Museveni apimwa na kukutwa tena na virusi vya Corona

Rais wa Uganda Yoweri Museveni ametangaza Jumatano kuwa amepima na kupatikana tena na virusi vya Covid-19.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni apatikana tena kuwa na virusi vya Corona

Rais huyo mwenye umri wa miaka 78 alitengwa baada ya kupimwa na kukutwa na Covid mnamo Juni 7 na alipangwa kufanyiwa vipimo vua mwisho siku ya Alhamisi.

Katika taarifa yake iliyochapishwa kwenye Twitter alasiri, Museveni alisema matokeo yake yalikuwa chanya ingawa hakuwa mgonjwa.

“Sijisikii mgonjwa na nilihisi homa kidogo tu katika siku 3 au zaidi za kwanza. Vinginevyo, ninahisi kuwa tayari kuondoka kwenye hali hii ya kujitenga. Hata hivyo, leo, tena, tulifanya vipimo vya corona na bado nilikuwa na virusi, “amesema.

Kwa hivyo, Museveni amesema atafuta safari ya kidiplomasia siku ya Alhamisi unaowaleta pamoja wakuu wengine sita wa nchi kujadili vita vya Urusi na Ukraine.

“Nilipaswa kujiunga nao kesho. Sasa nimetuma ujumbe rasmi kwamba, kwa sababu ya kuendelea kwa hali yangu ya corona, siwezi kujiunga nao. Dr Rugunda atatuwakilisha. Tayari yuko Poland. Kutoka Poland, wataenda Urusi kukutana na Warusi. Naitakia misheni mafanikio,” amesema, akimzungumzia Mjumbe wake Maalum wa Majukumu Maalum.

Hata hivyo amesema ataweza kuhutubia Bunge siku ya Alhamisi wakati kusomwa kwa bajeti.

“Kwa kuwa sisafiri kwenda Kiev na Urusi, nitaweza kuhutubia Bunge kesho, kwa njia ya mtandao, Siku ya kusomwa kwa bajeti,” taarifa hiyo ilisema.