Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Iringa

Jeshi la Polisi mkoani Iringa inamshikilia Mohamed Njali kwa tuhuma za kumbaka mjamzito Atka Kivenule na kumsababishia kifo.

Kamanda wa Polisi mkoani humo Allan Bukumbi, amethitisha kutokea kwa tukio hilo lilitokea Jumamosi usiku, mtaa wa Maweni,Kata ya Kitazini ambapo mtuhumiwa huyo amedaiwa kuvamia nyumbani kwa marehemu saa 5, usiku na kudaiwa kufanya kitendo hicho.

Kamanda Bukumbi amesema Jeshi la Polisi linamshikilia mtuhumiwa huyo kwa mahojiano zaidi ili kujua sababu za mauaji hayo.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Alfred Mwakalebela amethibitisha kupokea mwili wa mwanamke anayedaiwa kubakwa hadi kufa akiwa na ujauzito wa wiki 10.

“Inasemekana alikuwa amelala ndani akavamiwa na mtu na katika uchunguzi tumegundua alivunjwa koromeo na tulikuta michubuko hivyo inaonekana mbakaji alikuwa akimnyonga shingo ili atimize azma yake,’ amesema mganga huyo.

Akizungumzia tukio hilo kwa masikitiko, mume wa marehemu, Adeline Kileo, amesema siku ya tukio alikuwa pamoja na kaka yake na wakazi wengine wakiangalia pambano la ngumi la Mandonga.

Amesema wakiwa wanaendelea kuangalia pambano hilo mtuhumiwa alimfuata na kumwambia kuwa “mkeo ni mzuri sana,na ana shepu hatari.”

Amesema kuwa kutokana na maneno hayo hakupendezewa nayo lakini alimpotezea na kuendelea kuangalia pambano hilo.

Amesema kuwa, baada ya kumalizika kwa pambano hilo alirudi nyumbani lakini cha kushangaza alikuta mlango wa nyumba yake upo wazi na alipoingia ndani alishikwa na butwaa baada ya kumuona mkewe akiwa amelala kitandani akiwa kifudifudi na akiwa uchi.

Amesema kuwa alipojaribu kumwamsha haikuwezekana ndipo aliposhirikiana na majirani na kumkimbiza hospitali lakini daktari alisema alishafariki.