GEITA

Na Antony Sollo 

Siku chache baada ya Mbunge wa Sengerema, Khamis Tabasamu (CCM), kuanika kisa cha kutishiwa kuuawa, ni vema tukatafakari kwa kina sababu za kutokea hali hiyo.

Akiwa bungeni wiki iliyopita wakati akichangia Bajeti ya Wizara ya Nishati, Tabasamu aliibua madai kwamba baada ya kushauri uwekaji wa vinasaba kwenye mafuta ufanywe na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), alipigiwa simu za vitisho.

Baadaye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, akakiri kupata taarifa hizo akisema: “Jeshi la Polisi linazifanyia kazi; linaendelea kufuatilia uhalisia wa madai hayo.”

Simbachawene ametoa onyo kali akitaka waliotoa vitisho kuacha mara moja.

“Kama kweli jambo hilo lipo, waache mpango huo kwani si tu unakiuka misingi ya amani na usalama, bali unaingilia uhuru wa wabunge kutoa maoni yao kwa masilahi ya taifa na wananchi,” anasema Simbachawene.

Akizungumza katika viwanja vya Bunge, Tabasamu anasema alipigiwa simu za vitisho baada ya kuzungumzia umuhimu wa fedha nyingi zinazolipwa kwa kampuni binafsi kwa ajili ya kuweka vinasaba kwenye mafuta, akitaka ziende kwenye taasisi za serikali.

“Wanadhani ninapanga kuanzisha mapambano nao. Nimewahi kuleta hoja bungeni kwamba suala hili (la kuweka vinasaba kwenye mafuta) linatakiwa kufanywa na taasisi ya umma, si kupewa mtu binafsi. Ni gharama kubwa sana.

“Sasa ninafikiri Spika amenielewa. Inabidi kuharakisha. Ametoa maelekezo sheria iletwe bungeni haraka, ndani ya siku 30, tuipitishe ili sasa uwekaji vinasaba iwe kazi ya taasisi ya serikali,” anasema Tabasamu.

Anaitaka serikali itengeneze vinasaba vyake badala ya kutegemea vinasaba kutoka nje, akionya kuwa ni hatari kubwa kumpa kazi mtu binafsi ambaye hata hajulikani kufanya kazi hiyo, kwa hoja kwamba vinaweza kutumika kukwepa kodi.

Kauli zake ndani ya Bunge zikasababisha simu za vitisho na tayari amekwisharipoti Polisi na Ofisi ya Spika.

Spika ameahidi kulifuatilia, huku Simbachawene pia akifuata nyayo za Spika; kulifuatilia suala hili kwa karibu ili kupata taarifa ni akina nani wametoa vitisho hivyo.

Utata unabaki kuwa; madhumuni yao yalikuwa nini hasa?

Wakati wa utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ili mtu awe kiongozi wa kisiasa ni lazima atenganishe biashara na siasa.

Hiki kilikuwa kipimo cha kuona nani atakuwa mwakilishi bora wa wananchi. Leo hii baada ya kubadilishwa kwa kanuni na taratibu za nani awe kiongozi, tumeshuhudia wabunge wengi wakiwa pia ni wafanyabiashara, hususan biashara ya mafuta; ambayo ni kitovu cha ustawi wa maisha ya watu.

Nionavyo mimi, Mbunge wa Sengerema, Tabasamu, amejaribu kuonyesha ujasiri na uzalendo kwa taifa.

Inashangaza kushuhudia kuwapo ongezeko kubwa la bei ya mafuta tangu pale tuliposhindwa kudhibiti mfumo wa kisiasa kutenganisha na biashara.

Leo ni nani atatoka kutetea wananchi wanyonge wapate nafuu ya maisha kama si viongozi walioko bungeni? Hawa wanapaswa kudhibiti mfumko wa bei za bidhaa hii muhimu, mafuta.

Kwa mujibu wa maelezo ya Tabasamu, vinasaba huwekwa kwenye mafuta yanayotumika nchini ili kuyatambua yaliyolipiwa kodi. Mafuta yasiyo na vinasaba ni yale yanayopita (in transit) kwenda nje ya nchi na hayalipiwi kodi.

Tabasamu ameweka wazi kuwa mauzo ya mafuta ya petroli kwa siku ni lita milioni 12 na kampuni moja (bila kuitaja jina) iliyopewa kazi ya kuweka vinasaba, inatoza Sh 14 kwa lita; yaani ni zaidi ya Sh milioni 168 kwa siku!

Maana yake kwa mwezi kampuni hii hupata kati ya Sh bilioni 5 hadi 6.

Tabasamu, Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini, anasema ndani ya kamati walibaini kuwa kampuni iliyopewa kazi kwa miaka sita imepata zaidi ya Sh bilioni 400 na mkataba wake umemalizika.

Anasema shida iliyopo ni Tanzania kugeuzwa dampo la mafuta yasiyolipiwa kodi, kwa kuwa yanayotakiwa kupitia kwenda nje ya nchi huishia mipakani na kurejeshwa kuuzwa nchini.

“Sasa wengi walikuwa wanafanya ‘dumping’, wanagonga zile karatasi zao katika mipaka ya Rusumo, Mutukula, Kabanga na Kigoma au Tunduma na Kasumulu,” anasema Tabasamu. 

Akithibitisha kutokuwapo kwa miiko ya uongozi pamoja na mgongano wa kimasilahi, Tabasamu anasema vitisho anavyopata vinatokana na kuonekana anataka kuzuia ulaji wa watu kwenye eneo hilo, huku akiwalaumu baadhi ya wakurugenzi wa taasisi za serikali na wabunge kuwa si wazalendo.

“Hoja yangu ilikuwa ni kuja kuzuia ulaji wa watu, kwa sababu kama mtu anapata Sh milioni 168 kwa siku, hii ni hatari sana kama kazi inatishiwa kuondolewa. Kibaya zaidi mkataba wao ulikwisha mwaka jana,” anasema.

Kwa ujumla nimefurahishwa na msimamo wa mbunge huyu ambaye anatamka wazi kuwa pamoja na vitisho hivyo hawezi kubadili msimamo wake.

“Kama nilikuwa ninakwenda msikitini kuswali, nitakwenda bila hofu. Kama nilikuwa ninakwenda kufanya shughuli zangu zozote, nitakwenda bila hata matatizo, kwa sababu anayelinda uhai wangu na kuudhibiti ni Mwenyezi Mungu peke yake, kwa hiyo binadamu hawezi kulinda maisha yangu.

“Ila tu kibinadamu lazima kuchukua tahadhari. Na hao wanaojaribu kunitisha na wao wasidhani kwamba Tabasamu ni mtu wa kawaida.

“Tahadhari za kibinadamu zipo, lakini tunaviachia vyombo vya dola. Vyombo vya dola viko kazini vinashughulika na hawa watu kwa sababu walitumia simu zao kunipigia mimi na watu wa ‘cyber’ wanaendelea kufanya kazi,” anasema.

1596 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!