Almasi ya Mwadui inavyompamba Malkia Elizabeth II wa Uingereza

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizojaaliwa kuwa na aina mbalimbali za madini na inatajwa kuwa kitovu cha madini ya vito barani Afrika.

Miongoni mwa madini hayo ya vito ni almasi. Asili ya neno ‘almasi’ kwa lugha ya Kiswahili haifahamiki vizuri, lakini Warusi hutumia neno ‘almaz’ kumaanisha ‘diamond’ kwa lugha ya Kiingereza. 

Almasi ni moja ya madini adimu yenye mvuto mkubwa kwa wavaaji wa vito tangu zama za kale. Almasi inachukuliwa na wapenzi wake kama kielelezo cha utukufu (wafalme, watawala, makuhani na watu wenye mamlaka); lakini pia ni kielelezo cha utajiri na nguvu ya kifedha kwa watumiaji wengine. 

Kwa asili yake, madini ya almasi hayana rangi (transparent with no hue); hata hivyo, kasoro katika uumbaji wake yaani mchanganyiko wa kikemikali na mpangilio usio sahihi wa atomu (chemical impurities and structural defects) husababisha uwepo wa rangi mbalimbali katika madini ya almasi. 

Uwepo wa rangi unaweza kuongeza au kupunguza thamani ya jiwe la almasi kulingana na mahitaji ya soko. Rangi zinazoongeza thamani ya almasi ni nyekundu (ndiyo adimu kuliko rangi zote), bluu na pinki. Rangi nyingine ni njano, nyeusi, kijani na kahawia.

Hapa Tanzania, mgodi pekee wenye historia kubwa ya uzalishaji almasi ni mgodi wa Williamson Diamonds Limited (WDL) uliopo Kishapu mkoani Shinyanga. Mgodi huu ambao pia unaitwa ‘Mwadui’ kwa heshima ya jina la chifu wa eneo hilo, uligunduliwa na Mjiolojia, Dk. John Williamson, katika mwaka 1940. WDL ilisajiliwa rasmi kama kampuni mwaka 1942 na Serikali ya kikoloni kwa mtaji wa hisa 400 kila moja ikiwa na bei ya £500 sawa na jumla ya mtaji wa £200,000.

Mgodi huu unasifika duniani kwa mambo mengi lakini pia ni miongoni mwa wazalishaji wachache wa almasi za rangi ya pinki (rangi adimu na inayopendwa sana duniani). Kwa kawaida, mgodi wenye umaarufu wa kuzalisha almasi za rangi ya pinki ni mgodi wa Agyle ulioko Australia Magharibi ambao hutoa 90% ya almasi zote ya pinki duniani. 

Pamoja na uwepo wa mgodi wa WDL, Tanzania pia inachimba almasi kupitia mgodi wa kampuni ya El Hillal Minerals Limited iliyopo jirani na mgodi wa WDL huko Kishapu, Shinyanga. Almasi pia zinachimbwa kwa uchimbaji mdogo katika eneo la Maganzo, Shinyanga, Mabuki mkoani Mwanza na maeneo mengine ya nchi yetu.

Almasi za pinki hupatikana katika migodi michache sana duniani na uadimu wake hufanya madini haya yatafutwe zaidi (high demand). Tanzania inasifika kwa utoaji wa almasi za rangi ya pinki katika Afrika. Almasi za rangi ya pinki hupatika kwa nadra sana. “Ukiwa na madini hayo umetukuka na wewe unakuwa miongoni mwa watu maarufu au tajiri sana,” inasemwa.  

Madini ya almasi huuzwa na kununuliwa kulingana na soko kwa vigezo vya uzito (carat), usafi wa jiwe (clarity) mkato (cut) na rangi yake (colour) maarufu kama ‘4C’s’! 

Kwa upande wa rangi, kipimo cha ubora wake hujulikana kwa kutumia mpangilio huu: kuanzia kundi ‘D’-‘N’, rangi ya juu kabisa kwa almasi inaanzia ‘D’ hadi ‘N’. Mpangilio huu unaokubalika zaidi duniana ulitolewa na Taasisi ya Jemolojia ya Marekani (Gemmological Institute of America-GIA). Taasisi hii ndiyo iliyobobea zaidi katika utambuzi na uthaminishaji wa madini ya almasi na vito duniani.

Septemba 2015, mgodi wa WDL ulibahatika tena kupata jiwe kubwa la almasi ya pinki lenye uzito wa carat 23.16. Almasi hii imeweka rekodi nyingine kwa mgodi wa Mwadui, kwani iliuzwa kwa dola za Marekani milioni 10.05 huko Antwerp nchini Ubelgiji. Hii ni rekodi mpya kwa thamani kuwahi kupatikana na kuuzwa kwa mgodi huo au mgodi mwingine wowote wa almasi hapa nchini.

Mbali na jiwe hili la carat 23.16 pinki nyingine kubwa kuwahi kupatikana katika mgodi wa Mwadui ilikuwa na uzito wa carat 54.5 ambayo Dk. Williamson alimzawadia Malkia wa Uingereza (Queen Elizabeth II) mwaka 1947 kama zawadi ya harusi. 

Jiwe hilo halikuwahi kuuzwa au kuingizwa sokoni lakini linadhaniwa kuwa ni almasi bora ya pinki kuwahi kupatikana. Pinki hiyo iliyotolewa kama zawadi kwa Malkia wa Uingereza baadaye ilikatwa na kutoa jiwe la carat 23.6 ambalo liliwekwa katika mfano wa ua (Williamson pink brooch). Pambo hili ni miongoni mwa mapambo adimu yanayopendwa kuvaliwa na Mtawala huyo wa Uingereza.

 Wananchi wanafaidika na uwepo wa madini ya almasi kwa kiasi kikubwa kwa kujipatia ajira za moja kwa moja migodini au kupitia huduma mbalimbali ikiwamo biashara na migodi husika, ajira kwenye kampuni zinazotoa huduma migodini na biashara kati yao na waajiriwa kwenye migodi inayowazunguka. Aidha, Serikali hujipatia fedha za kigeni, mapato kwa njia ya mrabaha, kodi na tozo mbalimbali kwa mujibu wa sheria. Mapato hayo yote yanasababisha uchumi wa Tanzania kuimarika.

Faida za moja kwa moja za madini hayo ni ajira. Mgodi wa Mwadui unatoa ajira za kudumu takribni 600 pamoja na ajira zisizo za moja kwa moja zaidi ya 500 kupitia kampuni zinazotoa huduma mbalimbali kwenye mgodi huo.  

Pia upo Mgodi wa El Hillal Minerals Limited uliopo wilayani Kishapu ambao unazalisha madini ya almasi. Nao unatoa ajira kwa wafanyakazi takribani 200. Kwa maana hiyo wafanyakazi zaidi ya 1,500 wanaendesha maisha yao kutokana na migodi hiyo miwili ya Williamson na El Hillal bila kuhusisha wachimbaji wadogo.

Takwimu za mwaka 2013 za Mgodi wa Mwadui zinaonesha kuwa mgodi huo ndiyo unaoshikilia rekodi ya dunia ya kuwa mgodi pekee uliochimbwa mfululizo kwa miaka 70; ndiyo mgodi mkubwa zaidi duniani unaochimbwa kwa staili ya shimo la wazi (open cast); unayo akiba ya almasi inayokadiriwa kuwa carat milioni 40; ukikadiriwa kuwa na uhai wa miaka 18 (Planned mine life). Aidha, mgodi wa Mwadui unatarajiwa kuendelea kuzalisha almasi kwa miaka mingine 50 ijayo.  

Kumbe Tanzania tuna madini ya kila aina na yenye thamani kubwa sana, na ubora wa juu. Ni vyema madini yote yanayopatikana Tanzania yakafuatiliwa kwa karibu ili Watanzania wote wafaidike na pia kupaisha uchumi wa nchi. Wachimbaji wote wakubwa kwa wadogo wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini Tanzania, ni vyema wakatoa ushirikiano kwa Serikali katika ulipaji wa kodi mbalimbali ili wananchi wa Tanzania wafaidike na madini yao.