Atafuna mamilioni ya kijiji

Wananchi wa Kijiji cha Sango, Kata ya Kimochi, Wilaya ya Moshi Vijijini, wamepoteza mapato yanayofikia Sh milioni 60 katika kipindi cha miaka mitatu kutokana na fedha hizo kuliwa na Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho.
Wananchi hao wamelieleza JAMHURI kuwa fedha hizo zinatokana na makato ya asilimia kumi kutoka kwa wananchi wa kijiji hicho, ambao waliuza mashamba yao na kutakiwa kulipa kiasi hicho fedha kwa Serikali ya Kijiji.
Lakini tofauti na malengo ya Serikali ya Kijiji, Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Haji Chambo, anatuhumiwa kutumia ofisi yake vibaya kwa kutembea na muhuri mfukoni ambako anadaiwa kuwagongea muhuri wanaouza mashamba na kiasi hicho cha asilimia kumi kuingia mfukoni mwake.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Sango, Christomoo Tenga, amesema kuwa Halmashauri ya Kijiji ilipitisha sheria ndogo za kuwataka wote wanaouza mashamba kulipa asilimia kumi kama moja ya vyanzo vya mapato ya kijiji.
Amesema kuwa pamoja na maazimio hayo, Mtendaji huyo amekuwa akitenda kinyume chake na hivyo kukikosesha mapato kijiji hicho kutokana na kuweka fedha mfukoni mwake.
“Halmashauri ya Kijiji baada ya kupata habari kwamba kuna watu wanauza mashamba na Mtendaji Chambo anapokea malipo yasiyorasimishwa kwa stakabadhi ya fedha, ilipendekeza kuwa wakati wa miamala ya mauzo ya mashamba baadhi ya wajumbe wanapaswa kuwapo,” amesema Tenga.

Amewataja wajumbe hao kuwa ni Mwenyekiti wa Kitongoji husika, Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Mipango, Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi la Kijiji na majirani wa pande zote nne za shamba linalouzwa kwa nia ya kudhibiti upotevu wa mapato ya kijiji.
Pia amesema Halmashauri ya Kijiji iliazimia wakati wa mauzo ya mashamba, Mtendaji wa Kijiji atunze nakala ikiwamo mikataba ya mauzo ya shamba itakayofungashwa na stakabadhi ya malipo pamoja na fedha za ushuru huo kupelekwa benki.
“Kinyume na makubaliano; Ofisa Mtendaji Chambo kwa makusudi amekataa kutunza hizo kumbukumbu na hivyo kusababisha Serikali ya Kijiji kupoteza ushuru wa mauzo ya mashamba,” amesema Tenga.
Hata hivyo, Mtendaji wa Kijiji hicho alipotakiwa na JAMHURI kujibu tuhuma hizo hakukiri wala kukanusha na kudai mwenye kulisemea hilo ni mwajiri wake ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini, Amede Amani, amekiri kuwapo kwa malalamiko ya wananchi wa kijiji hicho cha Sango, juu ya utendaji usioridhisha wa Mtendaji huyo.

Amelieleza JAMHURI kuwa tayari amemwagiza Ofisa Utumishi pamoja na Ofisa Malalamiko kushughulikia malalamiko ya wananchi hao na kuongeza kuwa malalamiko dhidi ya mtendaji huyo yamekuwa mengi.
“Kuna barua iko hapa ofisini kwa Mkurugenzi kutoka huko Sango wakimlalamikia Mtendaji wao wa kijiji, na hapa sasa namwagiza Ofisa Utumishi na Malalamiko waende huko wakayashughulikie na sio kupiga simu,” amesema.
Tuhuma nyingine dhidi ya Mtendaji huyo ni kutoitisha vikao vya kisheria vya Serikali ya Kijiji, zikiwamo Kamati za Kudumu, Ulinzi na Usalama, Kamati za fedha na mipango na vikao vya Halmashauri ya Kijiji.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa kijiji, hata ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya haina muhtasari wa mikutano mikuu ya Kijiji cha Sango, na kusisitiza kuwa tangu achaguliwe kushika wadhifa huo mwaka 2014, Mtendaji huyo hajawahi kuitisha Mkutano Mkuu wa Kijiji.

“Kama haitishi vikao, kama hakuna maazimio anafanya kazi gani? Hufika ofisini siku anayotaka mwenyewe na wakati mwingine haonekani kabisa hapa Sango,” anahoji Mwenyekiti huyo.
Wakati tuhuma hizo zikiendelea bila kupatiwa ufumbuzi, JAMHURI limebaini kuwa kwa sasa Mtendaji huyo hana sifa za kuwa mtumishi wa umma, baada ya kutajwa kwenye orodha ya watumishi wenye vyeti feki.
Uchunguzi umebaini pia jina la Mtendaji huyo lipo namba 3,100 likisomeka Haji Seleman na kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, majina yake matatu ni Haji Selemani Chambo.
Alipoulizwa kama jina hilo ni lake ambalo limetajwa na nini kutajwa katika orodha hiyo ya wanaotuhumiwa kughushi vyeti, alishindwa kujibu maswali ya mwandishi wa habari hizi.
Akithibitisha hilo, Mwenyekiti wa Kijiji hicho,Tenga, amesema baada ya jina la Mtendaji huyo kutangazwa kwenye vyombo vya habari likiwamo gazeti hili kwa sasa halijulikani alipo.
Mwenyekiti huyo amesema kuwa, kwa sasa nafasi ya Mtendaji huyo wa kijiji inakaimiwa na Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Lyakombila kilichopo Kata hiyo hiyo ya Kimochi, Anna Raphael.