Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imeanza kuwa na mabadiliko makubwa ya kiutendaji katika kipindi cha miaka miwili iliyopita. Katika kudadisi hilo, Mwandishi Maalum amefanya mahojiano na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit C.V. Kakoko yanayobainisha hatua baada ya nyingine juu ya nini kimeimarisha utendaji wa Bandari. Endelea…

Mkurugenzi tangu umeteuliwa kushika nafasi ya Ukurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania imekuwa na mabadiliko makubwa katika utendaji, udhibiti wa nidhamu ya watumishi, mizigo kuingia na kutoka Bandarini, utaratibu wa kuhudumia wateja, na mambo mengine. Katika mahojiano haya tunalenga kubainisha ufanisi wa Bandari uliopatikana tangu Mhe. Rais Dk. John Magufuli aingie madarakani.

Swali: Wakati unaingia TPA wafanyakazi walikuwa katika hali ya wasiwasi kutokana na uongozi wa kiimla. Tangu umeingia, vyanzo vingi vya habari vinaonesha kuna utulivu wa hali ya juu bandarini na mambo yanakwenda kwa mujibu wa sheria. Je, ni jambo lipi hasa ulilofanya kurejesha amani bandarini?

JIBU:Menejimenti ya TPA inathamini na kutambua mchango mkubwa unaotolewa na wafanyakazi. Tunatambua kuwa wafanyakazi ndio wateja wa kwanza wa TPA na vikao vinafanyika hadi ngazi ya idara, lakini kubwa zaidi ni kwamba tumekuwa tukifanya kazi kwa karibu kwa kushirikiana na Chama cha Wafanyakazi Bandarini cha Dock Workers Union of Tanzania (DOWUTA). Tumekuwa tukiendelea kuheshimu na kutekeleza makubaliano mbalimbali tunayoingia baina yetu katika vikao vyetu vinavyohusisha pande zote mbili yaani Menejimenti na Wafanyakazi. Uhusiano huu mzuri uliokuwapo baina yetu na uelewa mzuri wa wafanyakazi ndio umepelekea kuwepo kwa amani bandarini.

Swali: Flow meter za KOJ zilielezwa kuharibika, ila baadaye taarifa zikaonesha kuwa zimeanza kufanya kazi. Je, kwa sasa mita hizo zinafanya kazi kwa ufanisi kiasi gani?

JIBU:Kwa sasa mita hizi hazitumiki kutokana na baadhi ya vifaa katika mtambo huo kuharibika baada ya kukaa kwa muda wa miaka mingi bila kutumika na kwakuwa gharama ya kuzitengeneza kwa sasa zilionekanakuwa kubwa sana hatua za manunuzi ya mita mpya zinaendelea.

Swali: Kulikuwapo mpango wa kununua mita mpya za kupimia mafuta yanayoingia nchini eneo la KOJ kwa nia ya kusaidiana na mita ya diesel iliyopo Mji Mwema, Kigamboni. Mpango huu umefikia hatua ipi?

Jibu: Hatua za manunuzi ya Mshauri na Mkandarasi zinaendelea na zinatarajiwa kukamilika katika robo ya kwanza ya 2017/2018.

Swali: Wastani wa meli zinazoingia umepungua, ila taarifa za mara kwa mara zimeonesha kuwa kiasi cha fedha zinazokusanywa kinaongezeka. Naomba ufafanuzi kuhusu suala hili na ufanisi uliopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita chini ya uogozi wako.

Jibu: Sio jambo jipya kutokea kwa mzigo kuongezeka au kushuka katika bandari zetu. Mfano hivi karibuni kwenye soko la China yalitokea mabadiliko na waagizaji mizigo nao wakapunguza idadi ya mizigo wanayopitisha katika bandari zetu.

Kwetu sisi jambo la msingi hasa ni kuhakikisha kwamba bandari zetu zote zinakuwa na ufanisi katika kutoa mzigo wakati wowote na kwamba tunakuwa tayari kuwahudumia wateja wetu bila kujali mazingira yaliyopo katika soko la dunia au usafirishaji.
Katika kipindi cha mwaka mmoja tumekuwa na ufanisi mkubwa kwanza katika kudhibiti mianya yote ya rushwa na uzembe ambapo hatuna uvumilivu kwa mfanyakazi mzembe au mla rushwa (zero tolerance).
Hii inamaana kuwa kwa mzigo uleule kiasi chote cha fedha kinapatikana kwa ukamilifu bila opotevu.

Swali: Katika kusafisha uozo, Bandari ya Dar es Salaam inatajwa kufukuza watumishi kadhaa walioonekana hawaendani na kasi ya Hapa Kazi Tu. Je, kwa sasa umefanikiwa kuondoa uzembe wa wateja kuambiwa muda wa kazi umekwisha, benki zimefungwa na wakati mwingine kuambiwa mifumo ya TEHAMA iko chini? Je, benki zinafanya kazi saa 24?

Jibu: Niwahakikishie wateja wetu wote kwamba tumeondoa na tumeweza kudhibiti uzembe. Tunafanya kazi saa 24 siku 7 kwa wiki. Tumeimarisha Idara yetu ya TEHAMA na mifumo husika na inapokuwa chini hatua za haraka huchukuliwa na wateja wetu sasa wanahudumiwa ipasavyo. Pia benki za NMB na TIB zipo, zinafanya kazi kwa saa 24 siku 7 za wiki ndani ya Bandari. Wito wetu sasa ni kwamba wateja watumie huduma hizi na wadau wetu wengine wote waingie katika kutoa huduma kwa saa 24 kwa siku zote 7 saba kwa wiki.

Swali: Je, wafanyakazi wanaokaidi maelekezo ya uongozi (kama wapo) ni hatua zipi mnazochukua kurekebisha hali hiyo?

Jibu:Kama nilivyotangulia kusema hapo juu hatuna uvumilivu (zero tolerance) na wafanyakazi wote ambao wanakaidi maelekezo ya kutoa huduma nzuri kwa wateja wetu. Tunashukuru kwa sasa wafanyakazi wote wanaendana na mabadiliko na wapo tayari kutoa huduma na naomba nitumie fursa hii kuwapongeza na kuwaomba waendelee kutoa huduma nzuri kwa wateja wetu kwa wakati mwafaka na kwa ufanisi.

Swali: Uamuzi wa ICDs kupewa mzigo baada ya kujaza Bandari umesaidiaje kuongeza mapato ya TPA?

Jibu: Kwa sasa tunatekeleza makubaliano (MoU) baina yetu na hizo ICD kwamba endapo Bandari ya Dar es Salaam itakosa nafasi ya kuweka mzigo kipaumbele kitakuwa ni kuipeleka iliyokosa nafasi bandarini kwenye ICD kwa utaratibu tuliokubaliana.

Hivyo basi, kwa kuweka mzigo Bandari ya Dar es Salam kabla ya kupeleka kwenye ICD ni wazi kabisa imetuongezea mapato tofauti na kugawana mzigo na ICD na wao kutupatia sehemu ya faida ya kuhudumia mzigo husika.
Swali: Serikali imeamua kununua meli katika maziwa ya Nyasa na Victoria. Ujenzi wa meli hizi umefikia hatua ipi?

Jibu:Ujenzi wa Meli mbili kati ya tatu katika ziwa Nyasa, Bandari ya Kyela sasa umekamilika na tunaendelea na hatua nyingine ya meli ya tatu kupitia TPA na kuanza taratibu za manunuzi za ujenzi wa meli katika ziwa Victoria kupitia Shirika la Meli (MSCL).

Swali: Kuna meli kubwa na kongwe kama mv Victoria katika Ziwa Victoria na mv Liemba katika Ziwa Tanganyika, ambazo zinahitaji kufanyiwa ukarabati mkubwa. Ukarabati utagharimu kiasi gani na utakamilika lini?
Jibu: Taratibu za kukarabati meli hizi zinaendelea vizuri kupitia MSCL.

Swali: Katika Central Corridor kulikuwapo mizani minane, ambayo ni Kibaha, Vigwaza, Mikese, Mikumi, Tanangozi, Makambako, Chimala na Mpemba. Je, mmechukua hatua zipi kupunguza muda unaopotea kwenye mizani kwa magari ya transit kutokana na utitiri wa mizani?

Jibu: Suala hili lipo chini ya TANROADS, na sisi kama wadau tunashiriki kwa karibu katika vikao vyote vya kuboresha ukanda huu wa usafirishaji (central corridor) na mpaka sasa idadi ya mizani imepungua kwa kiasi kikubwa.

Swali: Wakati unakuwa Mkurugenzi Mkuu wa TPA kulikuwapo Traffic Check Points 30 kati ya Dar es Salaam na Tunduma. Je, mmechukua hatua zipi kupunguza vizuizi hivi barabarani kwa nia ya kuwahisha kasi ya usafirishaji mizigo ya transit?

Jibu: Kama nilivyosema hapo awali kwa kirefu tumechukua hatua mbalimbali, hii ikiwa ni pamoja na kufanya vikao vya majadiliano na wadau mbalimbali wanaohusika na usafirishaji katika ukanda huu wa kati kama vile CCTFA, TRA, Jeshi la Polisi, Shirika la Reli Tanzania, TATOA pamoja na TANROADS na vizuizi vimepunguzwa.

Swali: Uondoshaji mizigo bandarini ni eneo lililokuwa na utata. Wakati Mombasa mzigo ulikuwa unatolewa bandarani kwa siku 5, Afrika Kusini siku 4, hapa Tanzania ilikuwa ni zaidi ya siku 10. Je, hali ikoje sasa?
Jibu: Kwa sasa hakuna utata wowote maana tumetoka kwenye siku 10-14 za awali na sasa tuko kwenye siku 8. Ila nikumbushe kwamba, kazi ya utoaji mzigo bandarini ni ya uwajibikaji wa pamoja kila mdau anayehusika katika sehemu yake ni lazima atimize wajibu wake.

Katika kutoa mzigo bandarini wapo wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na sisi wenyewe TPA tunawajibika na kuweka miundombinu, mazingira mazuri na vifaa vya kutosha, lakini pia wapo TRA, Mashirika yetu ya Reli ya TRC na TAZARA, TICTS, TFDA, TBS, wenye malori, Mawakala wa Ushuru na Forodha, Mawakala wa Meli, na wengie wengi. Sasa hawa wote wanapaswa kuwajibika na wasipowajibika inarudisha nyuma jitihada zetu za kutoa huduma nzuri.
Kwa hiyo kumekuwepo na mikutano ya pamoja na muda si mrefu tutafikia kiwango cha siku 5 hususani baada ya kutekeleza majukumu yetu kwa saa 24 siku 7 za wiki. Tukishaongeza mashine za ukaguzi sita (6) zaidi hali itafikia huko.

Swali: Bandari za Tanzania ziligubikwa na wizi, ambako makontena zaidi ya 11,000 yalitajwa kupotea au kuondoshwa katika Bandari Kavu bila kufuata utaratibu kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2012 na 2015 na hivyo kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 48. Wafanyakazi wanane walifunguliwa mashtaka. Je, hali hiyo uongozi wako umeidhibiti kwa kiasi gani hadi sasa?

Jibu: Kwa zaidi ya miaka miwili sasa hatuna tukio la upotevu wa mali ya mteja ndani ya bandari ya Dar es Salaam, hii ni kwa sababu mbalimbali lakini nyingi tayari nimeshazitaja hapo juu.
Maboresho katika TEHAMA yametusaidia sana katika udhibiti wa mapato kwa kuziba mianya yote ambayo iliiachwa wazi.

Swali: Kuna fomu ya C28 iliyopandishwa ada yake kutoka Sh 20,000 kwenda dola 200 za Marekani na ikiwa lori lina tela inalipiwa dola 400. Kenya wanayo fomu hii, lakini hawatozi hiyo dola 200 au 400 hali inayokwamsisha madereva wa Tanzania. Je, malalamiko haya umeyapata na umeyashughulikiaje?

Jibu: Sijapata malalamiko kama haya, na naomba kutumia nafasi hii kuwaomba wadau na wateja wetu pale wanapokuwa na malalamiko wawasiliane na TPA au ofisi husika. Hata hivyo nimepokea hoja hii na nina ahidi kuifanyia kazi.

Swali: Baadhi ya Bandari nchini (ikiwamo Bandari ya Dar es Salaam) zilikuwa na mtindo wa kuingiza vibarua hewa na kuingia mikataba ya zabuni mbalimbali isiyo na uhalisia. Je, tangu umeingia madarakani umeidhibiti mchezo wa vibarua hewa kwa kiwango gani? Je, kuna takwimu zozote za vibarua hewa waliolipwa bila kufanya kazi angalau kwa miaka miwili kabla ya uongozi wako?

Jibu: Suala la kulipa vibarua hewa kupitia kampuni tumelifanyia kazi na kulidhibiti na wapo watumishi ambao tumewachukulia hatua za kinidhamu. Kwa sasa kazi zote za vibarua zinaratibiwa vizuri ili kuepusha malipo kwa vibarua hewa na baadhi ya kampuni hazikupewa tena muda wa nyongeza baada ya kukamilisha muda wa awali ili kuondokana na tatizo hili.

Swali: Mfumo wa Tenkonolojia ya Mawasiliano na Habari Bandarini, umetajwa kuwa kikwazo cha ufanisi kwa muda mrefu ambako kampuni kadhaa zimepewa zabuni na kuishia kutofanya kazi kwa viwango vilivyotarajiwa. Tatizo hili umelipatia ufumbuzi gani hadi sasa?

Jibu: Tatizo la TEHAMA ndani ya Bandari limefanyiwa
kazi na tumekuwa tukiendelea kuiboresha mifumo yetu ya malipo kwa kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao eGA.
Kwa sasa ipo mifumo mikubwa zaidi na mipya ambayo inanunuliwa kuondoa kabisa changamoto hiyo.
Kada ya wafanyakazi wa IT sasa ina wafanyakazi wapya ili kuimarisha utendaji kupitia TEHAMA.

Swali: Chuo cha Bandari kinaendelea kufanya kazi, ingawa wapo watu wanaosema kwa sasa hakitoi wataalam kwa kasi sawa na zamani ilivyokuwa. Je, uongozi wako una mpango gani wa kukiendeleza chuo hiki kutoa wataalam na kuvutia wanafunzi kutoka nje ya nchi?

Jibu: Tumefanya maboresho makubwa ndani ya Chuo
chetu cha Bandari ikiwa ni pamoja na kurekebisha Uongozi, kupata usajili kutoka NACTE, kupitia upya muundo wa Chuo kwa kuajiri wakufunzi wenye taaluma na weledi na tupo katika mipango ya kupata majengo na eneo kubwa zaidi ili kuongeza miundombinu ya Chuo chetu.
Pia tunajipanga kuanzisha kozi mpya zitakazoendana na mabadiliko katika sekta ya uchukuzi na tunataka kukifanya chuo chetu kiwe kimbilio la wadau na wote wanaopenda kufanya kazi katika sekta ya usafirishaji hususan huduma za Bandari. Mipango itakapo kamilika tunatarajia tutaanza kutoa mafunzo kwa ngazi ya shahada.

Swali: Lipo tatizo la kampuni inayomilikiwa na mfanyakazi wa Bandari ya Hai Sub Suppliers ambayo imeendelea kuhudumu katika gati nane za Bandari ya Dar es Salaam kwa muda mrefu pamoja na kutangazwa na Mahakama kuwa haikuwa na sifa. Je, suala hili ambalo ni kero kwa watoa huduma bandarini umelishughulikiaje?

Jibu: Suala hili limefanyiwa kazi vizuri. Hata hivyo Mkataba wa Kampuni hii ulikamilika na hawafanyi tena kazi bandarini.

Swali: Serikali ilikuwa na mpango wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam na Ujenzi wa Bandari ya Mtwara. Hivi karibuni tumeshuhudia Mhe. Rais Magufuli akizindua Mradi wa Uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam (DSMGP). Je, utekelezaji wa mradi huu na ule wa Mtwara utaiongezea TPA uwezo kiasi gani katika kuhudumia wateja?

Jibu: Hii ni miradi mikubwa ambayo tunatarajia mara
baada ya kukamilika kwake Bandari zote hizi zitaongeza uwezo wa kuhudumia shehena kubwa ya mzigo. Mfano kwa bandari ya Dar es Salaam tunatarajia itaongeza shehena kutoka tani milioni 15 za sasa hadi kufikia tani milioni 28 mwaka 2022.
Serikali yetu kwa sasa inasisitiza juu ya uchumi wa viwanda hivyo ni matarajio yetu kwamba miradi hii imekuja wakati mwafaka hasa kwa kuzingatia kwamba kwa namna moja tunatoa mchango wetu katika kuunga mkono nchi ya uchumi wa viwanda kwani wenye viwanda wataweza kutumia miradi hii itakapokamilika kupitisha mizigo yao mbalimbali.

Swali: Katika Bajeti ya Mwaka 2016/2017, Serikali ilifanya uamuzi wa kisera kwa kuingiza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye gharama za kuhudumia mizigo ya Kimataifa (VAT on handling charges for transit goods). Uamuzi huu umelalamikiwa na nchi zinazopitisha mizigo hapa Tanzania na katika Bajeti ya Mwaka 2017/2018 Serikali imefuta VAT kwenye huduma za mizigo ya “transit”. Je, VAT ilipoteza wateja kiasi gani na kuondolewa kutaisadiaje TPA?

Jibu: Kwa sasa Serikali imeona kwamba ikiondoa VAT
katika huduma za kibandari itaweza kuongeza shehena ya mzigo na sisi tunashukuru kwani jambo hili limelalamikiwa kwa muda mrefu na wateja na wadau. Tunaamini bila shaka kwamba suala hili sasa litakuwa ni kivutio kwa wateja wengi zaidi kutumia huduma za bandari zetu mbalimbali.
Wateja wengi waliopotea ni kutoka DRC maeneo ya Lubumashi, Bukavu na Goma ingawa hata nchi nyingine walilalamika.

Swali: Katika kipindi hiki cha ushindani, Mamlaka imeweka vivutio vipi kuvutia wafanyabiashara waache kutumia Bandari za Beira (Msumbiji), Durban (Afrika Kusini), Mombasa (Kenya) na Walvis Bay (Namibia) zinazoonekana kuchukua masoko ya Malawi, Msumbiji, Zambia, Uganda, Rwanda na DRC waliokuwa wateja wa Bandari ya Dar es Salaam?

Jibu: Vivutio tulivyonavyo ni vingi nikivitaja vichache
ni pamoja na uwepo wa Ofisi za TPA katika nchi za DRC, Zambia, Rwanda, Burundi ambapo tumesogea karibu zaidi na mteja ili kumpunguzia adha ya mfanyabiashara kusafiri hadi Dar es Salaam kwa ajili ya kufuatilia mzigo wake.
Bandari pamoja na Wadau tunafanya kazi saa 24 siku 7 za wiki na tumeweka mifumo ya kisasa ya ulinzi CCTV kwa ajili ya usalama wa mizigo ya wateja wetu.
Serikali imeondoa VAT kwenye huduma za mizigo inayosafirishwa, tunao Wafanyakazi wanaowajibika na wenye ari ya kufanya kazi, vizuizi vya barabarani vimepunguzwa kwa kiwango kikubwa, tunatumia mifumo ya TEHAMA katika kutoa mizigo, tozo zetu ni shindani na hivi sasa Serikali inafanya Juhudi kubwa ya kufufua reli zetu na kujenga miundombinu ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) ambayo itarahisisha usafirishaji wa mizigo.

Swali: Je, TPA kwa sasa inayo miradi ipi mikubwa inayotekelezwa kwa nia ya kuboresha ufanisi wa Bandari mbalimbali nchini?

Jibu: Kwa sasa miradi mikubwa tuliyonayo ni ya kujenga na kuboresha miundombinu ya Bandari ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vifaa, kujenga bandari mpya na magati na kuboresha yale yaliyopo. Tumeanza kutekeleza Mradi wa Ujenzi wa Gati Jipya katika Bandari ya Mtwara na Mradi wa Maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam.
Mradi wa Kujenga Kituo cha Kupokelea Mafuta wa Chongoleani katika Bandari ya Tanga, kuna Mradi wa Kujenga Meli za Mizigo na Abiria kwa ajili ya gati zilizopo katika maziwa Makuu ya Tanganyika, Nyasa na Victoria. Kuna Mradi wa Kujenga magati ya Lagosa, Kalya, Sibwesa, Kabwe katika Ziwa Tanganyika, tunajenga magati Lushamba, Kyamkwikwi, Mwigombero, katika ziwa victoria na kule Nyasa kuna gati mbalimbali zinajengwa katika maeno ya Ludewa, Mbambabay, Liuli n.k. Kwa upande wa bandari mpya mipango ya kujenga bandari za Mwambani na Bagamoyo bado inaendelea na ipo katika hatua mbalimbali.
Mamlaka imeendelea kutwaa ardhi katika maeneo mbalimbali kwa matumizi ya Bandari Kavu katika dhana ile ile ya kusogea karibu na mteja.

By Jamhuri