Mhalifu anapopewa wiki 2 za kuharibu!

Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Jayaka Kikwete, ametangaza operesheni ya kuwaondoa wahamiaji haramu na majambazi katika mikoa ya Kagera na mingine nchini.

Uamuzi wake umekuja baada ya kimya kirefu cha Serikali, juu ya kuumizwa kihali na kisaikolojia kwa Watanzania wenzetu walio pembezoni kijiografia, hasa Kagera na Kigoma.

Ni jambo la kusikitisha kwamba pamoja na kelele zote za vyombo vya habari na wananchi, imemchukua Rais muda mrefu kuwashughulikia wazandiki na mabazazi hao wa ndani na wenzao wanaotoka nchi jirani.

Lakini kingine kinachosikitisha ni cha Rais kuwapa wiki mbili wahalifu, ama kuondoka nchini, au kufuata sheria za uhamiaji! Pia akawapa majambazi kipindi kama hicho kusalimisha silaha. Salamu zake zikawa kwamba atakayepuuza kufuata maelekezo hayo, ambayo kimsingi ni maelekezo halali, atakiona cha mtema kuni.

Sina shaka na hatua ya Ndugu Rais. Shaka yangu ni ya kuwapa wahalifu muda wa kuondoka nchini na wa kusalimisha silaha.

 

Kwa kawaida mtu unapopewa muda wa kukoma kufanya jambo fulani, bila shaka ndani ya muda huo utahakikisha unafanya ulichokusudia kukifanya kwa namna ambayo utakuwa ukijisemea, “baada ya hapa ndiyo basi tena”.

 

Jambazi anapopewa muda, maana yake afanye ujambazi kwa kasi na kwa bidii inayostahili ili muda wa ukomo ukiwadia, awe ameshakidhi matakwa yake.

Wahamiaji haramu, na hasa majambazi si watu wa kuwapa muda. Hao walipaswa wakutane na mkono wa dola mara moja wakiwa hawajajiandaa. Kuwapa muda ni kuwafanya wabuni mbinu nyingine za kuendeleza mapambano wakiwa ndani ya eneo ya mapambano.

Watu wanaoingia nchini wakiwa na makundi ya ng’ombe; watu wanaowaua raia wetu, watu wanaofyeka mashamba ya wenye nchi, watu wanaoiona Tanzania kuwa ni kama mahame yasiyo na mwenyewe, watu walio tayari kuingiza silaha nchini mwetu na kuongeza uhalifu; hao si wa kupewa muda wa kujiandaa kuondoka. Hao walipaswa Rais akishuka jukwaani, nao wawe wameshapata pa kutokea.

Maandishi hayafutiki. Uamuzi wa Rais umenikumbusha nyuma kidogo. Novemba, 2006 niliandika makala yaliyokuwa na kichwa cha habari, “Kigoma, Kagera si Tanzania tena”.

 

Kamanda wa Polisi wa wakati huo katika Mkoa wa Kagera, Venance Tossi, na wadau wengi, walinishukuru kwa zawadi. Siitaji, lakini ilikuwa takrima kwa maana halisi ya takrima kama inavyoelezwa kwenye kamusi. Sina hakika, lakini inawezekana makala hayo yalisaidia kuiamsha Serikali, ikaamua kuliimarisha Jeshi la Polisi na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), hata makamanda na wapiganaji wetu wakaweza kuwafurusha majambazi na wahamiaji haramu.


Bahati mbaya ni kwamba Tanzania hatuna vitengo vya “ukarabati”. Kila siku tunataka kujenga tu, lakini si kukarabati. Barabara za lami hadi zibomoke kabisa ndipo tuanze ujenzi mpya. Vivyo hivyo, kasi iliyofanywa na majeshi yetu mwaka 2006/2007 katika mikoa ya Kagera na Kigoma, iliachwa na matokeo yake ndiyo haya ya “kujenga upya”.


Kama kweli kazi ile ingesimamiwa vizuri, juzi tungemsikia Rais Kikwete akitoa pongezi kwa majeshi yetu, badala ya kutangaza kuanza kwa operesheni nyingine. Tujifunze kushikilia kile tunachoona kina manufaa.

Kwa kutambua kuwa hali ya maisha katika mikoa ya pembezoni ni mbaya, na kwa kuthibitisha kuwa mambo tunayoyaandika huwa yana mantiki, nimeomba niirejee makala hiyo ya mwaka 2006 neno kwa neno. Kwa wale watunzaji wa kumbukumbu wanaweza kuyapata makala hayo kwenye Tanzania Daima (gazeti nililoshiriki kuliasisi) ya Novemba, 2006.

Hii ni sehemu ya niliyoandika:

NIMEJITAHIDI kutafuta maneno murua, ninayoweza kuyatumia kuufikisha ujumbe huu kwa Watanzania, lakini nikiri kuwa nimeshindwa.

 

Sijui nitumie maneno au vionjo gani, ambavyo vitawapa picha halisi wananchi wanaoishi nje ya mikoa ya Kagera, Kigoma, Tabora na hata Rukwa, ili waelewe ninachotaka kusema.

Nia yangu ni kutaka wananchi wenzangu wajue jinsi Watanzania wenzetu, katika mikoa ya magharibi, walivyopoteza uhuru, utu na amani ndani ya nchi yao.

Baada ya kufika katika Mkoa wa Kagera, hasa katika wilaya za Biharamulo, Ngara, na Karagwe, sikuamini kama niko Tanzania.

Nilipofika Kibondo, Kasulu, na nilipotoka Kigoma kwenda Tabora, kupitia eneo la kambi za wakimbizi za Lufufu I na Lufufu II, sikuamini asilani kama kweli hii ndiyo nchi yangu.

Sikuamini kama hii ni sehemu ya Tanzania, nchi inayosifika kwa amani, utulivu, umoja na mshikamano. Nasema sikuamini kabisa. Sikuamini kwa sababu hakuna siku nimeomba polisi wanisindikize kutoka Mbezi kwenda Kariakoo.

Huku magharibi, hata kwenda sokoni, karibu wenzetu hawa watahitaji polisi wa kuwasindikiza!

Maisha gani haya? Je, kweli Serikali iko makini? Inasikiliza kilio cha haki cha wabunge wa mikoa hii? Kwa nini tumelala kiasi hiki wakati Tanzania imechukuliwa na wageni majambazi?

Katika maisha yangu, sijawahi kuona polisi wakiwa na bunduki zilizofungwa magazine tatu, nne, hadi sita! Sikuwahi kuona kituko hiki. Kwa anayeona hali hii kwa siku ya kwanza, kama ilivyokuwa kwangu, anaweza kudhani anachoshuhudia ni maigizo.


Kutoka Buselesele hadi Nyakanazi, wapo waliotushangaa, kwamba tumewezaje kupita katika pori bila ulinzi wa polisi. Kutoka Nyakanazi, tulikwenda moja kwa moja hadi Rusumo wilayani Ngara.

Barabara ni nzuri. Ni barabara ya lami iliyojengwa. Inapita katika milima na mabonde ya kuvutia. Barabara yote hii ni hatari. Majambazi ni wengi. Wanafanya unyama wa kila aina. Wanateka magari asubuhi, mchana, jioni na usiku. Ujambazi ni kwa saa zote 24!

Mwezi uliopita, majambazi walimuua mpiga debe katika stendi ya mabasi Ngara, siku iliyofuata waliingia Karugawe. Siku tano baadaye wakarejea na kuua watu wawili, na wengine kama hao walifia hospitalini.

Kutoka Ngara, tukawa na safari ya kwenda Karagwe. Usafiri kati ya sehemu hizi mbili ni wa matatizo makubwa mno kwa wananchi.

Kutoka Benako, unaingia katika pori la Kimisi. Hili ni pori kubwa, refu, na pana. Kwa gari aina ya Land Cruiser tulilokuwa tukisafiria, tulitumia muda wa saa nne hivi kukatiza pori hili. Barabara ni nzuri, na kwa muda wote huo, na kwa aina ya gari tulilokuwa tukitumia, bila shaka msomaji anaweza kujiuliza kuhusu ‘uzito’ wa pori hilo.

Tulipita tukiwa tunasindikizwa na polisi wawili wenye silaha na “magazine” zisizo na idadi, maana wanasema majambazi wengine huwa na risasi hata zaidi ya 600; kwa maana hiyo, wingi wa risasi ni jambo linalozingatiwa mno na polisi.

Majambazi katika pori hili, wengi wanadaiwa kuwa ni wakimbizi kutoka Rwanda, lakini kuna habari kwamba wanashirikiana na Watanzania; ambao bila shaka yoyote, wana asili ya huko huko au ni wadau tu wa uhalifu.

Ndani ya pori hili, maeneo hatari zaidi ni yake yanayopatikana mtandao wa simu selula.  Katika eneo hilo, wananchi wanajua wazi nafasi ya simu katika suala zima la ujambazi. Majambazi huwasiliana kirahisi. Hawa ni wale wanaoingia kwenye magari ya abiria, na wengine wanaokuwa maporini.

Siku za Alhamisi na Ijumaa ndizo mbaya na hatari zaidi, kwani ni siku za minada. Majambazi huteka magari na kupora abiria mali zao. Mauaji au kujeruhiwa katika matukio ya aina hiyo, si mambo ya kuulizwa.

Polisi wanaeleza wazi kuwa wamechoshwa na kazi ya kusindikiza magari, yawe ya abiria, mizigo au ya viongozi. Wenzao wamepiga kambi katikati ya pori hili. Hawa wanaishi maisha kama ya ngochiro! Hawana huduma muhimu, japo za mawasiliano. Wengine hawana redio za mawasiliano, eti wakipewa wanaweza kuporwa na majambazi, kisha wanazitumia kuendeleza uhalifu!

Katika pori hili la Kimisi, suluhisho la kumaliza ujambazi ni kuendesha operesheni ya kijeshi katika wilaya za Karagwe, Ngara, Biharamulo, Kibondo, Kasulu na Kigoma kwa jumla.

Hili si jambo la kuepukwa. Tuna makamanda na wapiganaji wa JWTZ, wanafanya nini wakati huu ambao hatuna ugomvi na majirani zetu?

Nani anayedanganya kuwa kazi hii inaweza kufanywa na polisi hawa wawili, watatu waliopo hapa Ngara, Karagwe, au Biharamulo? Helikopta za jeshi zinafanya nini? Vifaru na mizinga, ni kwa ajili ya nani?  Tuna haki ya kutamba kwamba Tanzania ni nchi ya amani, ilhali kuna Watanzania wenzetu wanaogopa hata kwenda kuteka maji kwa kuhofia kutekwa na kutendewa vibaya?

Kuna sababu gani zinazokwamisha Serikali kuweka vituo vingi kwenye mapori ya wanyamapori? Leo hii ni aibu kubwa kwa nchi yetu kuona kuwa majambazi wameanzisha jamhuri yao ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mfano, hakuna anayeweza kupita katika barabara kuu ya lami kuanzia Burigi Game Reserve-Ngazi Saba-Karugete-Mgodini. Eneo hili ni jamhuri ya majambazi.  Matatizo mengine yako katika pori linaloanzia Muleba hadi Biharamulo. Kwa gari tulilokuwa nalo, ilituchukua muda wa saa tatu hivi kukatiza pori hili. Barabara ni nzuri sana.

Hii ni ngome imara sana kwa majambazi. Kuna majambazi kutoka nchi jirani, walioingia na kujichimbia, wakiendesha vitendo vya kinyama kwa Watanzania. Mwisho

Ndugu zangu, kulinda usalama wa nchi na wananchi wetu ni wajibu wetu sote. Ni jambo la kutoa aibu kuona kuwa Tanzania tunayosema ni nchi ya amani, wananchi wakiwa wanasafiri kwa muda maalumu – kisa, kuwakwepa majambazi.

Hatuhitaji bajeti kubwa kama ya Marekani kuweza kuulinda utu wetu. Ni wajibu wa kila mmoja, na kwa nafasi aliyonayo, kushiriki kuimarisha ulinzi. Miaka ya 1960, 1970 hata mwanzoni mwa miaka ya 1980 suala hili liliwezekana.

Liliwezekana kwa sababu tulikuwa wazalendo kwa Taifa letu. Tulikuwa na mfumo madhubuti uliomfanya kila Mtanzania kuwa mlinzi wa Taifa lake. Tulikuwa na mfumo kuanzia nyumba kumi kumi hadi ngazi ya Taifa. Majahili waliojipenyeza wakaingia nchini, hawakutoka salama bila kunaswa.

Mtwara walifanya hivyo. Kagera walifanya hivyo. Kigoma, Zanzibar, Tanga, Mbeya, Rukwa na kila mahali katika Taifa letu. Uzalendo ukifikia kiwango cha juu kabisa.

Watanzania sasa ndiyo tunaowakaribisha wahalifu hawa. Tunawalea. Tunashirikiana nao kwenye uhalifu, Mauaji na uhalifu mwingine vinaongezeka. Serikali inarushiwa lawama kana kwamba ina nguvu za ‘kimungu’ za kubaini wabaya wote.

Tuna sababu zote za kuhakikisha nchi inakuwa salama ili Watanzania wote tuweze kuendesha shughuli zetu za kiuchumi bila hofu ya majambazi au wahamiaji haramu. Hilo linawezekana. Halihitaji itikadi. Tuungane na tuanze sasa.

Please follow and like us:
Pin Share