Makulilo ni nani kwenye udhamini wa elimu ughaibuni?

N

dugu wadau wote wa gazeti la JAMHURI, nimerudi tena kuungana nanyi. Kwa wale ambao mmekuwa mnafuatilia gazeti hili makini lilipoanza, nilikuwa naandika makala kila wiki kuhusiana na masuala ya UDHAMINI WA ELIMU YA JUU UGHAIBUNI yaani SCHOLARSHIP OPPORTUNITIES. Kwa hapa katikati nilipumzika kidogo na nimerudi tena. Hivyo kila wiki nitakuwa natoa makala za mambo ya udhamini wa elimu ya juu ughaibuni na fursa mbalimbali zilizopo kwa Watanzania na watu wengineo ughaibuni na hata ndani ya Tanzania. Karibuni sana, tuungane pamoja.

Ni vyema awali ya yote nijitambulishe kiundani mimi ni nani na ninaweza kuwa na msaada gani kwako na kwa wengine ambao wamekuwa wanatafuta udhamini wa elimu ya masomo ughaibuni. Utambulisho ni muhimu sababu ndio kiini cha kufahamiana na kujua utaalamu wa watu wengine katika fani zao watoapo ushauri na maoni ya kitaalamu. 

Unapotaka kuomba ushauri kwa mtu yoyote, unashauriwa kuomba ushauri kwa mtu mwenye sifa kubwa mbili. Kama mtu hana sifa hizi mbili, ni kuwa makini nao sana maana anakuwa hana “udhu” wa kutoa ushauri kwenye sekta hiyo. 

Sifa kuu ya kwanza ya mtoa ushauri ni kwamba lazima awe ANAJUA kitu anachotolea ushauri. Kujua/uzoefu wa kitu hicho ni muhimu kwani unakuwa umebobea na kujua kitu unachoweza kuzungumza. Ni ngumu kupata ushauri sahihi wa mambo ya kiuchumi kwa mwanabaiolojia. Ni vyema kuheshimu taaluma za watu na ujuaji wao kwenye sekta husika.

Sifa ya pili na muhimu zaidi ni kwamba mtoa ushauri lazima awe na NIA NJEMA. Nia njema ni muhimu sana maana unaweza kulishwa tango pori kwa makusudi sababu mtoa ushauri japokuwa anajua mambo anakuwa hana nia njema nawe. 

Mfano huu unaweza kutoa picha ya vigezo hivi viwili vyema. Ninapotaka kusoma PhD siwezi kuomba ushauri kwa mama yangu. Mama yangu ana sifa moja kati ya hizo mbili, ana sifa ya kunipenda sana na kunitakia mafanio makubwa maishani mwangu. Lakini kwa bahati mbaya hana utaalamu na masuala ya PhD. Hivyo ushauri wake utakuwa ni wa mapenzi mema lakini hauna utaalamu ndani yake. Sasa niombe ushauri kwa nani? Nina bahati ya kuwa na kaka wawili na dada mmoja wenye PhD. Hao wana sifa zote mbili. Wana PhD, wanajua na ni wataalam wa kitu nachotaka kuomba ushauri na kubwa zaidi wana nia njema name, wananipenda na wanataka niweze name kufanikiwa. Kamwe hawawezi kunilisha tango pori hata iweje.

Sasa, Makulilo ni nani, ana sifa gani katika suala zima la udhamini wa elimu ya juu ughaibuni? Sio kwamba najisifu, la hasha. Truth to be told, Nina sifa hizi mbili. Sifa hizi muhimu katika kutoa ushauri wa mambo ya udhamini wa elimu ya juu ughaibuni. Mimi nilisoma sana, kujifunza na kuwa mtaalamu kwenye mambo ya udhamini wa elimu ya juu ughaibuni. Mimi mwenyewe ni mnufaika wa udhamini wa elimu ya juu ughaibuni. Kwa wale ambao mlikuwa hamjui, nilikuja Marekani mwaka 2008 kwa udhamini wa Fulbright uliogharimu zaidi ya dola 36,000. Huu udhamini ulikuwa wa kufundisha Kiswahili katika chuo kikuu cha Marshall kilichopo West Virginia, USA. Baada ya kumaliza mkataba wa Fulbright mnamo May 2009, nilipata udhamini wa Joan B Kroc (dola 40,000) na udhamini wa Rotary Ambassadorial (dola 24,000) kuweza kufanya master’s degree ya Peace Studies and Conflict Resolution katika University of San Diego kilichopo California, USA. Hivyo kwa muda miezi 24 kuanzia August 2008 hadi May 2010 niliweza kupata udhamini wa dola 100,000 sawa na Tsh. 210,000,000/- (Usishangae, ndio ni shilingi milioni mia mbili na kumi). Swali najua unalojiuliza ni “Is Ernest smarter than me? Is he more intelligent than me?” The answer is NO, Absolutely NOT. Ernest Makulilo is not smarter or more intelligent than you. The only thing he possesses is THE SECRET ON HOW TO PREPARE A WINNING SCHOLARSHIP APPLICATION AND BE COMPETITIVE. 

Sifa ya pili ambayo nayo ninayo ni nia njema. Kwanza ifahamike kuwa huu ni mwaka wangu wa 8 nimekuwa nawasaidia watu jinsi ya kuomba na kupata udhamini. Ushauri wangu ni BURE 100%, Sijawahi kumtoza mtu hata senti moja kupata ushauri. Na hili nadhani sifa tumpe zaidi Baba Boniface Makulilo (RIP) na Mama kwa msingi mzuri walioutoa kwa watoto wote 13 wa Makulilo.  Swali unalojiuliza kichwani kwako, “sasa huyu jamaa anaifaidika vipi au anakula na vyuo commission flani?” Silipwi na vyuo au taasisi yoyote. Taarifa nazotoa zipo kwenye google nyingi. Faida nayoipata ni FURAHA YA UKWELI TOKA MOYONI. Ninapoona mtu anafanikiwa kwa taarufa ninazotoa naona mchango wangu katika jamii. Bishop Desmond Tutu on Ubuntu anasema “A PERSON IS A PERSON THROUGH OTHER PEOPLE’S EYES”. Huu ndio mchango wangu kwa wanadamu name. Nilipata shida sana wakati natafuta scholarships. Nilikuwa naomba kipindi hicho facebook, twitter, whatsapp, instagram, viber nk hazipo. Kipindi hicho ni yahoo messenger tu na hi5 ndio mtindo mmoja. Wachache waliotoka kipindi kile walikuwa wanabana kutoa taarifa za wao waliendaje ughaibuni, nikaahidi nikitoka name nitafanya kitu tofauti. Kuanzia 2007 mwishoni hadi sasa nimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha watu wengine nao wanafaidika. Ni aibu ughaibuni Watanzania ni wachache, wengi hawataki kuchangamkia fursa tofauti na nchi zingine.

Naamini sifa hizi mbili zitakuaminisha na kukusaidia wewe unayetafuta udhamini kujua unaweza kupata. Kwanini mimi nipate wewe ukose? Huhitaji kuwa motto wa kigogo au kujuana na mtu kupata udhamini. VIGEZO NA MASHARTI HUZINGATIWA UGHAIBUNI. Kikubwa ni kufuata masharti na kuacha mawazo ya bahati nasibu na zali la mentali.

Unaweza kutembelea blog yangu ya www.makulilo.blogspot.com kwa ajili ya taarifa zaidi za udhamini lakini pia links za fursa mbalimbali za udhamini wa elimu ya juu zipo huko.

Kwa wale watu wa wajasiriamali, pia kutakuwa na taarifa zaidi za ujasiriamali, huko napo nimebobea. Unaweza kuona maelezo yangu www.ebmwholesale.com na www.instagram.com/ebmsignature 

Mada ya wiki ijayo: KWANINI WATU WANAKOSA UDHAMINI UGHAINUNI?

Nawatakia umaliziaji mwema wa mwaka 2015 na ukaribishaji mzuri wa 2016.