Mahakama mjini New York imemhukumu rais wa zamani wa Honduras kifungo cha miaka 45 jela kwa makosa ya ulanguzi wa dawa za kulevya.

Juan Orlando Hernandez alihukumiwa Jumatano kwa kuyasaidia makundi ya wauzaji wa dawa za kulevya kuingiza nchini Marekani tani 500 za cocaine. Waendesha mashitaka wa Marekani walisema Hernandez aliigeuza Honduras kuwa taifa la dawa za kulevya wakati alipokuwa rais kuanzia mwaka wa 2014 hadi 2022.

Waendesha mashitaka walisema alitumia fedha hizo ili kujitajirisha na kufanya udanganyifu katika uchaguzi nchini Honduras. Jaji Kevin Castel alimuelezea rais huyo wa zamani kuwa mwanasiasa mwenye nyuso mbili ambaye alikuwa na uchu wa madaraka. Hukumu yake jana pia ilijumuisha faini ya dola milioni nane.

Hernandez, mwenye umri wa miaka 55, aliiambia mahakama jana kuwa hakuwa na hatia na alikuwa ameshitakiwa bila haki. Rais huyo wa zamani wa Honduras awali alidokeza kupitia mawakili wake kuwa angekata rufaa kupinga hukumu hiyo.