Na Eleuteri Mangi, JamhuriMedia, Arusha

Maandalizi ya michuano ya michezo ya Mei Mosi 2024 yanaendelea jijini Arusha ikiwemo kuweka vizuri mazingira ya Uwanja wa Sheikh Amri Abeid tayari kwa maadhimisho ya Sherehe  hizo.

Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Bw. David Lyamongi wakati akifungua  kikao cha Maandalizi ya Mashindano hayo kinachohusisha viongozi wa klabu za michezo za wizara, idara, taasisi, wakala za serikali na makampuni binafsi,  yanayotarajiwa kufanyika jijini humo kuanzia Aprili 16 – 30, 2024 na kusisitiza kuwa Arusha ipo salama tayari kwa mashindano hayo.

“Arusha inapokea wageni wengi, tunashukuru ujio wenu tubadilishane uzoefu wa kazi, mnatuongezea mapato katika mkoa wetu, wananchi wa mkoa huu unanufaika na uwepo wenu. Mtembelee mbuga za mkoa wetu wa Arusha na mkoa jirani wa Manyara katika Hifadhi za Taifa za Ngorongoro, Manyara na Arusha ili kufanya utalii wa kutembea kwa miguu, magari na kupiga picha na wanyama wakiwemo nyati” amesema Bw. Lyamongi.

Bw. Lyamongi amewahimiza wanamichezo kuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Filamu ya Royal Tour ambayo imesaidia kuleta watalii wengi kutoka maeneo mbalimbali hatua inayopelekea hoteli nyingi za jijini hapo na kwenye maeneo ya utalii kujaa mapema.

Aidha, Bw. Lyamongi amewapongeza viongozi hao wa vilabu kwa kusimamia michezo na kuwasisitiza waziandae vizuri timu hizo ili kuongeza hamasa na ushindani katika mashindano hayo kwa kuleta tija kwa watumishi wenyewe kwenye utendaji kazi wao na taifa kwa ujumla.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo ya Mei Mosi Taifa Bi. Roselyne Massam amesema kamati hiyo inaendelea na maandalizi ya Michezo ya Mei Mosi 2024 itakayofanyika jijini Arusha.

“Sisi viongozi wa Kamati ya Michezo ya Mei Mosi tumejipanga vizuri kwa kufanya maboresho  kulingana na tathmini ya michezo ya 2023, tutazingatia kanuni zetu, marefa na wasimamizi wa michezo kwa kuja na mkakati wa kutumia watu ambao wana weledi na mahiri katika mchezo husika ili kusimamia vizuri michezo yetu” amesema Bi. Massam.

Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa kikao hicho, Bi. Mary Thomas Mwenyekiti wa Klabu ya Mwanga DC amesema ushiriki wa wanawake katika mashindano hayo utaongezeka ikizingatiwa taasisi zitakazoshiriki  zitaongezeka hatua inayotoa fursa watumishi wa Serikali za Mitaa kushiriki hatua inayoleta umoja, ushirikiano, afya njema, kutoa msongo wa mawazo na kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yao ya kazi wanazofanya kila siku. 

Michezo ya Mei Mosi inaundwa na mashirikisho manne ya michezo ya watumishi kutoka Shirikisho la SHIMIWI, SHIMUTA, SHIMISEMITA na BAMMATA.

4 hours ago

Share

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Bw. David Lyamongi akifungua  Kikao Kazi  cha Maandalizi ya Mashindano ya Mei Mosi 2024 kinachohusisha viongozi wa klabu za michezo za wizara, idara, taasisi, wakala za serikali na makampuni binafsi,  yanayotarajiwa kufanyika jijini Arusha kuanzia Aprili 16 – 30, 2024.

Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo ya Mei Mosi Taifa Bi. Roselyne Massam akimkaribisha Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Bw. David Lyamongi (hayupo pichani) kufungua Kikao Kazi  cha Maandalizi ya Mashindano ya Mei Mosi 2024 kinachohusisha viongozi wa klabu za michezo za wizara, idara, taasisi, wakala za serikali na makampuni binafsi,  yanayotarajiwa kufanyika jijini humo kuanzia Aprili 16 – 30, 2024.

Katibu wa wa Kamati ya Michezo ya Mei Mosi Taifa Bw. Alex Temba akitoa taaarifa ya mashindano ya Mei Mosi 2023 kabla ya ufunguzi wa Kikao Kazi cha Maandalizi ya Mashindano ya Mei Mosi 2024 kinachohusisha viongozi wa klabu za michezo za wizara, idara, taasisi, wakala za serikali na makampuni binafsi, yanayotarajiwa kufanyika jijini humo kuanzia Aprili 16 – 30, 2024.

 Baadhi ya wajumbe wa Kikao Kazi cha Maandalizi ya Mashindano ya Mei Mosi 2024 kinachohusisha viongozi wa klabu za michezo za wizara, idara, taasisi, wakala za serikali na makampuni binafsi wakifuatilia ufunguzi wa kikao hicho cha maandalizi ya michezo ya Mei Mosi inayotarajiwa kufanyika jijini Arusha kuanzia Aprili 16 – 30, 2024