‘Akiba ya fedha za kigeni inaridhisha’

Waziri wa Fedha na Mipango,Dkt.Mwigulu Nchemba amesema kuwa akiba ya fedha za kigeni inaridhisha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi.

Akizungumza Bungeni,Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka 2022 na mpango wa maendeleo wa taifa wa mwaka 2023-24, Dkt. Mwigulu amesema kufikia Aprili, 2023 mwaka huu akiba ya fedha hizo ilikuwa Dola za Marekani Bilioni 4.88 ambayo inatosheleza kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 4.4.

“Mahitaji ya nchi kisheria ni kuwa na kiasi cha fedha za kigeni kinachotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa muda usiopungua miezi 4.0,” amesema Dkt. Nchemba wakati akiwasilisha taarifa hiyo ya hali ya Uchumi.

Aidha, Dkt. Nchemba amesema mwenendo wa thamani ya Shilingi ya taifa dhidi ya sarafu za nchi washirika wakuu wa kibiashara imeendelea kuwa tulivu, licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali za kiuchumi duniani hususan ongezeko la bei za bidhaa.

“Hali hii imetokana na utulivu wa mfumuko wa bei nchini ukilinganishwa na nchi washirika wetu wa kibiashara, utekelezaji wa sera thabiti za fedha na bajeti, na uwepo wa chakula cha kutosha nchini,” ameeleza Dkt. Nchemba

Dkt. Nchemba amesema katika mwezi Aprili, 2023 Dola moja ya Marekani (USD 1) ilibadilishwa kwa wastani wa shilingi 2,324.07 ikilinganishwa na shilingi 2,322.16 kipindi kama hicho mwaka 2022. Pia, katika kipindi cha kuanzia Aprili 2022 hadi Aprili 2023 Dola moja ya Marekani (USD 1) ilibadilishwa kwa wastani wa shilingi 2,310.14.