DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Mgongano wa kimasilahi na kufilisika kwa mume ni miongoni mwa sababu zinazodaiwa kusababisha kifo cha mkazi wa Vigoa, Chamazi, Mwajabu Bakari.

Mwajabu amefariki dunia kwa kuchinjwa na aliyekuwa mume wake, Naibu Ramadhani.

Akizungumza na JAMHURI, mkazi wa mtaani hapo ambaye ni mwanasheria mstaafu, Silivanus Banigwa, anasema amefanya uchunguzi na kubaini mambo kadhaa yaliyosababisha mtafaruku huo.

Anasema mwanzoni Mwajabu na mume wake waliishi vizuri na kupata watoto wawili.

“Matatizo yalianza baba alipokosa fedha kukidhi mahitaji ya familia. Mama akampa muda wa kuishi katika nyumba yao. Akamwambia hafai kwa kuwa hana kitu,” anasema Banigwa. 

Wawili hao wakakubaliana kuwa baada ya muda fulani, mwanamume angeondoka katika nyumba hiyo kama alivyotakiwa; akaomba muda atafute nauli ya kumrejesha kijijini kwao. 

“Mwajabu akaahidi kumpatia nauli hiyo, kitendo kilichopingwa na Ramadhani akisema angetafuta mwenyewe. Akapewa Julai 22, mwaka huu kama siku ya mwisho kuishi katika nyumba hiyo.

“Siku moja kabla ya siku hiyo, akafua nguo na kuzinyoosha tayari kwa safari. Wakala chakula pamoja vizuri tu, wakalala. Ugomvi ukaanza majira ya saa sita usiku. Kabla ya alfajiri, Ramadhani akafanya mauaji na kukimbia,” anasema Banigwa.

Taarifa zinasema kwamba Mwajabu aliolewa na mume wa kwanza wakaachana kwa kisa kinachofanana na cha safari hii, kufilisika.

Yeye na mume wake wa kwanza walizaa watoto watatu na kujenga nyumba, wakiishi kwa furaha na amani huko Moshi, Kilimanjaro.

“Alipofilisika, wakakosana. Mama akawa hamthamini mume wake. Wakaachana na kutimkia Dar es Salaam kuanza maisha mapya bila hata kupewa talaka. Akaanzisha mahusiano na Ramadhani ambaye sasa anatuhumiwa kumuua,” anasimulia Banigwa.

Banigwa anasema mwaka 2018, mume halisi wa Mwajabu akaja Dar es Salaam na kukuta mkewe akiwa tayari na mtoto mwingine, juhudi za kumshawishi arudi Moshi kuendelea na maisha ziligonga ukuta, akaamua kuondoka.

Maisha yalianza kuyumba baada ya kupata mtoto wa pili na Ramadhani, kipato kikapungua, Mwajabu akaenda Moshi kuuza nyumba ya familia.

“Hakumshirikisha mtu yeyote. Kukazuka mgogoro mkubwa kati yake na familia, lakini ndiyo tayari ameshauza! Akarejea Dar es Salaam na Novemba mwaka jana akanunua kiwanja. Akajenga ndani ya mwezi mmoja tu, akahamia Desemba,” anasema Banigwa.

Mafundi waliojenga nyumba hiyo wanadai kuwa Mwajabu alikuwa akiwaeleza kwamba mumewe hana kitu, ameshafilisika na kwamba nyumba ile haimhusu.

“Ndiyo maana akampa muda wa kuondoka kwa hiari walipokosana. Alitaka abaki akiishi kwa uhuru zaidi,” anasema Banigwa.

Banigwa anasema wakati Mwajabu akijishughulisha na biashara ya mamalishe, Ramadhani alikuwa mtu wa nyumbani, hana rafiki, wala hakuwa mzungumzaji.

Baba mdogo wa Mwajabu azungumza

Sadiki Ramadhani ni baba yake mdogo Mwajabu, anasema taarifa za msiba wa mtoto wa kaka yake zimemshitua sana kutokana na mazingira ya kifo chake.

“Mimi huyu mwanangu nilimwona kwa mara ya mwisho muda mrefu uliopita. Sikuwa na habari kama amehamia Dar es Salaam! Mawazo yangu ni kwamba anaishi Moshi kwa mume wake. Kwa kweli taarifa za msiba huu zimenishitua,” anasema.

Anasema mipango ya kwenda kumzika Mwajabu mkoani Tanga inafanyika na anayesubiriwa ni baba yake mzazi.

Mtoto wa Mwajabu, Helena Godwin, anasema uhusiano kati ya mama yake na mtuhumiwa wa mauaji ulianza tangu mwaka 2017 wakati wakiishi Pasua, mjini Moshi; mama yake akifanya kazi Kiwanda cha Sukari cha TPC, huku baba huyo akijishughulisha na kung’arisha viatu ‘shoeshine’.

“Mama alipoona maisha ya Moshi ni magumu, akahamia Dar es Salaam akatuacha Moshi,” anasema Helena.

Helena anasema baadaye walichukuliwa na kuhamia Dar es Salaam maeneo ya Tabata Kimanga.

“Kulikuwa na ugomvi wa mara kwa mara kati ya mama na baba. Mama alikuwa akimwambia baba kuwa hafai tena kuitwa baba kwa kuwa hawezi kuyamudu majukumu ya kulisha familia,” anasema Helena. 

Helena anasema walihamia katika nyumba yao Desemba mwaka jana baada ya mama yake kuijenga ndani ya mwezi mmoja tu.

Anasema hata walipohamia katika nyumba hiyo, ugomvi kati ya baba na mama yake ulikuwa ni wa kudumu, mama akimtaka kurudi kijijini kwa kuwa kuwapo kwake nyumbani kunamuongezea mzigo.

“Tukiwa katika makazi mapya mama alibahatika kupata sehemu ya kufanya biashara ya mama lishe akawa anauza chakula.

“Baba alikuwa anakaa nyumbani, siku moja moja tu ndiyo alikuwa anakuja na pesa kidogo na wakati mwingine mikate, anatugawia tule, akidai kuwa ndiyo amehangaika na hicho ndicho alichopata,” anasema mtoto huyo.

Anasema usiku wa siku ya tukio aliamka ghafla baada ya kusikia mtu akipiga kelele za kuomba msaada.

Alipotoka nje akamsikia mama akimwita kaka yake aitwaye Yohana, wote wakaenda kwenye mlango wa chumba cha mama yao. 

“Tulipofika tukasikia akikoroma kwa ndani. Tukagonga mlango, baba hakufungua, akasema tusubiri, alipotoka akawa kama ana wasiwasi huku akiwa amebeba mkoba wake wa nguo tayari kwa kuondoka.

“Akatuambia sasa ingieni ndani mumuone mama yenu. Tulipoingia ndani, baba alitaka kutufungia mlango. Tukapambana naye, mwishowe akatushinda nguvu. Akatoka nje,” anahadithia Helena.

Anasema alipotoka nje, wakamfuata na kuanza kumkimbiza huku wakipiga kelele za kuomba msaada. Akawashinda mbio na kupotelea gizani.

Mjumbe wa eneo hilo, Fikiri Rashidi, anasema siku ya tukio alipigiwa simu na mjumbe mwenzake, Ashura Ali, akimtaarifu kuwapo kwa mauaji katika eneo lake.

“Nikaenda nyumbani na kuwakuta watoto wanalia. Nikaingia ndani na kumkuta Mwajabu akiwa amechinjwa na tayari ameshafariki dunia na kisha nikatoa ripoti polisi,” anasema. 

By Jamhuri