Askofu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Martin Shao, amepinga amri ya Mkuu wa Wilaya (DC) ya Moshi, Kippi Warioba, kuzuia ujenzi wa barabara vijijini katika Jimbo la Vunjo.

Barabara hizo zinajengwa kwa nguvu za wananchi kwa kushirikiana na Taasisi ya Maendeleo Vunjo (VDF).

Askofu Shao ambaye ni Mwenyekiti wa VDF, amewambia waandishi wa habari kwamba hatua hiyo ya mkuu wa wilaya inakinzana na msimamo wa Rais John Magufuli anayesisitiza maendeleo kwa kusema hayana chama.

Amesema wananchi wa Vunjo bila kujali itikadi na dini zao wameamua kwa hiari kuchangia maendeleo kupitia makongamano, mikutano ya vijiji na kupitia vikao vya kamati za maendeleo za kata zote 16 za jimbo hilo.

Katika kongamano la tatu la maendeleo shirikishi lililofanyika Julai 23, mwaka huu ambako mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, alibariki ujenzi na ukarabati wa barabara hizo.

Askofu Shao anasema Mkuu wa Mkoa, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) walimwelekeza Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kusimamia mradi huo. Ujenzi ulianza Julai 28, mwaka huu.

Awamu ya kwanza wa ujenzi ulianzia barabara ya Marangu – Mshiri – Masia na baadaye barabara ya Babylon – Rengoni hadi Masia; zote zikiwa na urefu wa kilometa 8.8.

Awamu nyingine ilihusisha barabara ya Samanga – Sembeti – Mengeni ambazo zote zipo katika Kata ya Marangu Mashariki. Ujenzi ulianza Septemba 27,  mwaka huu.

Askofu Shao anasema kwa sababu ambazo hawazijui, Oktoba 8, mwaka huu DC alizuia ujenzi na kuamuru Mwenyekiti wa Kijiji cha Sembeti, Liberath Ngaseko awekwe rumande kwa saa 48.

“Wana Vunjo tuna alama yetu nayo ni furaha, amani, upendo na mshikamano na licha ya tofauti zetu za kisiasa na kidini, lakini tumeamua kwa pamoja kuifanya Vunjo kuwa mahala salama pa watu kuishi kwa amani na upendo,” anasema.

Anasema wananchi wa Vunjo wana nia, uwezo na sababu za kujiletea maendeleo kwenye eneo lao – akirejea kauli ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyoitoa wakati wa vita dhidi ya nduli Idi Amin.

Mashtaka Mahakama Kuu

Bodi ya Wadhamini ya VDF ilikutana Oktoba 30, mwaka huu na kuziteua kampuni mbili za uwakili na kumfungulia mashtaka mawili DC huyo katika Makahama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi na Dar es Salaam. Mawakili hao ni Mohamed Tibanyendera wa Star Chambers Advocates; na Harold Sungusia na Hardson Mchau kutoka Kampuni ya uwakili ya Sung Consultants.

Katika shauri la kwanza la madai namba 39/2018, VDF na wananchi wa vijiji vya Sembeti na Mshiri wanamdai DC Warioba fidia ya Sh bilioni 2.044 kutokana na hasara iliyosababishwa na yeye kusimamisha ujenzi wa barabara.

Wakili Sungusia anasema shauri jingine lipo katika Makahama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ambako wananchi wa Sembeti na Mshiri wanaiomba mahakama imzuie DC huyo na mawakala wake kuingilia maendeleo ya wananchi kinyume cha sheria.

JAMHURI limeona barua ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi inayozuia uchangiaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara katika Jimbo la Vunjo. Miongoni mwa sababu za uamuzi huo inatajwa kuwa ni akaunti inayotumika kutomshirikisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi.

“Katika barua yako ya kuomba mchango, umeandika anayetaka ufafanuzi anaweza kuwasiliana na ofisi ya mradi iliyopo Himo, hii inathibitisha watendaji wa vijiji na kata hawajashirikishwa, wananchi wanatakiwa kupata maelezo ya shughuli hiyo katika ofisi za tarafa, kata na vijiji; si katika ofisi zenu,” inasema barua hiyo.

Barua hiyo iliyoandikwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Moshi, L.J. Maufi na kunakiliwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, inafuta barua iliyotolewa na DC Warioba ya Novemba 28, mwaka jana iliyotoa ruhusa ya michango ya ujenzi wa barabara hizo.

“Kutokana na kasoro zilizojitokeza, taratibu na maagizo ya wilaya kutofuatwa, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ameagiza nikujulishe kuwa amefuta kibali cha kuchangisha, hivyo [kazi] zoezi la uchangishaji fedha na vifaa lisimame mara moja hadi hapo kutakapotolewa maelekezo mengine,” imeandikwa.

DC amezungumza kwa ufupi juu ya hatua ya ofisi yake kufuta kibali hicho akisema taratibu zimekiukwa ikiwa ni pamoja na wanaotekeleza miradi hiyo kutokuwa na vibali kutoka mamlaka husika na taasisi hiyo kutotambuliwa na ofisi yake.

Please follow and like us:
Pin Share