Wiki iliyopita katika toleo hili la Uamuzi wa Busara, tulisoma jinsi wanachama wa Chama cha TANU wanavyojivunia kuimarika kwa chama chao kiasi cha kuvifanya vyama vingine vinavyokipinga kuanza kupukutika. Wiki hii ni mwendelezo wa tulipoishia. Endelea…

Kutokana na uamuzi huo alioufanya Mwalimu Nyerere wakati huo, inatudhihirishia wazi kwamba kweli alifanya kazi kubwa ya kuimarisha TANU. Wananchi wengi tangu hapo, walianza kutambua kwa uwazi kwamba kazi ya TANU haikuishia wakati ule tulipomwondoa mkoloni na kujipatia serikali yetu wenyewe; la hasha! Mwalimu alizidi kufafanua umuhimu wa kazi mpya ya TANU.

Mwalimu alipopeleka risala yake ya Uhuru kwa TANU mwaka huo 1961, aliwakumbusha Wana TANU wote kuwa, ingawaje Uhuru ulikuwa umepatikana wakati huo, lakini aliwajulisha wote nini maana ya Uhuru huo na kazi zinazotegemewa kufanywa mara baada ya Uhuru.

Akielezea kwa kutoa mfano kuwa: “Tulichokipata ni sawa kabisa na mtu aliyekuwa akililia kiwanja cha kujenga nyumba sasa amekipata. Lakini kazi ngumu iliyobaki ni kuijenga nyumba yenyewe. Na baada ya kuijenga, hapana budi kuhakikisha kwamba inaangaliwa na kutunzwa.”

Ni sawa kabisa na kumzaa mtoto. Kuzaa si kazi kubwa. Kazi ngumu ni kumtunza mtoto hadi kufikia umri wa kuweza kujimudu mwenyewe. Hii si kazi rahisi, ni ngumu.

Mwalimu baada ya kueleza yote hayo ilimbidi ayatekeleze hayo yote kwa vitendo kwa kuwaendea wananchi popote pale walipo ili watambue kazi ngumu inayowakabili wananchi na taifa zima kwa ujumla.

Kama itakumbukwa, wakati huo vyama vingi vya siasa vilikuwa vimeanza kuzuka kama vile CONGRESS; wananchi wengine walikuwa wameanza kuwayawaya na kushindwa kujua wafanye nini na vyama hivi.

Lakini chini ya uongoza wa Mwalimu Nyerere, aliweza kuimarisha imani za wananchi katika chama kilichomwondoa mkoloni (TANU).

Mwaka 1962, mwezi Desemba karibu kabisa na Tanganyika kuwa Jamhuri, wananchi wote na si Wana TANU peke yao, walimwomba Mwalimu asimamie uchaguzi wa Rais wa Jamhuri mpya ya Tanganyika.

Mwalimu wakati huo alikuwa anajishughulisha na kazi zake tu kama Rais wa TANU. Kwa uamuzi wake wa busara alikubali kupigania kiti cha urais wa Jamhuri ya Tanganyika. Alishinda kwa zaidi ya asilimia 97 dhidi ya mpinzani wake.

Cheo cha uwaziri mkuu kikatolewa tangu hapo tarehe 9/12/1962. Kawawa ambaye alikuwa waziri mkuu, akafanywa Waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu.

Tangu hapo, TANU ikaendelea kuimarika zaidi na zaidi hadi kuvifanya vyama vingine vilivyotaka kuipinga TANU vikaanza kuteketea vyenyewe kimoja kimoja.

Hakika uamuzi huu ndio tunaojivunia hadi hivi sasa, hasa tunapoona Chama chetu cha TANU kinavyoendelea kushika hatamu za kuongoza taifa letu katika misingi ile ile ya kujenga usawa na hali bora kwa wananchi wote.

Idumu TANU milele!!

Chama cha TANU (Tanganyika African National Union) kilipozaliwa kutokana na TAA (Tanganyika African ssociation) mwaka 1954 hapakuwa na chama chochote cha siasa nchini Tanganyika.

Baadaye vikundi vingine vidogo vya siasa, kama vile UTP (United Tanganyika Party) na ANC (African National Congress) vilizuka na muda haukupita vikavunjika vyenyewe.

Kwa vile TANU ilikuwa chama cha pekee humu nchini, na kwa vile hakukuwa na chama kingine chenye uzito wa kupambana nacho, kulizuka mtindo wa wajumbe waliosimamishwa na TANU kupita bila kupingwa.

Kila mjumbe aliyesimamishwa na TANU alipita bila kupingwa. Kwa mfano katika mwaka 1963 na 1964 katika idadi ya viti 365 vilivyogombaniwa katika mabaraza ya serikali za mitaa wagombea uchaguzi 350 wa TANU walichaguliwa bila kupingwa.

Mara nyingi viongozi wa TANU walifikiria kuwa na utaratibu wa serikali ya chama kimoja cha siasa humu nchini. Viongozi hao waliwahi kutoa maoni fulani fulani juu ya faida ya kuwa na utaratibu huo wa serikali ya kidemokrasia ya chama kimoja.

Baada ya kupata Uhuru, Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1962 alifafanua jambo hili kwa kauandiaka:-

“Mataifa mapya kama hili la Tanganyika yanapata uhuru wao kutokana na vita ya kutaka uhuru kuepukana na ukoloni.

Hiyo ni vita ya wananchi ambayo huunganisha pamoja watu wote katika nchi bila ya kutoa nafasi ya kutofautiana na vyama vya wananchi baada ya kuwaunga mkono watu wote pamoja na kuwaongoza mpaka kufikia uhuru, ni lazima viunde serikali huru ya kwanza katika dola zao mpya.

Mara tu baada ya serikali huru ya kwanza kwisha kuundwa serikali hiyo hukabiliwa na kazi kubwa sana – kazi ya kujenga uchumi wa nchi hii katika kuinua hali ya maisha ya watu, ya kuondosha ugonjwa, ujinga na ushirikina.

Kazi hii kuweza kufaulu yataka umoja wenye nguvu zaidi kama vile umoja wa kupigana na ukoloni. Kwa hiyo hakuna nafasi ya kugawanyika wala kutofautiana.”

Wakati Halmashauri Kuu ya Taifa ya TANU ilipofanya mkutano wake mjini Dar es Salaam kutoka tarehe 10 mpaka 14 Januari, 1963, miongoni mwa mambo yaliyozungumzwa lilikuwamo suala la uhusiano baina ya Chama cha TANU na serikali.

Wajumbe wa Halmashauri Kuu walipata fursa ya kulijadili jambo hili kwa kirefu. Baada ya majadiliano kuhusu suala hilo mkutano ulikubaliana kwamba ni muhimu kuwe na muundo mpya wa kuendesha serikali kwa namna inayopatana na kanuni za asili yetu.

Kwa hiyo, mkutano huo ulikubaliana na kumuidhinisha Rais wa Jamhuri ya Tanganyika kuunda tume maalumu itakayobuni au kutengeneza Katiba mpya ya TANU na ya serikali kwa makusudi ya kuanzisha utaratibu wa serikali ya chama kimoja cha siasa.

Kuwekwa kwa Tume ya Rais na masharti ya uamuzi vilitangazwa na Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Jamhuri ya Tanganyika tarehe 28, Januari, 1964. Rais alieleza kwamba tarehe 14, Januari, 1963 alitangaza uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya TANU kwamba Tanganyika iwe na serikali ya kidemokrasia ya chama kimoja cha siasa.

Wakati huo huo alitangaza kwamba alipewa uwezo na Halmashauri Kuu ya Taifa kuweka Tume ya Rais ambayo itapewa kazi ya kufikiria mabadiliko ya Katiba ya nchi ya Tanganyika na Katiba ya TANU, na katika maendesho ya serikali ambayo yatalazimika, kwa kuleta matarajio ya serikali ya chama kimoja cha kidemokrasia katika nchi ya Tanganyika.

Tume hiyo iliwakilishwa vya kutosheleza na watu kutoka katika TANU, vyama vya ushirika, wazee, raia wa Jamhuri wasio Waafrika na watumishi wa serikali.

Kwanza ilikuwa na wajumbe kumi na watatu. Mwenyekiti wake akiwa ni R. M. Kawawa na A. J. Nsekela akiwa Katibu wa tume hiyo.

Tarehe 26, Aprili, 1964 Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ziliunganishwa kuwa ni utawala wa Jamhuri moja. Baada ya muungano huo, rais aliwachagua wajumbe wa Tanzania wanne kutoka Zanzibar kuingia katika tume hiyo.

Kabla ya kumaliza kazi yake tarehe 9, Oktoba, 1964, tume hiyo pamoja na taifa zima vilipatwa na msiba mkubwa sana kwa kufiwa na Sheikh K. Amri Abeid, ambaye alikuwa mjumbe mmojawapo wa tume hiyo.

Rais alitoa masharti ya kuiongoza tume hiyo kwa kutayarisha hati mbili; “Maadili ya Taifa” na “Kiongozi kwa tume kuhusu serikali ya chama kimoja” na kuwapa wajumbe wa tume hiyo.

Masharti hayo yalisisitiza kuwapo kwa uhuru wa uchaguzi, uhuru wa mazungumzo na uhuru wa kulaumu, utii wa sheria na kuheshimu binadamu. Misingi ya aina hii ilikusanya mambo yote muhimu ya uhuru wa kidemokrasia.

Tume hiyo ilifanya kazi yake iliyokuwa ngumu kwa bidii sana na mwezi Aprili, 1965 ilimkabidhi Rais Mwalimu Julius  Nyerere taarifa rasmi. Taarifa ya tume hiyo ilipelekwa mbele ya mkutano wa pamoja wa Halmashauri ya TANU na Halmashauri Kuu ya Afro Shiraz uliofanyika mjini Dar es Salaam tarehe 3-5 Mei, 1965.

Baada ya kufanya mabadiliko machache ya hapa na pale, mkutano huo ulithibitisha taarifa hiyo ya Tume ya Rais.

Halikadhalika Mkutano Mkuu Maalumu wa TANU ulipofanyika tarehe 1-2 Juni, 1965 ulithibitisha taarifa hiyo.

Kutokana na mapendekezo ya Tume ya Rais, Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano na Katiba mpya ya TANU zilitungwa. Katiba mpya ya TANU ilithibitishwa na Mkutano Maalumu Mkuu wa mwaka uliofanyika tarehe 1-2

Juni, 1965, na baadaye ilithibitishwa na Bunge. Katiba hiyo ilianza kutumika kuanzia chini mpaka juu na matokeo yake yanaonekana wazi wazi.

By Jamhuri