Wakufu wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) umelipatia Gazeti la JAMHURI Ruzuku ya Mabadiliko (Transformation Grant) kwa ajili ya kufuatilia habari za uchunguzi.
Gazeti la JAMHURI, limepata fursa ya kupewa ruzuku sambamba na gazeti jingine la Mwanahalisi, na redio nne ambazo ni Kili FM ya Kilimanjaro, CG FM ya Tabora, Ebony FM ya Iringa na Standard FM ya Singida.
“Vyombo hivi sita kwa ujumla wake tunavipatia ruzuku ya jumla ya Sh bilioni 2, viweze kufanya kazi ya uchunguzi wa kina kwa habari za uchunguzi na zenye masilahi ya jamii,” amesema Mkurugenzi Mkuu wa TMF, Ernest Sungura wakati wa kuzidua miradi hiyo katika viwanja vya Bunge hivi karibuni.

Katika uzinduzi huo ambao Spika wa Bunge, Job Ndugai alikuwa mgeni rasmi, TMF imetoa ruzuku ya taasisi na ruzuku ya mwandishi mmoja mmoja kwa ajili ya kuandika habari vijijini.
Sungura amesema wakati wa uzinduzi wa miradi hii kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma kuwa katika mpango huu wa ruzuku, pia waandishi 10 wamepewa “Fellowship” na waandishi 30 wamepewa ruzuku ya kundika habari za vijijini.
Amesema nia ya kuandika habari za vijijini na habari za uchunguzi ni kuwawezesha wananchi wasio na sauti habari zao kusikika. Pia ulitolewa ushuhuda wa habari za vijijini zinavyosaidia kubadili maisha ya wananchi kwa kutoa mfano wa Radio Kwizera ya Ngara iliyotangaza habari za mama kujifungulia chini ya mti, ambapo tangu habari hiyo itangazwe huduma za afya zimebororeshwa kwa kiwango kikubwa.

Akizungumza kwa niaba ya Spika, Abdallah Bulembo Majura, aliishukuru TMF kwa kuvisaidia vyombo vya habari kuandika habari za vijijini na akasema mchango wa vyombo vya habari ni mkubwa katika maendeleo ya taifa.
Vyombo vya habari vilivyopata ruzuku vitafadhiliwa kwa miezi 15 na waandishi mmoja mmoja, wanafanya kazi za uchunguzi na kuzichapisha katika maeneo waliyoombea kwa nia ya kuendoa kero za wananchi, hasa maeneo ya vijijini.
Gazeti hili la JAMHURI, limelenga kuitumia ruzuku hii katika eneo la uziduaji, ambalo linahusisha madini, mafuta na gesi kwa faida ya taifa la Tanzania.

“Tutapitia sheria zilizopo, tutatuma watu Ghana, Botswana na Afrika Kusini kufahamu wenzetu wanafanyaje katika sekta hii na wanapata faida ipi, ili habari tutakazoziandika zisaidie nchi yetu kufanya uamuzi sahihi katika kubadili sera na sheria za sasa.
“Nachukua fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza TMF kwa kulipa ruzuku JAMHURI, nilaloamini na kuuhakikishai umma ni kuwa gazeti la JAMHURI litafanya kazi ya uchunguzi kwa nguvu kubwa sasa kuliko wakati wowote.
“Tunawashukuru tena TMF kwa kutuunga mkono katika juhudi hizi za kujenga taifa letu, na tunaihakikishia jamii kuwa itapata habari zenye ubora mkubwa kuanzia sasa na baadaye,” amesema Mhariri Mtendaji wa JAMHURI, Deodatus Balile.
Katika mchakato huo, zaidi ya vyombo 100 viliwasilisha maandiko kuomba ruzuku hiyo, ila vyombo sita vilivyotajwa hapo juu ndivyo vimefanikiwa kupewa ufadhili.

By Jamhuri