Kundi la vitengo kadhaa vya usalama vimetumwa katika maeneo mbalimbali ya jiji la Nairobi ili kusubiri maandamano ya vijana yanayopangwa kufanyika siku ya Alhamisi.

Waandamanaji hao wameapa kuandaa maandamano ya kuelekea ikulu ya rais ikiwa ndio kilele cha maandamano ya siku saba kuelezea hasira na kutoridhishwa kwao na serikali ya sasa ya Rais William Ruto.

Baada ya maandamano mabaya yaliyoshuhudiwa Jumanne wakati waandamanaji walipovamia Bunge wakipinga Muswada wa Fedha wa 2024, timu za usalama zinaonekana kudhamiria kuzuia jaribio lolote la kuingia Ikulu iliyoko karibu na mji huo.

Maafisa wa usalama wamefunga barabara zote zinazoelekea na kuunganisha Ikulu, huku madereva wakielekezwa kutumia njia mbadala.

Maafisa waliojihami vikali pia wamewekwa kimkakati karibu na Ikulu na hakuna mtu anayeruhusiwa hata kukaribia kiingilio chochote.Vifaa vya usalama vya kijeshi pia vimetumwa karibu na Ikulu ili kuziba barabara inayoelekea Ikulu.

Licha ya Rais William Ruto kukubali kuondoa Muswada tata wa fedha wa 2024, waandamanaji hao wameapa kuendelea na mikutano hiyo wakionyesha kutokuwa na imani na serikali ya Kenya Kwanza.

Kufikia sasa hali imeendelea kuwa ya utulivu na shwari katika maeneo mengi nchini Kenya.