Wakati nchi inajiandaa kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu baadaye mwaka huu, amani ya nchi ni jambo linalotakiwa kuangaliwa kwa umakini mkubwa. 

Nchi zetu hizi zinazoitwa za dunia ya tatu, au nchi zinazoendelea, mara nyingi zimetokea kuvuruga amani yake wakati kama huu wa kutafuta madaraka ya kuiongoza nchi. Kipindi cha uchaguzi, hasa ukiwa Uchaguzi Mkuu, ni kama kipindi cha kuzitafutia kiama nchi hizi. Ni mara chache uchaguzi mkuu hupita na kuziacha nchi hizi salama.

Yapo mambo ambayo inabidi kuyaangalia kabla hatujachukua uamuzi mwingine wowote. Inabidi kujiuliza, wanaotafuta uongozi wanafanya hivyo kwa masilahi gani? Wanataka kuongoza watu kwa manufaa ya nchi au kwa manufaa yao wenyewe, kitu kinachoweza kuchukuliwa kama sehemu ya biashara yao binafsi? Sidhani kama uongozi wa nchi ungekuwa ni kwa ajili ya faida ya wananchi na nchi zenyewe, pangeweza kutokea tofauti, kwa sababu tu wagombea wanatoka katika vyama tofauti vya siasa. Hali ikishakuwa hivyo, tayari panaonekana hapo kuna upande unaotegemea kunufaika zaidi ya inavyotarajiwa.

Kwa mantiki hiyo, sitegemei mgombea afikie kutoa chochote ili kuwavutia wapiga kura wampendelee yeye zaidi ya mpinzani wake. Na kwa maana hiyo, sitegemei mambo ya chama tawala na upinzani yajitokeze. Ni kwamba vyama vyote vinavyoingia kwenye uchaguzi vinapaswa kuwa sawa kwa kila kitu.

Maana kinachotafutwa ni mamlaka, haiwezekani mamlaka hayo yakatafutwa katika uwanja ulio sawa iwapo kipo chama kingine kinachoonyesha kuyashikilia mamlaka hayo hayo yanayotafutwa. Ni lazima kuandaa mazingira ambayo yatamfanya kila anayetafuta mamlaka, akiwemo yule anayeyashikilia wakati huo, kuwa sawa, ili ushindani uwe wa haki.

Ni sawa na katika mchezo wa mpira wa miguu. Haiwezekani ushindani katika mchezo huo ukawa wa haki iwapo mmoja wa washindani ndiye mpuliza kipenga, kwa maana ya mwamuzi wa mchezo, ukategemea kupata haki yoyote. 

Hii ni kwa sababu, haiyumkini kuwa atatumia mamlaka aliyonayo ili kuhakikisha kila wakati wewe ndiye unayeotea au kufanya vurugu nyingine zinazolazimisha mpira upigwe kuelekezwa upande wako.

Hali ikiachwa iendelee hivyo, kutokana na kutotendewa haki, upande wa pili unaweza kulalamika na wakiona hata wakilalamika hawatendewi haki, hapo ndipo mwanzo wa kuvunjika kwa amani, kwani upande huo unaweza kutafuta njia nyingine za kudai haki yake.

Katika kujilinda kuhakikisha hali kama hiyo haitokei, tunatakiwa kuyaweka mambo yote katika uwazi utakaoeleweka kwa kila mwananchi. Ieleweke kwamba uongozi wa nchi, viongozi kuwapo kwenye nafasi zao ni kwa faida na manufaa ya wananchi. 

Mtu yeyote anayetafuta uongozi kwa kujaribu kumrubuni mpiga kura kiasi cha kufikia kuhonga kwa aina yoyote, huyo hafai kupewa uongozi.

Kwa sababu haiingii akilini kumrubuni mtu kwa kumhonga kwa ajili ya kitu ambacho ni kwa faida yake. Na hali hiyo ikikubaliwa, itakuwa hatutafuti uongozi ila utawala, maana atakayepatikana kwa kuhonga hawezi kuongoza, atakuwa ni mtawala tu.

Ikishakuwa hivyo, wanaotafuta uongozi wakawa watu wa kununua kura kwa kuwahonga  wapiga kura, lazima kutatokea ambao watashindwa kununua hizo kura hata kama uwezo wa kuongoza wanao mkubwa. Hao hawawezi kuridhika, hali itakuwa imechafuka.

Kama kweli tunajivunia hali ya amani tuliyonayo, inabidi tujiepushe na kitu cha aina hiyo. Tuhakikishe uongozi wa nchi hauna mwenyewe kipindi hiki tunachoelekea Uchaguzi Mkuu. Tujaribu kujiepusha na mambo ya chama tawala na vyama vya upinzani, kwa sababu unapofika wakati wa Uchaguzi Mkuu hakuna mtawala na mpinzani, wote wanakuwa sawa, kwa sababu watawala na wapinzani wote wanatafuta nafasi ya kuongoza. Kama utawala uliopo ungekuwa na haki ya kuendelea, basi kusingekuwa na haja ya Uchaguzi Mkuu, maana wanaojiita watawala wangeendelea kutawala moja kwa moja.

Unapofanyika Uchaguzi Mkuu, wote wanaoingia kwenye kinyang’anyiro hicho wanabaki kuwa wapinzani. CCM inabaki chama cha upinzani kama ilivyo Chadema, TLP, CUF na kadhalika, kwa sababu nacho kinapinga wale wengine kukabidhiwa dhamana ya uongozi.

Nayasema hayo kujaribu kuonyesha tunavyoweza kuilinda amani yetu katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu. 

Tunatakiwa tufanye kitu tunachokielewa. Tuelewe kwamba uongozi wa nchi hauna mwenyewe, kwa sababu hiyo si biashara ya mtu binafsi wala chama chochote, ila ni ya wananchi wenyewe kwa ujumla wao.

Anayejaribu kuonyesha umimi ndiye anayetakiwa kutazamwa kwa jicho kali, kwa vile atakuwa haitakii nchi yetu  majaliwa mema. Naamini kwamba hilo inabidi litoke sehemu zote, kwa wote wanaotafuta madaraka hayo.

Lengo langu ni kutaka kusema kwamba Uchaguzi Mkuu utumike kuilinda amani yetu tuliyonayo, kwa sababu tunafanya kitu chetu sote kwa pamoja, kuupata uongozi wa nchi. Atakayekwenda tofauti na makusudio ya walio wengi, kwa maana ya kutoka nje ya mstari, atakuwa ameroga kila kitu. Tunakiwa tumkemee kwa nguvu zetu zote bila kujali amesimama upande gani.

Kwa sababu, kwa uzoefu, tumekwisha kuona kuwa amani inapotoweka kinachofuata ni vurugu kwa kila mtu; vurugu haichagui mtoto wala mtu mzima. Hakuna anayeweza kujiona ni wa chama tawala au upinzani, vurugu haina macho, tujihadhari nayo.

Uchaguzi Mkuu utulindie amani yetu kwa ajili ya mustakabali mwema wa nchi yetu.

prudencekarugendo@yahoo.com

0654031701 / 0784989512

462 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!