Mkakati mahsusi umeandaliwa na raia wa kigeni kwa ushirika na taasisi mbili zisizo za kiserikali (NGOs) za hapa nchini, ukilenga kuichafua Serikali kupitia mgogoro wa ardhi katika Pori Tengefu la Loliondo, Ngorongoro mkoani Arusha, JAMHURI limebaini.

Raia wa Uingereza na Ufaransa, wiki kadhaa zilizopita waliingia nchini wakiwa wageni wa mashirika ya Pastoral Women’s Council (PWC) na Pingos Forum. Shirika la PWC linaongozwa na raia wa Kenya, Maanda Ngoitiko, na Pingos Forum kiongozi wake ni Edward Porokwa.
Taarifa kutoka Uhamiaji mkoani Arusha zinathibitisha kuwa Ngoitiko amenyang’anywa hati ya kusafiria ya Tanzania, lakini juhudi zimekuwa zikifanywa na baadhi ya viongozi kadhaa wa ngazi za juu Mkoa wa Arusha kuhakikisha anarejeshewa.
“Huyu baada ya kubaini si Mtanzania tulimnyang’anya hati ya kusafiria, lakini kuna wakubwa hapa mkoani wanataka tumrejeshee, tumegoma,” kimesema chanzo chetu.
Raia hao wa kigeni wametambuliwa kuwa ni raia wa Ufaransa, Profesa Jeremie Gilbert, na mwenzake raia wa Uingereza, Luke Tchalenko. Gilbert anatajwa kuwa anatoka shirika la kimataifa la Minority Rights Groups (MRG).
Tchalenko ni mpiga picha za filamu na majarida maarufu Uingereza, Kanada na Marekani yakiwamo The Times, The Globe and Mail na World of Interiors.

Vyanzo vya habari vimesema wawili hao wameletwa na mashirika hayo na kufanikiwa kupiga picha za filamu na za majarida; na kazi waliyoifanya ilipangwa kuanza kusambazwa duniani kote muda wowote kuanzia wiki hii.
“Waliandaliwa wananchi wa vijiji kadhaa Loliondo, wakafundishwa kuzungumza kwa jazba kuonyesha namna wanavyoonewa na Serikali ambayo wanasema inawanyang’anya ardhi yao na kuwapa wawekezaji.
“Kazi hiyo waliifanya kwa usiri na uangalizi mkubwa chini ya NGOs hizo, kwa hiyo tusubiri jina la Tanzania kuchafuliwa kimataifa,” kimesema chanzo chetu.
Imebainika kuwa upigaji picha na kuwahoji wananchi vilifanywa katika maeneo ya vijiji vya Soitsambu, Mondorosi na Sukenya.

“Kwenye vijiji hivyo walifanikiwa kupata ushirikiano kutoka kwa viongozi wa maeneo hayo na kuweza kuchukua picha za akina mama na vijana na kuandika ‘case studies’ mbalimbali kuonyesha mgogoro na kampuni ya Thomson Safaris. Walikuwa na vifaa vya kisasa vya kuwawezesha kuchukua picha kirahisi,” kimesema chanzo chetu.
Imebaini kuwa raia hao wa kigeni walifika nchini kwa mbinu za kijasusi, wakidanganya uhamiaji kwamba walikuwa wageni waliokuja nchini kwa mapumziko.
Kaimu Msemaji wa Idara ya Uhamiaji nchini, Mrakibu Msaidizi Rosemary Mkandala, ameulizwa na JAMHURI kuhusu ujio wa raia hao wa kigeni na kukiri kuwa ni kweli walifika nchini.
Rosemary anasema wageni hao, kama wageni wengine wanaokuja nchini, hueleza shughuli zilizowaleta.
“Kumbukumbu zinaonyesha kuwa walikuja kwa ajili ya holiday, basi,” amesema.

JAMHURI limebaini kuwa Jeremie na Tchalenko waliingia nchini Mei 25, mwaka huu kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) wakiwa katika ndege moja yenye namba KQ434.
Walikwenda moja kwa moja hadi Arusha ambako walikaa kwa siku kadhaa kabla ya kwenda Loliondo wakipita katika malango ya Engaruka, Longido na Engaresero. Wakiwa Loliondo walilala katika nyumba ya wageni ya Domel kuanzia Mei 28. Waliondoka Mei 31, kwenda Arusha mara baada ya kutimiza lengo lililowapeleka.
Uchunguzi wa JAMHURI unaonyesha kuwa wawili hao waliondoka nchini siku moja kwa ndege tofauti kupitia uwanja wa KIA. Jeremie aliondoka Juni mosi, kwa ndege yenye Na. KL571 iliyokuwa ikienda Amsterdam, Uholanzi.
Tchalenko aliondoka tarehe hiyo hiyo kwa kutumia ndege yenye Na. PW727.

“Wakiwa Loliondo pamoja na kuchukua picha za sinema na picha za kawaida, pia walizungumza na wananchi na kuwahimiza wasikate tamaa kwenye mapambano ya kuibana Serikali. Lakini kilichosikitisha ni kuwa walifikia hata hatua ya kuwataka wananchi ikiwezekana watumie mbinu ya kuchoma kambi za wawekezaji,” kimesema chanzo chetu.

Kesi ya raia wa Kenya
Ujio wa raia hao wawili wa kigeni, pamoja na ‘kuhamaisha vurugu Loliondo’, ulilenga pia kushuhudia kusomwa kwa hukumu ya kesi iliyokuwa imefunguliwa katika Mahakama ya Afrika jijini Arusha. MRG ndio waliokuwa wafadhili wa gharama zote kwenye kesi hiyo.
Kesi hiyo ilihusu jamii ya Ogiek (The Republic of Kenya vs Ogiek of Mau Forest) na ilifunguliwa katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu. Hukumu ilisomwa Mei 26, mwaka huu na kuwapa ushindi wananchi hao.
Uchunguzi unaonyesha kuwa PWC na Pingos Forum walipanga kikao cha siri kilichofanyika Soweto Garden, Arusha mnamo Mei 26 na Mei 27, mwaka huu.
“Mkutano ulihudhuriwa na viongozi wa vijiji vya Soitsambu, Mondorosi na Sukenya na wawakilishi kutoka MRG. Hoja kubwa ikawa kwamba baada ya ya Wakenya kupata ushindi, sasa ni zamu ya wakazi wa Loliondo kufungua kesi endapo Serikali itaendelea na mpango wake wa kutenga eneo la kilometa 1,500 za mraba kwa uhifadhi na kilometa za mraba 2,500 kwa ajili ya wananchi,” kimesema chanzo chetu.
Mmoja wa wasiri wetu kwenye kikao hicho amesema mambo kadhaa yaliafikiwa, yakiwamo makuu matatu- kuibua mgogoro mpya kwa wafugaji wanaoshi ndani ya eneo la hifadhi la Ngorongoro, kuleta waandishi wa habari kutoka MRG na mashirika mengine ya kimataifa, na pia kuwashirikisha viongozi wa vijiji na kata kuhamasisha wananchi kupinga hatua zozote za Serikali za kumega eneo la uhifadhi Loliondo.
Baada ya kikao hicho kilichoratibiwa na Ngoitiko na Porokwa, ndipo ukaandaliwa utaratibu wa kuwapeleka Loliondo raia hao wawili wa kigeni. MRG tayari imeshathibitisha kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya ufunguzi wa kesi katika migogoro ya ardhi Sukenya na Loliondo kwa jumla.

Mkuu wa Wilaya (DC) ya Ngorongoro, Rashid Taka, amezungumza na JAMHURI na kusema hana taarifa za ujio wa Gilbert na Tchalenko.
“Nikiri kuwa sina taarifa za hao watu, itashangaza kuona kama walikuja bila taarifa na kufanya hayo unayosema walifanya. Tangu Waziri Mkuu alipokuja Loliondo tumeweka utaratibu mgumu wa kudhibiti wageni wasiojulikana. Tumeweka utaratibu kila mgeni anayekuja tutaarifiwe na hao wanaomleta, tena kwa barua. Mfano, juzi tu hapa walikuja wageni kukagua miradi wanayofadhili, NGO zikatuandikia barua,” amesema Taka.
Taka anasema baadhi ya NGOs zimefunga ofisi na kuondoka baada ya maelekezo ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyoyatoa mwishoni mwa mwaka jana.
“Kama wamekuja kimya kimya na kufanya mikutano vijijini bila kutoa taarifa kwetu, ni kosa. Halafu hao Pingos Forum siwajui na sijawahi kuonana nao. PWC wao nawafahamu,” amesema.
DC huyo amezungumzia utitiri wa NGOs na kusema: “Muda si mrefu- za kupungua zitapungua tu.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dk. Hassan Abbas, ameliambia JAMHURI kuwa ofisi yake haina taarifa za ujio wa mpigapicha huyo na mwenzake.
“Kwenye kumbukumbu zetu hakuna mahali popote panaponyesha kama waliomba kibali cha kufanya kazi za kuandika na kupiga picha hapa nchini, hilo ni kosa kisheria,” amesema.
Kwa kawaida, mwandishi wa habari yeyote anayekuja nchini kuandika, kupiga picha au vyote, anapaswa kupata kibali kutoka MAELEZO. Kama ni mpigapicha za filamu, anapaswa kupata kibali kutoka Idara ya Filamu.
“Kote huku hakuna. Hakuna majina yao Maelezo wala kwenye Idara ya Filamu,” amesema Dk. Abbas.

Mikakati iliyopangwa
Pamoja na mambo mengine MRG waliwakabidhi viongozi wa vijiji husika kamera na vinasa sauti na wakawapa mafunzo ya namna ya kuvitumia.
“Lengo lilikuwa kwamba vifaa hivyo vitusaidie tunapokuwa na mikutano ya wananchi tuweze kupata picha za matukio na kuwapelekea taarifa mara moja,” kimesema chanzo chetu.
Baadhi ya wananchi na viongozi wa vijiji wanaotajwa kuwa bega kwa bega na PWC na Pingos Forum kwa ufadhili wa MRG wakati wa kesi mahakamani Arusha ni Naarang’rang Lengume (mkazi wa Mondorosi), Magreth Alaipukoi (PWC), Mwenyekiti Kijiji cha Mondorosi, Joshua Makko; Mwenyekiti wa zamani wa Kijiji cha Soitsambu, Lotha Nyaru, Manyara Karia (PWC), Mathayo Mbaryo (mfanyakazi Sekondari ya Emanyata), Mwenyekiti wa Kijiji cha Sukenya, Loserian Minis; Mwenyekiti Kitongoji cha Sukenya Juu, Parkipuny Musa, na Marco Oloru ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Soitsambu.

“Sisi ni miongoni mwa mashahidi kwenye kesi ya Sukenya. Tulipelekwa Arusha ili kujengewa hamasa kuhusu kuibua upya migogoro ya ardhi katika Pori Tengefu la Loliondo na Sukenya. Hii ni kazi ya PWC,” amesema mmoja wa viongozi hao, na alipoulizwa kwanini anashiriki jambo ambalo ni la kuleta migogoro, akahoji; “Ukiwa wewe utakataa pesa?”
Makubaliano mengine yaliyoafikiwa kutoka kwenye kikao cha viongozi hao ni kuitisha vikao na mikutano ili kuwahamasisha wananchi kuendelea kupinga mipango yoyote ya kutenga eneo la kilometa 1,500 za mraba.

“Walisema wataendelea kuwaita viongozi wa vijiji mbalimbali kuwajengea uwezo na kuwatia nguvu kwa namna mbalimbali wanazojua wao za kiuchochezi ili kuhakikisha kuwa hawakati tamaa katika kuendeleza vurugu kwenye Pori Tengefu la Loliondo,” amesema.

Waziri Mkuu alipofika Loliondo
Desemba 15, mwaka jana Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifika wilayani Ngorongoro kuendelea na ziara aliyoahirisha siku kadhaa kabla ya maadhimisho ya Uhuru. Alitua moja kwa moja Loliondo na kufungua ukurasa mpya kwa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano katika kuutatua mgogoro wa robo karne katika Loliondo.
Hii ilikuwa siku ngumu kwa NGOs 30 zilizoandikishwa kufanya kazi katika eneo hili.
Waziri Mkuu, aliitisha mkutano wa pamoja katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Wasso na kuhudhuriwa na watumishi na watendaji wa vyombo vyote vya Serikali, wawekezaji, viongozi wa NGOs na wadau wengine.
Katika mkutano huo, Waziri Mkuu hakutaka kumung’unya maneno. Alieleza ushiriki wa NGOs kwenye mgogoro wa Loliondo.

“Wilaya yenu ni nyeti, ina shughuli nyingi za kitalii, sehemu kubwa ya ardhi inamezwa na utalii. Taifa linategemea utalii kupata fedha-mapato makubwa yanatokana na utalii. Hakuna aliye na kitu asitake kukiendeleza. Sheria za kutunza na kuhifadhi mazingira zipo. Maeneo hayatoshi ndiyo maana tunakuwa wakali kwa wageni wanaokuja kulisha mifugo na huku.
“Maeneo ya utalii lazima yasimamiwe na sheria za uhifadhi. Hapa kuna Pori Tengefu, maeneo haya yana sheria zinazoyalinda. Tufanye marekebisho kadhaa ikibidi, lakini wajibu wetu ni kulinda shughuli zinazotuletea tija ili tutoe huduma. Tusiingize chuki, tusiingize migogoro, watu hawaishi kwa migogoro.

“Migogoro hapa ipo ama wawekezaji, au utalii, au uwekezaji au sheria za uhifadhi. Kuna vijiji tulivyosajili, kama tulifanya makosa, tuliyafanya.
“Ndio maana nimetaka Kamati iliyoundwa chini ya RC (Mkuu wa Mkoa wa Arusha), ifanye kazi na baadaye nitawatuma mawaziri watatu-(Waziri wa Maliasili na Utalii, Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi) ili tufanye mabadiliko. Hatuhitaji tena migogoro,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Salaam kwa NGOs
Akiwa ameshika nyaraka mbalimbali zenye kuonesha anavyojua vema vyanzo vya migogoro Loliondo na wahusika wake wakuu, Waziri Mkuu akasema:
“NGOs zinachochea migogoro hapa, kuna nyingine hazijasajiliwa, wengine hawafanyi kazi zao…Nimeshituka wilaya moja (Ngorongoro) ina NGOs nyingi kweli. Kuna nini Loliondo? Kuna NGOs zaidi ya 30 lakini zilizo active ni 15. Zipo zinazotuhumiwa kuchochea vurugu. Hiyo msahau katika nchi hii-kujiingiza nje ya utaratibu, kama utamaduni huo upo, uishe. Tutawafutilia mbali. Kama tumeweza kusajili, tutakufuta pale usipofanya yale yaliyofanya usajiliwe.
“NGOs ni wadau muhimu kama wanafanya kazi vizuri. Tunathamini mchango mzuri, lakini nje ya hapo hatuwezi kuvumilia. Hizi NGOs idadi yake ni kubwa, hili ni swali la kujiuliza,” alisema.
Waziri Mkuu akasema fedha zinazokusanywa na NGOs hizo kutoka kwa wafadhili ni nyingi mno, lakini hakuna thamani ya hizo fedha.
“Tuna taarifa za benki, kazi mnazofanya hazilingani na fedha. ACCORD Tanzania mpo? PWC? UCRT? PINGOs, Oxfam, NGONET, Makao, Engudeo, KIDUPO, Frankfurt…
“Kuwa na NGOs siyo tatizo, tatizo ni function ya hiyo NGOs,” alisema.

Waziri Mkuu akasema anazo taarifa za NGOs ambazo baadhi zinaundwa na wanafamilia, na kusema hilo si kosa hata kama NGO husika inaundwa na watoto na wazazi, lakini tatizo ni pale zinapoacha kutekeleza yaliyo kwenye usajili wake na kuamua kujihusisha na uchochezi.
“Nikikugundua unafanya uchochezi nakufutilia mbali. Kauli hii isikukwaze kama huhusiki na mambo nje ya malengo ya kusajiliwa kwako. Kama ni siasa sajili chama cha siasa. Wote hapa mmesajiliwa kwa ajili ya kuleta maendeleo,” alisema.
Waziri Mkuu Majaliwa aliwanyanyua baadhi ya wamiliki wa NGOs hizo na kuwauliza bajeti zao. Wengi walitoa majibu ya kujikanganya, jambo lililozua vicheko ukumbini.
“Tunajua mnayofanya, wengine mna akaunti Kenya. Mna- operate Tanzania, lakini akaunti ziko Kenya. Serikali hii haitaruhusu…lazima mwende na filosofia mpya ya Serikali, hatutaki ubabaishaji,” alisema.
Waziri Mkuu alitaja baadhi ya fedha zinazokusanywa na NGOs hizo kila mwaka, lakini thamani ya fedha imekuwa haionekani.
Alitoa mfano wa PWC ambao kwa mwaka wanapata Sh bilioni 2.5 kutoka kwa wafadhili huku wakidanganya kuwa wamejenga shule, lakini ukweli ukiwa kwamba shule hiyo ni ya binafsi inayoendeshwa kibiashara.
“Serikali iko makini, hakuna ubabaishaji, tutafuta zote za ubabaishaji,” akasisitiza.

Akasema kuna NGOs nyingine zinafanya kazi kwenye briefcase, na akaagiza lazima ziandikishwe BRELA na zilipe kodi zinazostahili.
“Kama PWC anapewa Sh bilioni 2.5 kwa mwaka na shirika la UCRT linapokea Sh bilioni 1.5 kwa mwaka, lakini hajui yanafanya nini.
“Nina taarifa zenu mnapata hela nyingi, lakini mnahudumia vipi jamii- hakuna, sasa ngojeni ukaguzi ufanyike halafu nitachukua maamuzi [uamuzi] maana kila siku Loliondo, kuna nini hapa? Mnasajiliwa halafu hakuna cha maana.
“Najua mnachokifanya, sasa nawaambia Serikali haitawafumbia macho kuona hiki mnachokifanya hapa na ikigundulika mnafanya kinyume cha matakwa ya usajili tutazifuta,” alisisitiza.
Kutokana na kutoeleweka vema kwa matumizi ya fedha katika NGOs hizo, Waziri Mkuu akamwagiza Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afike Ngorongoro haraka iwezekanavyo kufanya ukaguzi katika asasi hizo.
“Kwanini nisilete Mkaguzi Mkuu wa Serikali kama kweli tuko serious kuleta maendeleo, na Baraza la Madiwani likapata nafuu, wananchi wakajisikia kupata msaada. Kama haturidhiki, kwanini tusiondoe? Hapa hakuna mchezo. Siyo Serikali hii…” alisema.
Kusikia hivyo, Mkurugenzi wa PWC, Maanda Ngoitiko, alisimama na kutaka kuzungumza, lakini Waziri Mkuu akamjibu: “Sikuja kufanya kesi, natoa maelekezo ya Serikali.
“Taasisi zinazolalamikiwa sana, kwa NGOs zote, nawapa muda wa matazamio kuanzia Januari hadi Juni 2017.

“CAG anakuja kukagua fedha na matumizi na miradi kama zina tija. Atanieleza zipi ziendelee, zipi zisiendelee, nasikia nyingine wajumbe wa Bodi ni wanafamilia, sina tatizo, mimi nataka matokeo ya hizo NGOs. Serikali itafanya kazi na wadau. Tulisajili, kama mlikuwa holela, sasa mambo yawe kwenye mpangilio. Nawapa miezi sita ya matazamio-kujua fedha mnazoingiza na kazi mnazofanya kwenye jamii. Lazima mbadilike, na wale wote mnaofanya mambo nje ya utaratibu mnapaswa kuacha mara moja, mkipuuza tutashughulika na ninyi. Fuateni kanuni na sheria. Nidhamu tumeanza ndani ya Serikali na tunataka ifike hadi nje mliko. Hili zoezi ni endelevu, lazima mjue msimamo wetu (Serikali ya Awamu ya Tano), atakuja CAG, tutakwenda saiti kukagua kazi zenu zote. Wenye akaunti nje ya nchi rudisheni nchini. Mnafungua NMB kwa gelesha, rudisheni, fanyeni kazi mlizosajili. Serikali hii haina mzaha, wote wa mambo ya ovyo tutawafutilia mbali.
“Watumishi wa Serikali wanaoshirikiana na NGOs tutawashughulikia. Kuna picha zinapigwa za kandambili chafu na kuwekwa kwenye mitandao wanasema ndio hali ya Loliondo. Ndio kazi mnazofanya? Nitafuta. Mnaandika kwenye mitandao… tutawafuta. Migogoro ya ndani lazima iishie ndani badala ya kuipeleka nje.

“Wapo wanaoshirikiana na raia wa kigeni kuichafua nchi yetu, taarifa zenu zote tunazo, e-mail zenu zote tunazo. Mswedeni alipigwa PI halafu mnamleta nchini kinyemela. Taarifa zote tunazo, na ikibidi tutamfuata huko huko aliko. Ninyi Watanzania ndio mnaoshiriki kuichafua nchi. Nidhamu zenu tutazifuatilia ndani na nje ya nchi, ukifanya mambo kwa kunyoosha tutakusifia. Ukichanganya mambo ovyo tupo pamoja na wewe. Kazi yetu sote ni kuwatumikia Watanzania na kuilinda nchi yetu.
“Halafu hizi NGOs kwanini wengine msiende Mbeya? Msiende Uvinza? Msiende Ruangwa? Sasa mmejaa hapa tu, tutajua yale yanayoendelea ili kujenga ‘discipline’ ndani na nje ya Serikali,” alisema Waziri Mkuu.
Baadaye kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Wasso, Waziri Mkuu alirejea msimamo wa Serikali wa kuzifuata NGOs kukomesha vurugu na migogoro Loliondo.

Alisema inastajabishwa kuona NGOs ikipokea Sh bilioni 1.4 na kutumia Sh milioni 120 pekee kununua mbuzi 400 huku fedha nyingine zikiishia kwa viongozi wa asasi hizo.
“Serikali makini ya Dk. Magufuli, haina ubabaishaji. Hakuna ruhusa kwa NGO kufanya chochote eti tu wewe ni NGO, hakuna. Atakayehamasisha wananchi kuvuruga miradi ya maendeleo tutamkamata,” alionya.
Hata hivyo, wakati miezi sita aliyoitoa Waziri Mkuu Majaliwa inaisha leo, bado hakuna taarifa zozote iwapo CAG alizikagua NGO hizo na kubaini iwapo walikuwa na matumizi sahihi ya rasilimali au la.

By Jamhuri