Home Makala Ndugu Rais simama mwenyewe baba

Ndugu Rais simama mwenyewe baba

by Jamhuri

Ndugu Rais, wako watu wema wengi sana katika nchi hii ambao wana fikra nzito zilizo juu ya vyama vya siasa. Kwao wao ni nchi yangu kwanza! Na kama mkosi vile wako pia watu wenye fikra finyu kabisa ambao fikra zao zote ni kwa vyama vyao vya siasa badala ya nchi kwanza! Ole wao watu hawa! Ole wako Taifa langu!

Leo baadhi ya wabunge wanahasimiana na baadhi ya wakuu wa wilaya na mikoa, ustawi wa wananchi utawezekana vipi? Lakini baba ni nani chanzo cha yote haya?
Ndugu Rais naugulia kifuani mwangu nikiililia nchi yangu! Nawalilia masikini wa nchi hii! Nakulilia na wewe baba! Najililia na mimi mwenyewe! Ninachokitetea katika nchi yetu ni haki sawa kwa wote! Tamaa niliyonayo ni kuiona amani ikitamalaki katika nchi yetu! Nimekuwa na nitawahubiria watu wa Mungu upendo siku zote, mpaka pumzi yangu ya mwisho itakapoutoka mwili wangu, nami nirudi kwa Baba nikapumzike!
Ndugu Rais, vita unayopigana si juu ya damu na nyama, bali ni katika ulimwengu wa roho! Kumbuka kuna mambo ambayo mwanadamu hawezi akajisimamia mwenyewe bila mkono wa Mungu. Ili uikamilishe katika njia ifaayo kazi njema hii unayoifanya, yakupasa umwombe Muumba wako asimame badala yako! Mwambie ‘Simama mwenyewe Bwana!’ Naye Simba wa Yuda atakushindia! Usimtegemee mwanadamu hata kama ana bunduki na risasi!
Ndugu Rais, uliposema hukwenda Ikulu kufukua makaburi nilikwambia, basi jenga hiyo nyumba juu ya hayo makaburi halafu uone kama kuna mtu atakuja kupata usingizi humo ndani. Baba bwana, sasa unauliza kinyumenyume, eti, “Hata kuyapalilia tu jamani?” Baba yapalilie, lakini dawa ya jipu nikulitumbua, siyo kulipaka mafuta! Kwa hili unahitaji mkono wa Mungu! Mwambie Mwenyezi, “Simama mwenyewe Bwana!” naye atakutangulia!
Baba hebu waambie watu wako, hili kaburi la ESCROW umelipalilia tu au umelifukua kweli? Maana mshikemshike wake, badala ya kusikitisha unachekesha. Watu wamechanganyikiwa! Ambao hatuwaoni, hatuwaoni, lakini tuna hakika ugali wanaokula ni uleule waliokuwa wanakula miaka yote, ila sasa siyo mtamu kama zamani.

Mmoja kasema anarudisha pesa kumbe anapeleka pesa! Kurudisha ni kupeleka kitu kule ulikokitoa, iwe ni kwa kuazimwa, kupewa au kuiba.
Akazipeleka TRA ndiko alikozitoa? Fedha ulipewa na Juma. Rudisha, unamrudishia Asumani wapi na wapi?
Ndugu Rais, wengine wanaweweseka nadhani wanahitaji wasaidiwe. Anasema, “Mimi niko tayari kuzirudisha, lakini nazirudisha kwa nani? Toka mwanzo nilisema hizi fedha nilipata kwa wema.” Anahoji azirudishe kwa nani, ameishamsahau aliyempatia? Chaguo la Mungu lina watu mpaka kanisani!
Mwenye busara angehoji, kwanini nizirudishe fedha nilizopewa kwa wema?

Kwani zile fedha zilikuwa na chapa ya ESCROW? Haiwezekani kuwa alinipatia fedha zilizotokana na vyanzo vyake vingine vya mapato yake kama labda kuuza bia au mabibo? Lakini mababu walisema, “Mwizi hujishikisha mwenyewe!”
Huyu anaelewa kuwa upanga hautiwi uharamu kwa mauaji, bali yule aliyeutumia upanga huo kufanya mauaji! Unataka kuoa umekwama mahari.
Kwa wema tu umesaidiwa fedha ukalipa mahari, ukafunga ndoa.
Ikijakubainika kuwa fedha zile zilikuwa za wizi, ndoa yako inakuwa haramu? Hata hivyo, kama mtu ametumia madhabahu na majoho yake kuwatangazia Watanzania chaguo la Mungu, akilipwa, kuna ubaya gani?
Ndugu Rais, katika hili lazima haki itendeke sawa kwa wote! Kama kuna yeyote aliyehusika na ufisadi huu wa ESCROW na mbele ya mahakama za wanadamu ana kinga, Baba usimguse! Lakini ajitafakari ili atambue na wewe Baba pia utambue, kuwa mbele ya mahakama ya Mwenyezi Mungu mwizi hana kinga!

Ndugu Rais, uongozi ulioshindwa hukimbilia kuanzisha vikundi vya ajabu ajabu ili kuwaghiribu wananchi. Nilifarijika kusikia umekataa kukutana na kikundi kinachojiita Kamati ya nini siju! Ah! Samahani baba, hukukataa ila hujakutana nacho hadi leo! Wapotoshaji wakasema Rais amekataa kuonana na viongozi wa dini! Ni viongozi wa dini gani hawa ambao walionekana katika televisheni wakiwa uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere unaofanyiwa upanuzi, eti wanauombea! Iko wapi tofauti yao na ushirikina? Wanapofanya hayo fedha wanazotumia ni zile zitokanazo na sadaka zitolewazo katika nyumba za ibada au ni kodi ya masikini ambayo hulali, ukiikusanya? Hawa wamepoteza kabisa nguvu za Ki-ungu! Baba futa vikundi vyote visivyokuwa na tija kwa Taifa!

Ndugu Rais, huko nyuma niliwahi kusimulia miujiza niliyoishuhudia kwa macho yangu mwenyewe ikitendwa na viongozi wa dini wa wakati ule nikiwa kijana mdogo. Moja ni katika kanisa la Parokia ya Mkulwe wilayani Momba. Akiwa anatoa mahubiri waliingia wasichana waliokuwa wamevaa nguo zisizostahili. Padri aliwafukuza watoke nje ya kanisa, lakini walikaidi. Mmoja wao alikuwa binamu yangu. Mama alikuwa amenipeleka Mkulwe ili nikapate komunio ya kwanza, hivyo tulifikia kwao (kwa mjomba). Misa ilipoisha, walipofika nyumbani, wote waliziona siku zao!
Muujiza wa pili niliushuhudia kwetu Kamsamba wakati huo ndiyo naanza shule ya msingi. Mahakama ya Mwanzo haikuwa na nyumba ya hakimu.

Hakimu alikuwa anakuja mara mojamoja tu. Kwa kuwa alikuwa ni ndugu yake mama kila akija alifikia kwetu. Wakati huo Kamsamba watu hawajui kitu kinaitwa nyumba ya wageni, soda au bia. Akihukumu kesi ya ndoa aliamua kuivunja. Katika kutetea ndoa yake, mume akadai ndoa ilifungwa kanisani. Hakimu akaamuru Padri akaitwe aje aivunje ndoa. Padri alimwambia hana mamlaka ya kuvunja ndoa kwa kuwa imeandikwa alichounganisha Mungu mwanadamu asikitenganishe! Hakimu akaamuru kuivunja ndoa na akaamuru Padri ashikiliwe! Hakuna aliyemgusa Padri.
Naye alifungua kitabu chake cha sala na kwa mwendo wa pole kabisa

akawa anaelekea kanisani kwake! Tulipotoka shuleni tulimkuta hakimu ameugua karibu ya kufa! Viongozi wa dini wanaohubiri upendo wa Mwenyezi Mungu kwa waja wake wamebaki wachache!
Ndugu Rais unachokifanya kuhusu ufisadi wa ESCROW unawafanya Watanzania sasa waanze kuelewa kwanini Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwakataa baadhi ya watu wasigombee uongozi katika nchi hii.
Mwalimu alisema, “Nchi haiwezi kuendeshwa kihunihuni! Kazi za kihunihuni ziko nyingi huko mabarabarani. Mhuni akafanyie uhuni wake huko! Ukipewa kazi ya nchi lazima ujiheshimu!”

 

PASCHALLY MAYEGA
SIMU: 0713 334 239

You may also like