Asante Rais Samia kushiriki Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari

Na Deodatus Balile, Arusha

Wiki hii nimerejea katika ukumbi huu. Msomaji wangu niwie radhi sikuweza kuandika katika wiki mbili zilizopita, kwani nilikuwa na maandalizi mazito ya mkutano mzito ulioileta Afrika Tanzania. Huu si mwingine, bali ni mkutano wa Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (WPFD) uliofanyika Arusha, Tanzania.

Sitanii, naomba kuchukua fursa hii kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan. Siku hii Mei 3, 2022 imeadhimishwa siku iliyokuwa na ratiba ngumu mno kwa Rais. Ilikuwa ni siku ya Eid el Fitr, hivyo Rais alilazimika kuswali kwanza Swala ya Idd Dar es Salaam, baadaye akaja Arusha kufungua mkutano wa Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani ambayo kwa Afrika imeadhimishwa Tanzania na jioni akahudhuria Baraza la Eid Dar es Salaam.

Kwa hakika tumeiona faida ya usafiri wa uhakika, yaani matumizi ya ndege. Ingekuwa magari, nakuhakikishia Rais asingeweza kufanya ziara hizi zote akazikamilisha kwa wakati. Na hii niongezee. Ndiyo maana napingana na wanaomshutumu Waziri Nape Nnauye kwa kutumia helikopta katika kukamilisha mradi wa anwani za makazi.

Umefika wakati sasa viongozi wa kitaifa watumie helikopta au ndege. Kwa mawazo finyu tunaweza kudhani wanapata raha, si kweli. Fikiria kwa mfano Rais ana mkutano Kilimanjaro asubuhi, na jioni anapaswa kuwa Mpanda. Tukiwaza kwa ufinyu, litatolewa jibu la haraka kuwa haiwezekani, lakini tukitumia ndege na helikopta ni jambo la kawaida. Marekani wanafanya hivyo, na hata majirani zetu Kenya mawaziri wanatumia helikopta.

Ukimwambia mtu kuwa helikopta inapunguza gharama, utabishiwa. Lakini fikiria msafara wa magari, muda unaopotea barabarani na hatari za ajali zilizopo. Waziri Nape usife moyo, najua unashambuliwa kwa kutumia helikopta, lakini kila jambo lazima liwe na wa kulianzisha. Katika hili umeonyesha njia na si muda mrefu wengine watafuata. Mjadala huu una sura nyingi, wapo wanaolizwa na posho kwa kuwaza kuwa wakitumia magari idadi ya siku za safari inaongezeka, lakini kwao ufanisi na uchovu hawayafikirii.

Sitanii, nimeligusa la Nape baada ya kuona nchi inaacha mambo makubwa inajadili vitu visivyoongeza tija. Mama, Mheshimiwa Rais nakwambia sisi Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na wadau wa habari, umetupa heshima kubwa. Ungeweza kumtuma mwakilishi katika mkutano wetu na ugumu wa ratiba yako ungeeleweka kwa kila mtu.

Nikushukuru pia kwa kuwajulisha kuwa nilipowasiliana na wewe tukakubaliana usiahirishe ujio wako katika shughuli hii kwa kuwa maandalizi yalikwishakamilika, maana wapo waliokwishaanza kusambaza umbea kuwa nimewadanganya usingekuja. Ulipofika, aibu imewazingira kila kona. Asante sana Mhe. Rais kwa heshima kubwa uliyotupa wanahabari kwani ni mara ya kwanza mkutano huu