Benki Kuu yaichunguza BOA

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeanza kuichunguza Benki ya BOA ambayo Gazeti la JAMHURI limeandika kwa wiki mbili mfululizo kuelezea jinsi inavyochezea dhamana za wateja, JAMHURI limeelezwa.

Wateja wengi wa BOA wamejitokeza na malalamiko ya aina mbalimbali dhidi ya benki hii yenye kuonyesha ukiukwaji mkubwa wa Sheria ya Benki na Maduka ya Fedha ya Mwaka 2006, ikiwamo kuwaongezea wateja riba nje ya makubaliano ya kimkataba, kukata fedha za wateja kwenye akaunti zao bila makubaliano wakidai wamewalipa madalali wa kukusanya madeni, kutumia hati za wateja waliomaliza mkopo kukopea mikopo mingine na madai mengine mengi.

“Baada ya habari yenu kutoka, Benki Kuu ya Tanzania imeona ni lazima ichunguze suala hili. Kwa mujibu wa Sheria ya Benki na Maduka ya Fedha ya Mwaka 2006, BoT ndiye mdhibiti wa biashara ya benki na maduka ya fedha.

“Ni kwa msingi huo BoT inalinda masilahi ya wateja na kuhakikisha benki hazipotezi haki yake. Kitu mlichokiandika kimetushtua mno. Ikiwa ni kweli kuwa BOA wanaweza kutumia dhamana ya mteja ambaye hakutoa idhini kumkopesha mteja mwingine mikopo mitatu, basi hii itakuwa ni hatari. Tanzania ya sasa haiwezi kwenda hivyo.

“Lakini pia lazima tujiridhishe kuwa wateja hawafanyi ujanja ujanja kuzamisha benki kwa kutumia mbinu zisizo halali kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu. Yote haya tutayachunguza na ukweli utajulikana,” amesema ofisa mmoja wa Benki Kuu aliyeomba asitajwe gazetini.

Kinachoshindaniwa ni Benki ya BOA kubomoa nyumba tano za Jimmy Mwalugelo anayedaiwa kuwa alimdhamini Rose Miago Asea kupata mkopo kutoka benki hiyo kwa kutumia hati yake kati ya mwaka 2011 hadi 2015.

Mwalugelo ameliambia JAMHURI kuwa yeye hajawahi kumdhamini na wala hamfahamu Rose Asea, hivyo Benki ya BOA imetumia vivuli vya mkopo alioomba mwaka 2011, lakini akakataa kuuchukua baada ya kudaiwa rushwa ya Sh milioni 24.

“Mimi nilikuwa mteja wa muda mrefu wa BOA. Nasisitiza baada ya kuwa wamenizungusha kwenye mkopo nilioomba niliwambia wanipe nyaraka zangu. Wakanirejeshea. Mwanzoni walikuwa wamezihitaji kwa ajili ya kuhakiki uhalali wa mali. Leo wanasema nilimdhamini huyo Rose, kwa kutumia nini? Hati yangu ipo kwenye taasisi ya serikali ilikowekwa kama dhamana, sasa wao wametumia hati ipi?” amehoji Mwalugelo.

JAMHURI limepata taarifa za uhakika kuwa BOA wanadai walimkopesha Rose kwa dhamana aliyoiweka Mwalugelo mwaka 2011, lakini uchunguzi unaonyesha kuwa mwaka 2012 ndipo BOA walipata hati ya nakala inayoonyesha kuwa Mwalugelo alipoteza hati yake, hivyo Wizara ya Ardhi ikampa nakala halisi ya hati.

“Benki wanayo maswali ya kujibu. Walimpaje mkopo Rose mwaka 2011 wakati Mwalugelo akiwa hati yake imepotea? Mimi nasisitiza, hati ipo na ninayo. Sasa waeleze wao ni hati ipi hiyo waliyonayo,” ameongeza Mwalugelo.

Kutokana na utata huo, Unosye Mwalugelo (mke wa Mwalugelo) alifungua kesi Na. 441 ya mwaka 2016 dhidi ya Rose Miago Asea, Bank Of Africa (T) LTD na Mabunda Auctioneer Mart Co. LTD. Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Catherine A. Kiyoja, alitoa zuio la muda (Interim Order) kwa wadaiwa kutoshikilia na kuuza nyumba katika kiwanja Na. 671/1, 682/1, 698/1, Block ‘C’ Ukonga, eneo la Stakishari Desemba 16, 2016.

Hata hivyo wakati kuna zuio la mahakama, Machi 22, mwaka jana Benki ya BOA waliuza viwanja hivyo kwa Yusuf Omary na kubadilisha umiliki. Mei 22, mwaka jana kesi aliyofungua Unosye ilitupwa kwa maelezo kuwa Mahakama ya Wilaya ya Ilala kwa mujibu wa Kifungu cha 4 cha Sheria ya Mahakama ya Ardhi, kinainyima Mahakama ya Ilala mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Baada ya kutupwa kwa kesi hiyo, Jimmy Mwalugelo alifungua kesi Na. 152 ya 2017 katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala dhidi ya Rose Asea, Bank Of Africa (T) LTD na Mabunda Auctioneers Mart Co. Ltd akiiomba mahakama itoe amri ya upande mmoja (Ex-Parte Drawn Order) baada ya amri ya kwanza iliyowazuia mdaiwa wa 2 na 3 kushikilia na kuuza nyumba za mlalamikaji zilizopo katika viwanja namba 660/1, 662/1, 696/1 na 698/1, Block ‘C’ eneo la Ukonga Stakishari hadi shauri la msingi litakaposikilizwa.

Juni 2, 2017, mahakama ilitoa amri nyingine ya kuwazui mdaiwa wa 2 na 3 kushikilia na kuuza nyumba hizo ambayo ilikuwa inafikia kikomo Septemba 3, mwaka jana, lakini walalamikiwa tayari walikuwa wameuza nyumba za Mwalugelo. Julai 28, mwaka jana hati ya Mwalugelo ilibadilikishwa na kuwa mali ya Yusuf Omary. Omary alilipa fedha alizonunua nyumba hizo kwenye akaunti ya Asea aliyeshindwa kulipa mkopo.

Mnunuzi wa nyumba hizo, Omary amezungumza na JAMHURI na kuthibitisha kuwa nakala za malipo lilizonazo gazeti hili ni halisi, kwani  alielekezwa na BOA kulipa kupitia akaunti hiyo ya Asea na kwamba yeye alikuwa mshindi wa pili wa mnada wa kuuza nyumba za Mwalugelo.

Omary amesema hamkumbuki mshindi wa kwanza wa mnada huo, wala kampuni iliyokuwa imeendesha mnada. Mwalugelo ameeleza kuwa hajawahi kusikia tangazo lolote la kupiga mnada nyumba zake.

Mwalugelo amelieleza JAMHURI kuwa kutokana na nguvu asiyojua BOA wanaipata wapi, hakuna kesi yoyote ya msingi aliyoifungua yeye au mkewe iliyowahi kusikilizwa na mahakama zaidi ya mahakama kutoa amri dhidi ya walalamikiwa na kupuuzwa. Kesi ya msingi iliyokuwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala iliondolewa na mlalamikaji baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa mahakimu, akaihamishia Mahakama Kuu na kusajiliwa kwa Na. 701 ya 2017.

Katika kesi hiyo BOA walibanwa mahakamani. Walimweleza Jaji Moses Mzuna wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuwa walikwishauza nyumba hizo kwa Yusuf Omary, hivyo mlalamikaji alitakiwa kufungua kesi upya akimwongeza mnunuzi wa nyumba hizo miongoni mwa wadaiwa.

Mlalamikaji alifungua kesi upya Mahakama Kuu liliyopewa Na. 802 ya 2017 iliyomuunganisha mnunuzi wa nyumba hizo kama mdaiwa wa nne. Hata hivyo, wakati shauri bado halijasikilizwa Benki ya BOA walibomoa nyumba zote tano likiwemo Kanisa la Moravian, zilizokuwemo katika viwanja vyenye nakala ya hati ililiyokuwa benki na Jaji Mzuna alieleza kuudhiwa na kitendo hicho.

Akitoa uamuzi Oktoba 18, mwaka jana, Jaji Mzuna alisema mahakama haikutoa baraka zozote kwa walalamikiwa kujichukulia uamuzi na kupoteza hadhi ya utendaji wa mahakama. Alisema nyumba hizo ndizo zilikuwa zinalalamikiwa hivyo BOA walipaswa kusubiri uamuzi wa mahakama kabla ya kufanya jambo lolote hata kama haikuwapo amri ya zuio kwa kuwa kesi ilikuwa inaendelea mahakamani.

Hukumu ya Mahakama ya Biashara

Benki ya BOA ilifungua kesi Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara dhidi ya Rose Assea iliyopewa Na. 138 ya mwaka 2017, ikimdai Sh milioni 101.6561 kwa kuisababishia benki hasara na kulipa gharama za kesi husika.

Benki ya BOA ambayo katika shauri hilo ilikuwa ndiye mlalamikaji, iliiambia mahakama kwamba kwa nyakati tofauti mwaka 2011, 2014 na 2015 Asea alipewa mkopo wa Sh milioni 100, Sh milioni 200, na mkopo mwingine wa Sh milioni 200 ikiwa ni mtaji wa kufanyia biashara za jumla za kuuza nguo na mikoba kutoka nje.

Wakiwa katika Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara, BOA walidai kwamba dhamana ya mikopo hiyo kwa mteja wao huyo ni hati ya viwanja namba 662/1, 662/1 na 698/1, Kitalu ‘C’, Ukonga Stakishari, Ilala, jijini Dar es Salaam, ambavyo vinamilikiwa na Jimmy Mwalugelo.

BOA walidai kuwa mteja wao huyo alitakiwa kulipa mkopo wake wa mwisho na riba kufikia Aprili, 2016 kulingana na makubaliano waliyoafikiana naye.

Katika shauri hilo BOA inasema Aprili 4, mwaka juzi ilimpa notisi ya siku 60 mdaiwa wao, notisi hiyo ilimtaka mdaiwa kulipa mkopo, lakini hakufanya hivyo na baadaye wakatoa notisi nyingine ya siku 14 kwamba watauza dhamana iliyowekwa kwa ajili ya mkopo, bado hakulipa.

Pamoja na ushahidi uliotolewa kwa upande wa mlalamikaji na hukumu kutolewa kwa upande mmoja (Ex-Parte Judgment) Jaji wa Mahakama Kuu, A. R. Mruma, aliyekuwa anasikiliza shauri hilo alitupilia mbali madai ya BOA akiyataja kuwa ni ya ajabu na yenye hila ndani yake.

“Ni wakati mwafaka kwa mabenki kufahamu kwamba wanapoamua kutumia mamlaka yao ya kuuza mali zilizowekwa dhamana kwa mujibu wa mkataba, na uuzwaji wa dhamana kushindwa kufikia gharama halisi aliyokopeshwa mteja, hawawezi kuja mahakamani kudai kwamba hawakupata kiwango cha fedha walichotakiwa kulipwa na kuomba kuuza kwa mnada mali nyingine za mdeni.

“Mali pekee zilizowekwa kama dhamana ndizo zitumike kurejesha fedha kwa mujibu wa mkataba wa mkopeshwaji. Hivyo shauri hili la kibiashara Namba 138 la mwaka 2017 limetupwa,” inasema hukumu ya Jaji Mruma.

Nyumba zavunjwa

Wakati kwa kawaida mkopaji akishindwa kulipa deni nyumba huwa zinauzwa, kwa Mwalugelo imekuwa tofauti. Nyumba tano likiwemo Kanisa la Moravian zilizokuwa katika kiwanja kinachodaiwa kuwa hati yake ilitumika kama dhamana zimebomolewa na BOA, Oktoba 17, mwaka jana, majira ya saa 10 alfajiri. Nyumba hizo zilikuwa na wapangaji 12 wakiwemo watoto wa Mwalugelo na vitu vyote vilivyokuwemo katika nyumba hizo viliibwa na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh bilioni 3.

Baada ya ubomoaji wa nyumba hizo, alifungua tena shauri Na. 940 ya 2017 akijumuisha gharama za mali na wapangaji 12, lakini shauri hilo pia lilitupiliwa mbali na Jaji Mzuna kwa kutaka kesi ya msingi iendelee na gharama zote za mali zilizoharibiwa zitafuata baadaye. Hadi sasa hakuna kesi iliyosikilizwa.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI unaonyesha kuwa maofisa wa benki hiyo walitumia vivuli vya hati hiyo kumkopesha Asea mkopo wa Sh milioni 100 mwaka 2011, Sh milioni 200 mwaka 2014 na Sh milioni 200 mwaka 2015 wakati mmiliki wa hati hiyo akiwa hafahamu kinachoendelea. Hii ilikuwa baada ya kuwakatalia baadhi ya maofisa wa BOA rushwa ya Sh milioni 24.