Nikiwa mwananchi ninayeipenda nchi yangu, nimeamua kuchukua muda mfupi kumshauri Rais wangu, Dk. John Magufuli, kuhusu uendeshaji wa nchi yetu. 

Maana kama anavyoeleza yeye mwenyewe, urais ni kazi ngumu kupita kiasi. Kwa hiyo, kwa wananchi wazalendo wenye kuipenda nchi yao, ni muhimu kila wanapopata nafasi kumshauri rais nini cha kufanya ili, kwanza, kumrahisishia yeye kazi ya kutuongoza; pili, kuifanya nchi yetu izidi kumeremeta kama ilivyokuwa muda wote tangu tupate Uhuru.

Lakini ili ushauri uwe wa maana, unapaswa kujikita kwenye mambo ya msingi kama vile kuimarisha uchumi, kudumisha amani, upendo na faraja, hivyo kuifanya nchi kuzidi kuwa kimbilio la wenye upungufu wa vitu hivyo.

Tunapozungumzia utendaji wa rais tuache kutumia lugha za ajabu kama ‘atajijua’, kwa sababu hii ni nchi yetu sote. Na mambo yanapoharibika wenye kuumia na kuathirika ni sisi wenyewe. Na kadiri ninavyomuona Rais Magufuli, ni mtu wa kusikiliza maoni ya wananchi kulingana na yanavyotolewa, hivyo na mimi nikapata nguvu ya kutoa ushauri wangu.

Yanapotolewa maoni ya ukaidi anayapokea na kuyashughulikia kiukaidi, maoni muafaka anayapokea, anayashughulikia kimuafaka. Hilo limeniongoza katika aina ya ushauri nitakaoutoa na jinsi nitakavyouwasilisha.

Sababu si jambo muafaka kumkaripia Amiri Jeshi Mkuu wa nchi ambaye amepewa kila nyenzo za kuhakikisha hatetereshwi na jambo lolote kwenye nafasi yake hiyo ya kuiongoza nchi, wakati anayefanya hivyo hana hata manati. Suala kuwa si ‘atajijua’, ila tutajijua, maana waathirika ni sisi sote!

Nakumbuka Baba wa Taifa aliwahi kusema kuwa Katiba ya nchi inampa madaraka makubwa rais  – kuweza kumfanya kuwa dikteta mwenye uwezo wa kufanya mambo ambayo wala hayafikiriwi na mtu yeyote. 

Hilo hutokea kama mtu aliyepewa dhamana hiyo anakosa umakini. Kwa kuwa na yeye ni binadamu, akiwa hana dalili za Umungu, tusimfanye akafadhaika na kuukosa umakini.

Bahati nzuri Tanzania tumejaliwa kuwa na marais makini; kuanzia kwa Baba wa Taifa na wengine waliofuatia, ingawa inafahamika kuwa urais ni kazi ngumu, yenye majaribu makubwa.

Anayekuwa na wasiwasi kuhusu hilo aanze kujiangalia mwenyewe namna anavyoiongoza familia yake; mke wake na watoto na afanye hicho kuwa ni kipimo cha kuliongoza taifa zima. Kama kuna wakati mambo ya kuiongoza familia peke yake yanakwama, iweje kuliongoza taifa zima iwe kazi nyepesi?

Rais Magufuli ameonyesha kuwa anaimudu kazi tuliyomkabidhi, maana katika kipindi chake tumeshuhudia mambo mengi kutoka kwake. Ameweza kufanya uamuzi ambao kwa muda mrefu watu walidhani kuwa hauwezi kufanywa na kiongozi yeyote nchini. Lakini amekwenda mbali zaidi kwa kutekeleza uamuzi huo mgumu wa mambo ambayo viongozi waliomtangulia walishindwa kufanya.

Mfano wa kwanza, amehamisha makao makuu ya nchi kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma. Huo ni uamuzi uliotolewa na Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mwaka 1973. 

Lakini hadi mzee huyo anatutoka mwaka 1999, zaidi ya miongo miwili na nusu, uamuzi huo ulikuwa bado ni ndoto. Ni uamuzi uliofanyika na kubaki tu kwenye makabrasha!A

Ulikuwa ni uamuzi mzuri ambao kwa muda mrefu ulisubiri utekelezaji kiasi kuwa watu wengi wakaamini kuwa jambo hilo haliwezekani. Sasa amekuja mtekelezaji na kulifanya lililofikiriwa haliwezekani. Rais Magufuli ameonyesha kuwa linawezekana, tena kwa muda mfupi tu wa chini ya mwaka mmoja.

Kwa muda mrefu tangu tumejitawala tulisema nchi yetu ni maskini, kitu ambacho mimi binafsi kilinipa wasiwasi. Mara akaja Dk. Magufuli na kusema nchi yetu ni tajiri sana, na sasa utajiri huo unaonekana.

Tumeanza kufanya mambo mengi kwa utajiri wetu sisi wenyewe ambao kwa siku za nyuma tungehitaji wafadhili. Mambo mengi yanaonekana, sidhani kama kuna ambaye angehitaji yaorodheshwe yote kwa sababu yanaonekana wazi.

Kitu ambacho ninampongeza Rais Magufuli ni kule kutotaka kutumia utajiri wa nchi kujinufaisha yeye mwenyewe binafsi, kwa kisingizio kuwa nchi yetu ni maskini. Ujanja huo upo na unaweza kutekelezwa, kwa kuwa mifano ipo mingi. Nitoe mfano mmoja wa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Hiyo ni nchi iliyojaliwa utajiri mkubwa sana lakini wananchi wake ni maskini wa kutupa. Inahesabika katika nchini maskini sana duniani. Lakini hata hivyo ilikuwa nchi yenye rais tajiri sana. Rais Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu wa Zabanga, alikuwa rais tajiri ambaye hakulinganishwa na rais yeyote wa Marekani! Wakati Marekani likiwa taifa tajiri kuliko yote duniani!

Hata Dk. Magufuli angetaka kufanya hivyo angeweza, kulingana na utaratibu wa uongozi wa nchi yetu ulivyo, Katiba ya nchi, ila nafsi yake haijamtuma kufanya hivyo. 

Yeye ameona kwa nini utajiri huo asiuonyeshe kwa wananchi wote wa nchi yake? Ndipo akafanya haya tunayoyaona yakiendelea kufanyika. Pamoja na mambo yote, walau tukampongeze kwa hilo.

Isipokuwa kuna kitu kimoja bado kinamtatiza, demokrasia! Yatafanyika yote mazuri lakini lisiposhughulikiwa suala hilo, uzuri wa yote utabaki umefunikwa.

Sisi binadamu ni viumbe wenye utata mwingi. Ukitendewa hili, utatamani bora lingekuwa lile! Kinachohitajika ni pale tu mwanadamu awe amejiamulia ni kipi anachokitaka. Lakini sidhani kama atakuwa amefanyiwa kitu kizuri yeye akitamani kilicho cha ovyo, isipokuwa ni kumuachia alinganishe mwenyewe.

Pale anaponyimwa nafasi ya kulinganisha anaweza kukitamani hata kilicho kibovu, akidai ndicho bora! Ili hali isiwe hivyo, ni afadhali kumuachia akajiamulia kusudi asije kufanya uamuzi batili, akidhani amefanya kitu salama!

Nchi zote zilizopata mafanikio ya maendeleo duniani zimeligundua hilo na kuwaachia wananchi wake kufanya uamuzi wa wanachokitaka kwa kuona kuwa kinawafaa.

Nchi kama Japan, India na nyingine za aina hiyo zimetoa kipaumbele kwa demokrasia na tunaona jinsi zilivyo. Nadhani kutoruhusu demokrasia ni kitu ghali sana kwa taifa dogo kiuchumi kama Tanzania. Nguvu inayotumika kuziba demokrasia ingeweza kuwekezwa sehemu nyingine na kulisukuma mbele taifa kwa kiasi kikubwa.

Maendeleo ambayo yangepatikana kwa kuitumia nguvu hiyo katika maeneo mengine, kungezidi kumjenga Rais Magufuli na serikali yake kiasi kuwa asingehitaji nguvu nyingine kubwa kuwashawishi Watanzania kumuunga mkono, kwa sababu kila mmoja angekuwa ameona matunda ya kile kilichofanyika.

Huo ndio ushauri wangu kwa rais wetu, naomba kuwasilisha.

[email protected]

0784 989 512 / 0654 031 701

By Jamhuri