Kulikuwa na utatanishi juu ya kuleta mwili wake hapa nyumbani kutokea Uingereza mara baada ya kufariki Oktoba 14, mwaka 1999.

Uingereza walitoa ndege ya ROYAL AIRFORCE, ili ilete mwili wa Mwalimu Nyerere. Ni usafiri wa bure kama ilivyo kwa Serikali ya Afrika Kusini. Nao walitoa ofa ya kuleta mwili wa Baba wa Taifa.

Hatukujua njia ambayo Afrika Kusini ilipanga kutumia ama kuweka kama Cargo au kuuleta ndege maalumu.

Baada ya vuta nikuvute ya Serikali ya Afrika Kusini na Uingereza, baadhi ya wafanyakazi wa ATC tukazungumza na Jenerali Ulimwengu, wakati huo akiwa Mjumbe wa Bodi ya ATC na Mwenyekiti wa Bodi ya Wahariri wa Magazeti ya MTANZANIA, RAI, THE AFRICAN, DIMBA ili atufikishie ujumbe wetu kwa Rais Benjamin Mkapa.

Tulimwambia Ulimwengu maneno haya: “Tunaona fedhea mwili wa Mwalimu kuletwa na wataalamu wa kigeni, wakati vijana wake tupo na ndege yenye uwezo wa kwenda London na kurudi bila ya matatizo yeyote.”

Tukamwambia tena Ulimwengu: “Tunaiomba Serikali, kuwa mwili wa Mwalimu tukauchukue wenyewe na ndege yetu aina ya Boeing 737-300 iliyokuwa na rangi za bendera ya Taifa letu (Blue, Green, Yellow, black) ili tuidhinishie duniani kuwa Watanzania tumeendelea na tunamheshimu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.”

Ombi lilikubaliwa. Kundi lote lililokwenda Uingereza ilikuwa na marubani, wahandisi na wahudumu wa ndani wa Tanzania wakiongozwa na Kapteni Anderson Wililo na Kapteni Lessane (marehemu) walirusha ndege kutoka Dar es Salaam hadi London kupitia Cairo, Misri.

Kadhalika kutoka London, Uingereza kupitia Cairo hadi Dar es Salaam marubani hao walihakikisha ndege inaingia Dar es Salaam kwa wakati uliopangwa saa 3.15 asubuhi (09:15am) na kupokewa na umati mkubwa wa Watanzania ukiongozwa  na Rais Mkapa wakati huo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam.

Baada ya kukamilika shughuli zote za msiba hapa Dar es Salaam, mwili wa Mwalimu Nyerere ulipelekwa Mara kwa ndege ya Serikali aina ya F50 chini ya Kapteni Massawe kwa ajili ya mazishi.

Tulifanya hivyo, bila ya mwili wa Mwalimu kuguswa na Mzungu yeyote na hasa Makaburu waliokuwa wamekaa tayari kusaidia kama tungekwama ili wafanye kazi hiyo, kisha watutukane.

Hiyo ndiyo kazi ya vijana wa Tanzania walivyoifanya kwa kujitoa. Ni kama kwenye vita vya Uganda vilivyomalizika Aprili, mwaka 1979 ambako Mwalimu alishirikiana vema na vijana wake.

Mara baada ya vita vile, Mwalimu Nyerere alimteua Profesa Yusuf Lule kuwa Rais wa Uganda akitokea Edinburg, Scotland alikokuwa anafundisha.

Profesa Lule alifikia Dar es Salaam kutoka Scotland na kwenda Uganda kuwa Rais baada ya Dikteta Idd Amin kung’olewa madarakani kwa nguvu baada ya mapambano ya kivita yaliyodumu kwa miezi sita- kuanzia Oktoba, 1978 – Aprili, 1979.

Profesa Lule alipelekwa Uganda kwa ndege ya ATC kwa usiri mkubwa chini ya Kamandi ya Kapteni Anderson Wililo aliyetumia ndege aina ya Twinotter DHC -6 (De Havelland of Canada) na kutua salama katika Uwanja wa Ndege wa Entebbe chini ya ulinzi mkali wa ndege za kivita za Tanzania zilizokuwa zikiongozwa na Jenerali Robert Mboma, wakati huo akiwa Mkuu wa Jeshi la Anga.

Profesa Lule alipelekwa Kampala chini ya ulinzi mkali wa majeshi ya Tanzania na kutangazwa kuwa Rais wa Uganda na akaunda Baraza lake la Mawaziri.

ATC ilifanya shughuli za kitaifa kwa maslahi ya taifa kwa vile lilikuwa ni shirika la umma. Kwa hiyo, Serikali ilikuwa inaitumia ATC kwa matumizi yeyote ya kitaifa kutokana na maelekezo ya Ikulu.

Pia ilifanya kazi nyingi za huduma kutokana na maelekezo ya viongozi wa Serikali baadaye tena baadhi ya viongozi wakaanza kuihujumu ATC  kwa kuyapendelea mashirika mengine ya ndege ya mataifa mengine kwa sababu wanazozijua wao na mashirika hayo ili yatekelezewe matakwa binafsi na si kwa maslahi ya ATC na  taifa.

Rais Dk. John Magufuli uamuzi wako wa kununua ndege za ATC umeonesha uzalendo wa hali ya juu kwa taifa katika historia ya anga tangu Mwalimu Nyerere alivyokuwa Rais wa Tanzania.

Baada ya Mwalimu kuondoka madarakani, hakuna rais aliyeonesha nia hiyo. Wote waliofuata wakawa wanabariki kifo cha ATC bila ya kuwa na uchungu wa heshima ya taifa.

Hakuna ubishi kwamba baadhi ya viongozi wa Serikali walichangia kwa kiasi kikubwa shirika hili kuanguka. Kwa kawaida, wenzetu wenye uzalendo huwa hawapandi ndege za mashirika mengine kama shirika la taifa lipo na linashika njia hiyo hiyo.

Baadhi ya viongozi wa Afrika Kusini au Kenya tu, kwa mfano, kama wanakwenda nje ya nchi na ndege ya nchi yake inashika anga la huko, basi atapanda ndege ya shirika la kizalendo.

Rais Dk. Magufuli tangu umetoa tamko rasmi la kuifufua tena AIRTANZANIA kwa kununua ndege sita japo siyo kwa mara moja, hakika umeamsha ari mpya kwa wataalamu hususani marubani na waandishi ambao wameumia kwa muda mrefu kutokana na kukosa ajira wakiwa na ujuzi ambao taifa halikuuthamini.

Ajabu ni kwamba wengi wa wataalamu hao wakaamua kufanya shughuli nyingine kinyume cha utalaamu kwa sababu hawawezi kuzikuta Boeing mitaani na nchi haina makampuni binafsi ya usafiri wa anga yenye ndege hizo.

Ndiyo, marais kuanzia awamu ya pili; ya tatu; na ya nne hawakuona umhimu  wa kuwa na ATC imara.

Hakika wataalamu wa ndege tunakuunga mkono asilimia 100 na tunakuombea kwa Mwenyezi Mungu azidi kukufunulia kuondoa kero za muda mrefu za wanyonge ambazo zimechangiwa na wanasiasa wanaozingatia zaidi maslahi binafsi.

 

USHAURI BINAFSI:

Rais Dk. Magufuli naamini kuwa mambo mengi ya watendaji wa Serikali unayajua kwa undani kwa vile umekuwa mfanyakazi wa kwa zaidi ya miaka 25. Umekuwa katika nyadhifa mbalimbali za uongozi wa kazi za umma.

Wapo viongozi ambao ni wanafiki na wengine ni wa kweli. Kwa kwa maana wanaofanya kazi kwa manufaa ya taifa na wale wanafiki wanaojishughulisha kujipendekeza kwa Rais au Waziri Mkuu.

Kiongozi bora ni yule asiyejipendekeza bali anafanya kazi kwa maslahi ya taifa. Mara nyingi viongozi wanaojipendekeza ni watu hatari.

Mtangulizi wako, Rais wa awamu ya nne, Dk. Jakaya Kikwete alipata kuwaamini baadhi ya viongozi na sasa wanajifanya kwako kuwa ni wachapakazi hodari na waadilifu kwa umma.

Tafadhali, Rais Magufuli usiwaamini hata sekunde moja kwani Rais Kikwete hakuwahi kuwapa darasa la uadilifu na utii kwa umma.

Viongozi hao walichukua nafasi ya upole wake na wakajifanyia mambo kiholela bila kujua kuwa wanaoumia juu ya ubadhirifu wa mali za umma ni wananchi wa kawaida.

Ni wananchi wanaohitaji huduma za msingi kama matibabu, chakula, elimu na amani ya maisha yao. Nakuomba Rais Dk. Magufuli uongezee mbinu zaidi za kupambana na viongozi wasiokuwa waadilifu katika utendaji wa ngazi zote za serikali kwani elewa kuwa Rais Kikwete alipokuwa madarakani viongozi hao hao ndiyo waliokuwa wakimtukuza na leo ndio haohao wanamdharau.

Chini ya Kikwete, viongozi hao walikuwa na wajibu wa kuwa waadilifu bila kujali upole wake pia sidhani kama alikuwa anakataa ushauri wao wa maana kwa maendeleo ya taifa.

Natoa mfano mmojawapo wa maneno ya Mwalimu Nyerere aliposema ‘mtu anapokuja kuwambia jambo la kipumbavu na akijua kuwa jambo analokuambia ni la kipumbavu na ukaitikia kwa kushangilia atakuona JUHA.’

Ndiyo maana Mwalimu katika maisha yake, hakuwapenda tabia za Wazungu za kutaka Waafrika wawe majuha kwao. Wazungu wana tabia ya kusifu kwa kejeli kama walivyowafanyia akina Kamuzu Banda wa Malawi, Jomo Kenyatta wa Kenya na Mobutu Seseseko wa Zaire (sasa DRC), na Mfalme Hassa wa Morocco nakadhalika.

Rais Dk. Magufuli ili ufanikishe azma yako ya kuwatumikia wananchi kwa njia ya usawa, huna budi kuwa na viongozi wengi wasiopenda unafiki na kwa sababu viongozi wengi wameonja asali katika awamu zilizopita na wamekuwa matajiri kwa viwango mbalimbali kutegemea na eneo lake la kazi.

Rais Dk. Magufuli mambo yote unayofanya ni sahihi kabisa hata mbele ya Mwenyezi Mungu aliyeumba mbingu na nchi ila binadamu wengine wana hila za shetani kwa maana kuwa hawampendi binadamu anayetenda mema ya kumpendezesha Mwenyezi Mungu.

Ndiyo maana hata mitume na manabii walipata misukomisuko. Biblia ni ushahidi wa Yesu alivyokutana na misukosuko kadhalika Mtume Muhammad S.A.W yeye pia alipata misukosuko kule Makka na akakimbilia Madina (Saud Arabia).

Hivyo, Rais Dk. Magufuli endelea bila woga na sisi wananchi wenye mapenzi mema na nchi yetu tuko pamoja nawe kwa hali na mali – hatutakuangusha.

Tutakusaidia kuwafichua wabadhirifu wa mali za umma na wapinga maendeleo walioko ndani na nje ya nchi yetu Mwenyezi Mungu ibariki Tanzania na watu wake.

 

Mwandishi wa makala hii ni Mwanajeshi mstaafu wa Jeshi la Anga la Wananchi wa Tanzania na Mhandisi Mstaafu wa Shirika la ndege Tanzania (ATC). Anapatikana kwa namba 0785 042 078.

By Jamhuri