*Augeuza mwambao wa Ziwa Tanganyika kuwa himaya yake

*Paroko wa Kanisa Katoliki, viongozi wa Serikali wakimbia kuhofia maisha

*Inspekta wa Polisi ajeruhiwa, apelekwa Hospitali ya Benjamin Mkapa Katavi

Na Mwandishi Wetu

Katika hali isiyotarajiwa, mganga wa jadi anayeaminika kuwa na nguvu za kuagua amesababisha mtafaruku mkubwa mwambao wa Ziwa Tanganyika.

Kwa miezi kadhaa sasa mganga huyu maarufu kwa jina la ‘Kamchape’ (maeneo mengine humwita Lambalamba), amekuwa akirandaranda vijijini huku mamlaka za serikali zikimwacha akiendelea kusababisha maafa na uharibifu wa mali za Watanzania wasio na hatia.

Baada ya kudumu katika Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma ‘akifanya kazi’ ya kusaka wachawi, Kamchape, sasa amehamia Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi na tayari amesababisha madhara makubwa katika kata za Ikola na Karema.

Wananchi wachangishana kumwalika

Taarifa zilizolifikia JAMHURI wiki iliyopita zinadai kuwa wakazi wa kata za Ikola, Karema na Kapalamsenga, wengi wao wakiwa ni vijana, ndio walioamua kumwalika Kamchape.

“Tumechoka na maisha haya. Watu hatulali kwa sababu ya wachawi. Kazi tunafanya, pesa hatupati ndiyo maana ni lazima sasa Kamchape aje kuwasaka wote wanaosababisha ugumu wa maisha kwa wengi wetu,” anasema kijana mmoja (jina tunalihifadhi) katika mkutano uliofanyika Julai 15, mwaka huu Ikola.

Mkutano huo ndio chimbuko la ujio wa Kamchape mkoani Katavi. Siku chache baadaye, vijana zaidi ya 100 wakafanya mkutano mwingine Karema; mikutano yote ikiwanyoshea kidole cha lawama watu wenye uwezo wa kifedha kuwa ndio wanaosababisha ugumu wa maisha Tarafa ya Karema.

Inadaiwa kuwa katika siku ya kwanza ya kampeni, zaidi ya Sh 400,000 zilikusanywa na chanzo chetu cha habari kinasema:

“Ni vigumu kufahamu jumla ya fedha zilizopatikana ndani ya wiki mbili za kampeni. Lakini ni fedha za kutosha zilizomshawishi Kamchape kuhamishia kazi Karema.”

Kwa nini Kamchape?

Akizungumza na JAMHURI akiwa mjini Mpanda mkoani Katavi, Paroko wa Karema, Padri Nicodemus Kyumana, anasema dhana ya kutafuta wachawi/uchawi katika jamii inatokana na umaskini na fikra duni.

“Jamii imeugua. Inahitaji ukombozi wa kiakili. Lakini kikubwa watu wafanye kazi. Wasitafute njia za mkato au watu wa kuwatupia lawama,” anasema Padri Kyumana ambaye ni mmoja wa Watanzania waliolazimika kuondoka Karema kwa usalama wao.

Mahubiri mfululizo aliyokuwa akiyatoa kukemea mwaliko wa Kamchape ndicho chanzo cha wanaounga mkono kuelekeza lawama kwake na hata tishio kwa uhai wake na mali za Kanisa Katoliki.

Hivi karibuni kwenye maziko ya mama mzazi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya (DED) ya Makete yaliyofanyika Ikola, Padri Kyumana alizungumzia suala la Kamchape akisema:

“Ni uchonganishi utakaosababisha uhasama miongoni mwetu.”

Jumapili ya Agosti 20, mwaka huu, Padri Kyumana alionya tena suala hilo, na siku hiyo akahudhuria kikao cha kamati ya kumwalika Kamchape kilichofanyika Karema.

“Nilikwenda. Nikawaomba na mimi nihudhurie, wakanipokea. Nikaanza kuwahoji sababu za kumleta Kamchape. Wakaniambia ni kutokana na matatizo mengi yanayowakabili.

“Nikawahoji ni hatua gani wamechukua kutatua matatizo ya msingi kama kuwapatia watoto chakula shuleni na mengine kadhaa? Hawakuwa na majibu.

“Kijana mmoja akasema, ‘hata Biblia imeandika kuwa Mungu aliumba vitu vinavyoonekana na visivyoonekana, kwa hiyo Kamchape anakuja kusaidia kuviona hivyo visivyoonekana’,” anasema.

Pamoja na hoja hiyo ambayo ilijibiwa vema na Padri Kyumana, mkazi mwingine alidai kuwa babu yake alijiua kutokana na ugumu wa maisha, na sasa anamtaka Kamchape aje amsaidie.

“Nikajaribu kuwapa somo la kwa nini kisaikolojia mtu anafikia hatua ya kujiua, lakini hawakutaka kunielewa, hivyo tukaachana bila kukubaliana,” anasema Padri Kyumana.

Kamchape atinga Karema

Hatimaye Agosti 28, mwaka huu, Hassan Athuman Mahuba (Kamchape) akaingia Ikola na kupata mapokezi makubwa, huku huo ukiwa mwanzo wa uharibifu mkubwa wa mali za raia kuwahi kutokea katika maeneo hayo.

Wa kwanza kuathirika alikuwa ni Diwani wa Ikola, Philemon Molo, ambaye nyumba zake za biashara ikiwamo nyumba ya wageni, ziliteketezwa kwa moto na mali nyingi kuibwa.

Molo ambaye amelazimika kukimbilia mjini Mpanda ameliambia JAMHURI kuwa kinachoendelea kwa sasa ni utapeli wa kusikitisha na kushangaza.

“Na bahati mbaya hatupati msaada wa vyombo vya dola. Ni kama hatupo Tanzania. Wanakuja matapeli wanawadanganya wananchi na wananchi wanakubali,” anasema Molo.

Anasema Kamchape ameungana na waganga wa jadi watatu waliopo Ikola kuwaaminisha watu kwamba wanaweza kuonyesha uchawi uliofichwa, mazindiko na mambo kama hayo.

Anasema walioharibu mali yake ni wananchi wala Kamchape hakuwapo na walifanya hivyo saa tano asubuhi.

“Nikatoa taarifa polisi, wakaja askari watano na silaha. Wakadhani wangefaulu kuwadhibiti, lakini ikashindikana,” anasema.

Molo si mtu pekee anayeishi ‘uhamishoni’ kwa sasa kwa kuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Karema, Cyril Mkondola, naye ni mwathirika mwingine, na analiambia JAMHURI:

“Makumi ya vijana walivamia nyumbani kwangu usiku; huku wakirusha mawe juu ya paa, wakanilazmisha kusaini nyaraka kuruhusu Kamchape afanye kazi.

“Wakanilazimisha kugonga na mhuri. Nikaona maisha yangu yamo hatarini. Nikampigia Mtendaji wa Kata, akaniambia nifanye kama wanavyotaka.”

Hata hivyo, pamoja na kusaini karatasi hizo, bado vijana hao waliharibu nyumba yake na kuichoma moto, wakidai kuwa ni yeye ndiye aliyesababisha wenzao kukamatwa na polisi.

Baadaye alifanikiwa kutoroka Karema hadi Kapalamsenga alikopanda basi na kwenda Mpanda mjini.

Mali zaidi zateketezwa

Wengine ambao wameathiriwa na ujio wa Kamchape kwa mali zao kuchomwa moto na kuibwa ni Mwenyekiti wa Parokia ya Karema pamoja na makamu wake.

Mfanyabiashara Josephat Zongwe amelazimika kukimbia makazi yake akiacha nyuma uharibifu mkubwa ili kuokoa maisha.

Zongwe anasema alitoroka kupitia mlimani, mashambani (Mamboya) hadi Kapalamsenga usiku wa manane.

“Nikampigia simu dada yangu anayeishi Kahama. Akanitumia pesa ambazo nilikodi bodaboda kwa Sh 70,000 hadi Mpanda mjini; kesho yake nikasafiri kwenda Kahama.

“Hali ni mbaya, wala sijui itakuwaje,” anasema Zongwe ambaye nguruwe aliokuwa akiwafuga wameuawa.

Watu wengine waliolithibitishia JAMHURI kuharibiwa kwa mali zao ni Bosi Kazabi, Marius Mwanamese, Pascal Mwanangaya (nyumba mbili zimechomwa moto) na Daud Matipa (magunia zaidi ya 100 ya mpunga na mahindi yameibwa).

Lakini aliyeathirika zaidi ni Idrisa Ogoza wa Ikola ambaye waporaji wamemwibia zaidi ya Sh milioni 110 fedha taslimu na mali zake zingine.

“Ni kama hatuna viongozi wa serikali huku kwetu. RPC, DC na OCD hawatusaidii kitu. Wanawaacha watu wanafanya ujambazi mchana kweupe,” anasema Ogoza.

Anasema wakati duka lake likivamiwa, alimpigia simu OCD aliyekuwa amejificha kilomita chache nje ya Ikola, lakini hakumsaidia.

DC alikoroga, askari ajeruhiwa

Wakati lawama zikielekezwa serikalini kwa kuchelewa kudhibiti hali mwambao wa Ziwa Tanganyika, Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu, anadaiwa kukoroga zaidi mambo.

Taarifa kutoka vikao vya ndani vya chama wilayani Tanganyika zinasema kwamba Buswelu alibanwa kuhusu kauli aliyoitoa kuruhusu Kamchape aendelee kufanya kazi.

“Alipobanwa zaidi akajitetea akisema kuwa alilazimika kusema hivyo kwa kuhofia usalama wake,” anasema mtoa taarifa wetu.

Kwa upande mwingine, askari Polisi aliyefahamika kwa jina la Inspekta Shadrack anadaiwa kujeruhiwa vibaya na vijana wanaomuunga mkono Kamchape.

Inspekta Shadrack amelazimika kupelekwa Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo Dodoma.

“Alilazwa kwa siku kama tatu hivi, sasa anaendelea vizuri na ameruhusiwa,” anasema mtoa taarifa wetu kutoka Dodoma.

Kikosi maalumu chapelekwa, viongozi wagoma kuzungumza

Pamoja na lawama zinazoelekezwa kwa serikali kushindwa kuwasaidia wakazi wa Karema dhidi ya Kamchape, si Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Caster Ngonyani wala DC wa Tanganyika, Onesmo Buswelu, waliokuwa tayari kuzungumzia sakata hilo.

JAMHURI limeelezwa kwamba huenda ukimya wa maofisa hao wenye dhamana ya kulinda usalama wa raia na mali zao unatokana na kuwapo taarifa za kuwasili kwa kikosi maalumu kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kuzima kadhia hiyo.

Hata hivyo haikuweza kufahamika mara moja ni wapi kilipowekwa kikosi hicho kabla ya kuingia mitaani kupambana na Kamchape.

Mtazamo wa kisheria

Andiko la UNICEF la Aprili 2021, ‘Addressing Witchcraft in Tanzania’, linasema:

“The Witchcraft Act of 2002 stipulates that witchcraft includes sorcery, enchantment, bewitching, the use of instruments of witchcraft, the alleged use of magical or supernatural powers and the alleged possession of any supernatural beliefs and knowledge.

“Anyone found guilty of exercising witchcraft with the intent of causing harm, death, fear or misfortune to people can be sentenced to seven years’ imprisonment or more.”

Akizungumza na JAMHURI, Wakili wa kujitegemea mkazi wa Morogoro, Evarist Mnyele, amesema kwa mujibu wa sheria, anayepasawa kuwajibishwa ni Kamchape.

“Kuvunjika kwa amani na usalama Karema kumetokana na ujio wa Kamchape. Awali watu walikuwa wakiishi kwa amani na utulivu.

“Hii maana yake ni yeye ndiye amezua hofu kiasi kwamba kuna watu wamekimbia nyumba zao na kwenda kuishi Mpanda mjini; mali zao zimeharibika na hawajui mustakabali wa maisha yao.

“Serikali inapaswa kumkamata Kamchape haraka na kumfikisha mahakamani,” amesema. JAMHURI linaendelea kufuatilia matukio yanayofanyika katika Tarafa ya Karema hadi hali itakaporejea kama awali.


By Jamhuri