Tatizo la ajira ambalo linaendelea kusumbua nchi nyingi duniani, Tanzania ikiwemo, limegeuka kuwa ajenda kubwa katika mijadala ya aina mbalimbali. Mingi ya mijadala hii inalenga kutoa maoni juu na namna nzuri ya kukabiliana na tatizo hilo.

Ajenda kubwa hapa ni namna ya kukabiliana na tatizo hili na ikiwezekana kupunguza ukali wake kwani linaonekana kuleta shida mno. Idadi kubwa ya wanafunzi wanaendelea kuhitimu kila mwaka kwenye viwango mbalimbali vya elimu lakini wanaoajiriwa na kuingia kwenye mifumo rasmi ya ajira ni wachache mno.

Tunaambiwa hapa Tanzania kila mwaka karibia vijana 700,000 huingia kwenye soko la ajira lakini uwezo wa taifa kuajiri ukiwa chini ya watu 50,000 kwa mwaka. Kwa maana hiyo ni watu wachache sana ambao wanahitimu masomo katika ngazi mbalimbali ambao wanapata fursa ya kuajiriwa.

Watu wengi wametoa maoni yao, wakieleza mbinu ambazo wanaamini zinafaa kutekelezwa ili kupunguza tatizo hili. Mijadala mitamu sana imeibuka jinsi ya kulikomboa taifa kutoka katika tatizo hili linaloonekana kushika kasi sana hasa miongoni mwa vijana.

Katika kupitia hoja zinazotolewa na wadau mbalimbali kuhusiana na tatizo hili, nikamsikia Waziri Mkuu mstaafu, mzee wetu Mizengo Pinda, akiishauri serikali kubadili mfumo wetu wa elimu ili kuruhusu wanafunzi kujikita zaidi kwenye stadi za ufundi na ujasiriamali kuliko hali ya mfumo ilivyo sasa ambapo elimu imejikita zaidi kwenye nadharia kuliko vitendo.

Mwanafunzi anafundishwa na kumezeshwa nadharia halafu baadaye anapewa mtihani wa kinadharia na akifaulu, kwa kuwa hakuna ajira, anaambiwa aende akajiari mwenyewe!

Mzee Pinda alikwenda mbali zaidi kwa kutahadharisha kuwa si vema watoto (vijana) kudanganywa kuwa kuna ajira wakati kiuhalisia ajira ni chache mno. Hiyo ilikuwa hoja ya mzee wetu Pinda akiwa kule mkoani Songwe wakati akifunga kongamano la wawekezaji.

Hoja ya mzee wetu Pinda ni kama inakinzana na hoja ya wadau wengine mbalimbali kama Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla na Makamu Mwenyekiti wa Chama tawala, CCM, mzee wetu Philip Mangula, ambao wao kwa nyakati tofauti walijenga hoja zao kuhusu tatizo hili la ajira na namna ya kukabiliana nalo. Hawa wanawataka vijana wafikirie zaidi kwenye kujiajiri na kutafuta ‘connections’ zao kupitia elimu waliyoipata ili waweze kujiajiri.

Wakati mzee Pinda akijenga hoja ya serikali kubadili mfumo wa elimu yetu, hawa kina Kigwangalla wanafikiria zaidi kwenye upande wa vijana kufikiria zaidi kujiajiri kuliko kuajiriwa. Hawa ni kama hawajajikita sana kwenye mfumo wetu wa elimu ambao kwa wengine wanadai ndio kikwazo cha tatizo la ajira na hata kuwakwamisha vijana wanaohitimu viwango mbalimbali vya elimu kushindwa kujiajiri.

Lakini ni ukweli usiopingika kwamba, kijana au mtu yeyote kujiajiri na kutojiajiri kunaendana sana na aina na mfumo wa kumwandaa kijana au mtu huyo. Pia inategemea sana na mifumo iliyopo katika jamii kuhusiana na masuala ya ajira.

Hauwezi kutenganisha hivi vitu. Kabla hatujamtaka kijana ama mtu kujiajiri, tujiulize na kutafakari, vijana hawa wameandaliwa kujiajiri kwa tija? Je, jiko letu lililowaandaa vijana hawa lina kuni za kupika na kuwaoka vijana ili wakitoka hapo waweze kuhimili vishindo vya kujiajiri?

Kwa sababu ni jambo moja kujiajiri, lakini ni jambo jingine kabisa kuhakikisha kuwa kwanza, ajira hiyo inakuwa ni ya kudumu na pili, ajira hiyo inaleta tija na faida.

Hata kama tukiwa na mfumo mzuri wa elimu unaowaandaa vijana kujiajiri; tujiulize, kwenye soko tuna mifumo inayotengeneza fursa za watu kujiajiri?

Hivi elimu yetu inatengeneza watu wenye maarifa ya kujiajiri (job creators) au tunatengeneza vijana wanaohaha na mabahasha kuwinda ajira maofisini (job seekers). 

Kwa mfano, mfumo wetu wa elimu ulivyokaa hapa kwetu, kijana aliyehitimu masomo na kupata shahada pale UDOM au UDSM anaweza kuhangaika sana kujiajiri kuliko yule aliyemaliza na kufeli darasa la saba kisha akaenda Veta. Huo ni mfumo wa elimu.

Ni dhambi na ngumu sana kwa kijana aliyehitimu elimu ya nadharia kumtaka akajiajiri bila ya kumuwekea mazingira rafiki ya mitaji na ujuzi kufanya hicho tunachotaka akifanye.

Ajenda ya kujiajiri ni ya msingi sana hasa katika kipindi hiki ambacho idadi ya watu inaongezeka huku fursa na nafasi za ajira zikiwa zilezile au zikipungua.

Kabla ya kumsukumia kijana aende akajiajiri ni vizuri kuangalia mifumo yetu kama inaruhusu hayo tunayoyataka. Kama kijana anamaliza shahada yake huku akiwa ametumia fedha nyingi za serikali ama mzazi kusoma na mwisho anakuwa hana hata uwezo wa kupata mtaji wa kuanzisha hata banda la chips, vipi mtu huyu ataweza kujiajiri?

Bwanku ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu Dodoma na mchambuzi wa masuala ya kijamii

0657475347

By Jamhuri