Mwishoni mwa wiki iliyopita serikali ilipokea ndege mpya kubwa aina ya Boeing Dreamliner 787-800 ambayo imenunuliwa na serikali na kukodishwa kwa ATCL, ikiwa ni ndege ya nane kununuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano tangu iingie madarakani.

Ujio wa ndege hizi na kukodishwa kwa ATCL unaonyesha dhamira ya serikali kuliwezesha shirika hilo kufanya biashara na kupata faida.

Huo ndio msingi wa kuzingatiwa, kwamba hatua zote zilizochukuliwa na serikali katika eneo hili la ununuzi wa ndege ziweze kuonyesha matunda yaliyokusudiwa.

Waziri wa Uchukuzi, Isack Kamwelwe, amemwambia Rais John Magufuli katika hafla hiyo kuwa tangu serikali ilipoanza kuikodisha ATCL ndege hizo mpya, hadi sasa kampuni hiyo imekwisha kukusanya jumla ya dola za Marekani milioni 14.

Lakini wakati ATCL ikijinasibu kufanya hivyo, inapaswa kufahamu kuwa ujenzi wa biashara imara, hasa inayotegemea wateja kama chanzo cha mapato, unahitaji uangalifu mkubwa. Uangalifu unakuwa mkubwa zaidi katika mazingira ya biashara ya ushindani kama ambavyo inaonekana katika sekta ya anga.

Kama usimamizi wa karibu wa biashara hiyo hautakuwepo kutokana na kutokuwa na mipango mizuri ya biashara, hata serikali ikileta ndege nyingi kiasi gani, bado ATCL itashindwa kutengeneza faida.

Rais Magufuli amedokeza katika hotuba yake kuwa kumekuwa na malalamiko mengi miongoni mwa wateja kuhusiana na safari kufutwa au kucheleweshwa na wakati mwingine kuambiwa kuwa ndege zimejaa wakati bado siti nyingi zipo wazi. 

ATCL inaweza kujiona kama ina nafasi kubwa ya kufanya biashara ya usafiri wa anga nchini hivi sasa kwa sababu ushindani wa ndani si mkubwa sana lakini ifahamu kuwa iwapo itaendelea kumomonyoa imani ya wateja wake kwa kutoa visingizio badala ya sababu za msingi za kuahirisha au kuchelewesha safari, itafika muda abiria hao hawatakuwa na imani tena na shirika hilo.

ATCL inapaswa kufahamu kuwa mali bila daftari hupotea bila habari na kuwa na ndege nyingi mpya si waranti ya kupata faida. Kinachotakiwa ni kuifanya biashara hiyo kwa kufuata mipango waliyojiwekea, wakiheshimu misingi ya biashara na kuhakikisha kila mara mteja wao anaridhishwa na huduma anazopatiwa.

Kutoa taarifa au kufanya uamuzi kwa lengo la kumfurahisha mtu fulani au kuifurahisha serikali ambayo ndiyo yenye ndege hizo, kamwe hakutaisaidia ATCL kufanya biashara ya faida.

142 Total Views 2 Views Today
||||| 1 Unlike! |||||
Sambaza!