Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk. Alex Malalusa, amesisitiza umuhimu wa kulinda na kudumisha amani nchini, huku akihimiza mamlaka husika kuharakisha ufumbuzi wa migogoro iliyopo.

Askofu Dk. Malasusa ambaye pia ni Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania (KKKT), anaamini kuwa Watanzania hawahitaji vita katika kipindi hiki cha ushindani mkubwa wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii duniani.

Kiongozi huyo wa kiroho ambaye pia ni Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, anaamini pia kwamba bado kuna nafasi ya kushughulikia malumbano yanayojitokeza na kuimarisha mshikamano wa Watanzania.

Dk. Malasusa ameyasema hayo katika mahojiano maalum na JAMHURI Dar es Salaam hivi karibuni. Mahojiano hayo yamejikita katika suala zima la amani hapa Tanzania.

Mgogoro wa Malawi, Tanzania

Askofu Malasusa anasema tayari CCT imepenyesha mkono wa kiroho kusaka suluhu ya mgogoro wa kugombea mpaka katika Ziwa Nyasa kati ya Malawi na Tanzania.

Hatua hiyo ya CCT imekuja huku Tanzania na Malawi zikiwa tayari zilishatangaza kukutana kwa ajili ya mazungumzo ya amani kutafuta ufumbuzi thabiti wa mgogoro huo uliodumu kwa takriban karne moja sasa.

Mwenyekiti huyo wa CCT anasema jumuiya hiyo imeona haja ya kuwatuma maaskofu kadhaa kwenda kusaka suluhu ya mvutano huo nchini Malawi ili kuendeleza uhusiano uliopo.

“Tumeshiriki kutafuta suluhu ya mgogoro huo, tumetuma maaskofu wetu kwenda kukutana na Wamalawi,” anasema Askofu Dk. Malasusa.

Anasisitiza kuwa siku zote suluhu nzuri ya malumbano si mapigano ya kutumia silaha, bali ni mazungumzo ya amani baina ya pande zinavutana.

“Bado tunaamini kuwa Malawi watakuwa tayari kukaa na Tanzania katika meza ya mazungumzo ya amani,” anaongeza kiongozi huyo wa kiroho.

Azungumzia chokochoko za Rwanda

Kuhusu chokochoko zinazodaiwa kutolewa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, dhidi ya Tanzania, Askofu Malasusa anasema zinahitaji ufumbuzi wa haraka ili kuendeleza uhusiano uliopo baina ya nchi hizo.

Kwa mujibu wa mitandao mbalimbali ya kijamii na taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Tanzania, Rais Kagame anadaiwa kusikika akitoa matamshi ya vitisho kwamba atamtandika Rais Jakaya Kikwete.

Mbali ya Kagame, kumekuwapo na taarifa zisizo rasmi kwamba baadhi ya viongozi wa Serikali ya Rwanda wamekuwa wakimshambulia Rais Kikwete kwa kumpachika majina ya kejeli.

Hata hivyo, Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Dk. Ben Rugangazi, ameshakanusha tuhuma hizo na kuwaomba Watanzania na Wanyarwanda kuzipuuza kwa vile zina lengo la kuleta vurugu na uhasama baina ya pande hizo mbili.

Askafu Dk. Malasusa anasema; “Mawasiliano kati yetu [Tanzania] na Rwanda ni makubwa na ya muda mrefu. Tutafute chimbuko la kauli hiyo [inayodaiwa kutolewa na Rais Kagame].

“Watanzania hatuhitaji vita kwa sababu gharama ya kupigana ni kubwa sana, vita ina athari kubwa na za muda mrefu,” anasema Askofu hiyo.

Atabiri amani urais 2015

Alipoulizwa mtazamo wake kuhusu malumbano ya kisiasa hapa nchini katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2015, kiongozi huyo wa CCT na KKKT amesema anaamini uchaguzi huo utafanyika kwa amani.

“Ni matumaini yangu kuwa uzoefu tulioutumia kufanya chaguzi zilizopita kwa amani, tutautumia kufanikisha Uchaguzi Mkuu ujao kwa amani,” anasema na kuendelea:

“Nashukuru kuona ujio wa Katiba mpya kwani ni suluhisho linalotuandaa vizuri kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao. Watanzania wasiwe na hofu, Tume ya Katiba mpya ina viongozi wazuri.”

Dk. Malasusa anawahimiza Watanzania kuepuka malumbano na vitendo vinavyoweza kuvuruga uchaguzi huo na kuisababishia nchi hasara.

“Tumkatae shetani ambaye anaweza kutuletea shida. Uchaguzi Mkuu unagharimu fedha nyingi, hivyo, matokeo ya uchaguzi yakivurugwa tutapoteza fedha nyingi.

“Tumeshuhudia nchi mbalimbali zikipata machafuko na kusababisha mauaji ya watu wasio na hatia, wengi wakiwa wanawake na watoto. Tunaomba uchaguzi ujao uwe wa amani,” anasema.

Anasema kitendo cha Tanzania kuwa kimbilio la wakimbizi wengi kutoka mataifa mbalimbali, ni uthibitisho tosha kuwa nchi hii ni kisiwa cha amani inayohitaji kulindwa na kila mtu.

Kuhusu wanasiasa wanaoendekeza kauli za kupigana vijembe, kiongozi huyo wa kiroho anawakumbusha wanasiasa wa aina hiyo kutambua kuwa siasa ni mazungumzo ya kushindanisha hoja na sera, si malumbano na mapigano.

Akieleza msimamo wake kuhusu wanasiasa walioanza kutangaza nia zao za kuwania urais mwaka 2015, Askofu Dk. Malasusa amesema haoni tatizo kwa kuwa hilo ni suala la hiari ya mtu na ratiba ya chama chake cha siasa.

Hata hivyo, amewashauri Watanzania kutojikita zaidi katika siasa zinazolenga Uchaguzi Mkuu ujao, na kuweka kando mambo mengine ya kuwaletea maendeleo likiwamo la uzalishaji mali kupitia sekta mbalimbali.

Apuuza majeshi ya vyama

Askofu huyo wa KKKT ameeleza msimamo wake kuhusu uanzishwaji wa vikundi vya ulinzi katika vyama vya siasa, akisema hajui uhalisia wa taswira hiyo.

“Majeshi ya vyama [vya siasa] mimi binafsi kama Alex Malalusa sina uhalisia wake,” anasema na kuongeza:

“Mimi ninaamini kuwapo kwa vyombo vya ulinzi na usalama serikalini, wapo watu wenye dhamana na suala hili.

“Mimi ninaogopa sana kama vyama vya siasa vitakuwa na vikundi vya majeshi. Tungeacha suala hili kwa vyombo husika ambavyo kikatiba haviruhusiwi kujihusisha na siasa.”

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, maofisa wa majeshi ya ulinzi na usalama hawaruhusiwi kujihusisha na masuala ya siasa.

“Itakuwa ni marufuku kwa mwanajeshi yeyote kujiunga na chama chochote cha siasa, isipokuwa tu atakuwa na haki ya kupiga kura iliyotajwa katika ibara ya 5 ya Katiba hii,” inasema sehemu ya (3) ya ibara ya 147 ya Katiba hiyo.

Dk. Malasusa anaamini pia kwamba bado kuna nafasi ya dini na asasi mbalimbali kuandaa mpango mkakati wa kuvikutanisha vyama siasa na vyombo vya ulinzi na usalama serikalini kurekebisha mvutano uliopo.

Kwa upande mwingine, Askofu Malasusa ametumia nafasi hiyo kuwahimiza viongozi waliokabidhiwa madaraka ya nchi kuwatendea haki Watanzania kama njia mojawapo ya kudumisha amani hapa nchini.

“Tutaendelea kuiombea nchi [Tanzania] isiingie katika vita na kutuletea [Watanzania] shida,” anasisitiza kiongozi huyo wa kiroho.


Please follow and like us:
Pin Share