Na Zulfa Mfinanga, Jamhuri Media,
Arusha

Wakati dunia ikiingia katika teknolojia mpya ya akili bandia, Asasi za kiraia nchini zimeiomba Serikali kutunga sheria rafiki zitakazowezesha kuleta maendeleo kwa haraka kupitia teknolojia hiyo badala ya kutunga sheria zitakazominya kasi ya kuleta maendeleo hayo.

Wadau hao licha ya kukiri kuwa teknolojia hiyo mpya imekuja na changamoto zake lakini wamesema watahakikisha wanatoa elimu kwa jamii juu ya fursa na athari zake ili jamii iweze kuitumia katika mambo ya msingi ambayo yataleta tija kwa Taifa na kwa mwananchi mmoja mmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari, leo Oktoba 24, 2023, Mkurugenzi wa Shirika la Waandishi wa Habari (MAIPAC), Mussa Juma amesema wao kama wana AZAKI watashirikiana na serikali kuhakikisha teknolojia hiyo inatumika kuleta faida kwa jamii na siyo kwenda kinyume na sheria, kanuni pamoja na taratibu za nchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Qaandishi wa Habari (MAIPAC), Mussa Juma.

“Malengo yetu sisi kama wana AZAKI ni kuona jamii inafaidika na teknolojia hii mpya kwa maana ya kutoka hapa ilipo na kupiga hatua mbele kimaendeleo kwenye kilimo, ufugaji, elimu na katika nyanja zote zinazohusu maendeleo ya mwanadamu, lakini wito wetu ni kuiomba serikali kuweka mazingira wezeshi kwa jamii ikiwa ni pamoja na kutunga sera na sheria zinazotoa sapoti katika ukuaji wake bila kuathiri tamaduni zetu” amesema Mussa Juma.

Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA Dk Rose Reuben amezitaka Asasi za Kiraia kutenga fungu la fedha kwa ajili ya vyombo vya habari ikiwa ni pamoja kuvitumia kwa usahihi vyombo hivyo katika kutekeleza majukumu yao huku Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Nukta Africa, Nuzulack Dausen akisisitiza kuwa matumizi ya akili bandia kwa asasi hizo hayakwepeki hivyo kuwataka kuanza kujiimarisha katika teknolojia hiyo ili wasiachwe nyuma.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji na Mwazilishi wa mtandao wa kijamii wa habari wa Jamii Forum Maxence Melo amezitaka Asasi hizo kuhakiki taarifa kabla ya kuzipeleka kwa jamii ili kuepukana na taarifa potofu na zisizo sahihi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Forum Maxence Melo

By Jamhuri