rais Samia Sukuhu Hassan zimechangia Diplomasia ya Mikutano nchini kuendelea kustawi na kuimarisha shughuli za kiuchumi na kukuza pato la Taifa.

“Kwa sasa, wageni wanaipenda Tanzania na wanakuja Tanzania kwa wingi, namshukuru Rais Samia kw kazi kubwa aliyoifanya.

“Ninajua kuna Royal Tour, lakini amekuwa akishiriki mikutano mbalimbali kuitangaza nchi, hivyo Tanzania imeendelea kuwa chaguo muhimu na kuvutia mikutano mbalimbali ya Kimataifa.” amesema.

Aidha, amesema, baada ya kampeni kubwa ya kufungua nchi,wamekuwa na asilimia 10 ya market shares katika Afrika, hivyo kwa sasa wanandaa mikakati mbalimbali ya kuhakikisha wanafikia malengo makubwa ya kuleta kwa wingi fedha za kigeni nchini.

“Arusha kama kitovu cha utalii, na sisi kama kitivo cha utalii, tunashiriki kikamilifu kuhakikisha tunafanikisha shughuli hizo ili kuimarisha myororo wa thamani nchini.”

Amesema, pia huwa wanashiriki kutangaza namna ambavyo wageni wanaweza kufika na fursa zilizopo katika maeneo yao wakijumuisha vivutio mbalimbali vya utalii nchini hususani jijini Arusha.

“Tunajivunia na kujisikia fahari kwa vituo vyetu viwili (AICC na JNICC) kwa kufanikiwa kuandaa mikutano mbalimbali ya Kimataifa.

“Pia, tuna uwezo wa kutafsiri hadi lugha tano katika kumbi za mikutano kwa wageni wetu wakati mikutano ikiendelea.”

Amesema, AICC na JNICC vimekuwa na uwezo mkubwa wa kuandaa mikutano mikubwa ya Kitaifa na Kimataifa.

Pia, amemshukuru Msajili wa Hazina, Nehemiah Msechu kwa kubuni jukwaa kati ya wahariri ambalo linatoa fursa kwa taasisi na mashirika ya umma ili kuweza kuwaeleza watanzania wanachokifanya.

“Kwa hiyo AICC ilianzishwa mwaka 1969. Kazi zetu kubwa ni kuendesha mikutano, hivyo tuna kumbi za mikutano, nyumba za kupangisha na hospitali.”

Aidha, amesema msukumo mkubwa ni kuhakikisha Diplopmasia ya Mikutano inaendelea kuwa nguzo muhimu katika Diplomasia ya Uchumi nchini.

Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema kuwa, kupitia utafiti wao wamebaini kuwa diplomasia ya mikutano ina mchango mkubwa katika kuongeza fedha za kigeni na kuimarisha uchumi nchini.Majukumu makuu ya AICC ni kuandaa mikutano mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa.

Kuhusu AICC

Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema, Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) kilianzishwa chini ya Sheria ya Mashirika ya Umma Na.17 ya mwaka 1969 kwa agizo la Rais kupitia tangazo la Serikali namba 115, lililochapishwa tarehe 25 Agosti 1978.

Aidha,amesema kituo hicho kinamilikiwa na Serikali ya Tanzania na kinafanya kazi chini ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

“Kituo hiki kinafanya kazi kama shirika kamili la kibiashara huku utoaji wa huduma za mkutano ndio biashara kuu.”

Hata hivyo, AICC pia hukodisha ofisi katika majengo ya makao makuu na makazi katika Manispaa ya Arusha. Kituo kinatoa huduma za afya kupitia hospitali yake iliyopo Manispaa ya Arusha.

AICC pia inamiliki na kuendesha Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) kilichopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

JNICC ni Kituo cha Mikutano kilichojengwa kwa madhumuni mengi katika Jiji la Dar es Salaam, chenye teknolojia ya kisasa ya sauti-video, mawasiliano na habari. “Maono, ni kuwa mfano na kiungo muhimu katika biashara ya utalii hapa nchini.”

Amesema, AICC wanamiliki nyumba na ofisi mbalimbali ambazo wanaendelea kuziboresha na kuziendeleza ili kuongeza kipato kwa taasisi na shirika.

Pia, amesema hospitali yao (AICC Hospital) ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa zaidi ya 90,000 kwa mwaka, hivyo licha ya kutoa huduma ya afya pia imekuwa sehemu ya kutengeneza mapato.

Katika hatua nyingine, Mafuru amesema, JNCC ni kituo ambacho walikabidhiwa na Serikali, miaka kama tisa iliyopita kwa ajili ya kukiendesha.

“Hivyo tunaendelea kufanya hivyo na kadri siku zinavyoendelea tutaendelea kufanya maboresho makubwa ili kuongeza mapato ya Serikali.”

Wakati huo huo, Mafuru amebainisha kuwa, AICC na JINCC ni mwanachama wa Taasisi ya AIPC (The International Association of Convention Centres) ambayo inaviunganisha vituo vyote ambavyo vinatoa huduma za mikutano duniani.

“Tunaposhiriki katika mikutano huwa tunajifunza, mwaka 2019 kabla ya UVIKO-19 Afrika iliandaa mikutano zaidi ya 450, lakini mwaka 2022 iliandaa mikutano zaidi ya 200.

“Tanzania iliandaa mikutano 15 kabla ya UVIKO-19, lakini Tanzania baada ya 2022 ilianda mikutano 18, hatua ambayo ni kubwa.”

Changamoto

Mbali na hayo, Mafuru amesema kuwa, wanazidai taasisi mbalimbali zikiwemo binafsi na Serikali zaidi ya shilingi bilioni 7.4

“Taasisi na mashirika hayo zipo 20, kati ya hizo 17 ni za Serikali, hivyo tunaziomba hizo taasisi ziweze kulipa deni ili kuiwezesha AICC na JNICC kujiendesha kibiashara.”

Aidha, amesema ni vigumu kuzizuia taasisi za umma kufanya mikutano, lakini kwa upande wa zile binafsi ni rahisi, hivyo anawaomba wakurugenzi wa taasisi hizo kuwezesha madeni hayo kulipwa kwa wakati.