Home Kurasa za Ndani Barua ya Wana Moshi kwa Rais John Magufuli

Barua ya Wana Moshi kwa Rais John Magufuli

by Jamhuri

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. John Pombe Magufuli, barua yetu inahusu BOMOA BOMOA YA RAHCO KATIKA ENEO LA PASUA BLOCK JJJ ILIYOSABABISHWA NA MGONGANO WA MAMLAKA MBILI ZA SERIKALI.

Mheshimiwa Rais, kwanza tunapenda tuchukue fursa hii adimu, kukupongeza kwa dhati kabisa kwa kuchaguliwa kwako kuliongoza Taifa la Tanzania, na tunathubutu kusema, hakika tulichelewa sana kupata Rais wa aina yako, tuliyemtamani kwa miaka mingi.

Tunapenda kuchukua fursa hii, kukuhakikishia kuwa tunaunga mkono juhudi zote zinazochukuliwa na Serikali katika kudhibiti ufisadi, ubadhirifu, wizi wa mali ya umma, matumizi mabaya ya rasilimali na uonevu dhidi ya watanzania masikini.

Ni mambo ambayo yamelirudisha nyuma taifa letu, na kufanya watu wachache waishi maisha mazuri, huku kundi kubwa la watanzania wakiishi katika umasikini licha ya rasilimali tulizonazo. Tunakushukuru mheshimiwa Rais kwa kutufungua katika minyororo hii.

Ni kwa msingi huo, tunakuomba na kukusihi, uipitie barua yetu ya malalamiko na utumie mamlaka uliyonayo ili upatie ufumbuzi mgogoro wa ubomoaji wa nyumba za wananchi wasio na hatia katika eneo la Pasua Block JJJ Katika Manispaa ya Moshi unaotaka kufanywa na shirika Hodhi la Reli (RAHCO).

Tunapenda kukuthibitishia kuwa mgogoro huu ni tofauti kabisa na migogoro mingine yote kati ya RAHCO na wananchi. Sisi hatuko ndani ya mita 15 au 30 wala hatujavamia eneo hili bali tulipewa na mamlaka halali ya ugawaji ardhi ambayo ni Halmashauri ya Manispaa ya Moshi baada ya kupata baraka zote za Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Wala katika eneo hili hakuna hata kipande cha reli na pia si miongoni mwa maeneo yale ambayo ni ya reli ya tangu UKOLONI, bali eneo hili lilitengwa na Halmashauri yenyewe wakati ikipanga mji mwaka 1962, na kutenga eneo ambalo lingejengwa viwanda (havikujengwa) na kama vingejengwa, ingejengwa reli ya kuvihudumia.

Mheshimiwa Rais, mgogoro katika eneo hili si mgeni kwako, kwani mwaka 2007, baadhi yetu tulikufuata Dodoma wakati huo ukiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kukulalamikia juu ya kubaguliwa katika ugawaji wa viwanja hivi.

Msingi wa malalamiko yetu wakati huo 2007 yalihusu viongozi wa kisiasa kujigawia viwanja wao baada ya wewe kama waziri mwenye dhamana, kuridhia mabadiliko ya matumizi ya ardhi kutoka Corridor ya kujenga kipande cha reli kuhudumia viwanda na kuwa makazi.

Kabla ya kubadilishwa matumizi yake, huko nyuma kuanzia mwaka wa 1990, wapo wananchi 65 walivamia eneo hili na kujenga makazi ya kudumu, lakini Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, ikazivunja nyumba hizi kwa nguvu mwaka 1995.

Uvunjaji wa nyumba hizi uliibua mgogoro mkubwa wa kiserikali na kisiasa ambapo viongozi mbalimbali wa kitaifa wa Serikali waliingilia kati, na kuagiza libadilishwe matumizi yake na kupimwa viwanja na wale wananchi 65 wapewe kipaumbele katika ugawaji.

Tarehe 10.10.2007, ulikuja Moshi na kuhutubia mkutano wa hadhara eneo la Pasua na kuwaambia wananchi eneo hilo lilishabadilishwa matumizi lakini katika ugawaji uliokuwa ukiendelea, wale wananchi 65 waliovunjiwa nyumba mwaka 1995 hawapewi viwanja badala yake viongozi ndio wanaogawiwa.

Mheshimiwa Rais, taarifa rasmi ya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, katika kifungu cha 5.1 katika ukurasa wa 6 chini ya kichwa cha habari “Eneo lililokuwa limependekezwa kujengwa reli kitalu “JJJ” Pasua”, inaonyesha Halmashauri wakati ikiandaa master plan yake mwaka 1962, ilitenga eneo la viwanda ambavyo vingejengwa na Serikali. Ili kuhudumia viwanda hivyo, Halmashauri ikatenga Corridor ambayo ilipendekezwa ijengwe kipande cha reli kwenda kuhudumia viwanda hivyo, kama vingejengwa kama lengo lilivyokuwa mwaka huo wa 1962.

Hata hivyo, viwanda hivyo havikujengwa na badala yake eneo lote lililokuwa limetengwa kwa ajili ya viwanda lilivamiwa na wananchi na kujengwa makazi ya kudumu na hivyo kufanya azma ile ya kujengwa viwanda kufa. Hii maana yake ni kuwa hata ile Corridor iliyokuwa imetengwa ikawa imepoteza umaana wake uliokusudiwa.

Eneo hilo nalo likavamiwa na wananchi 65 miaka ya 1990 kama tulivyotangulia kueleza wakajenga nyumba, lakini Halmashauri ya Manispaa ya Moshi ikazivunja mwaka 1995, tukio ambalo lilileta mgogoro mkubwa kati ya Serikali Kuu, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na viongozi mbalimbali walifika Moshi kutatua mgogoro huu.

Mwaka 2002, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi ikaandaa rasimu ya mapendekezo ya mabadiliko ya Corridor hiyo kutoka viwanda na kuwa makazi na ombi hilo likakubaliwa na wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi tarehe 18.10.2002 wakati huo ikiwa chini yako, kwa kumbukumbu namba TP/P132/III/79 na kuilekeza Halmashauri kuandaa michoro mipya. (Rejea taarifa ya Halmashauri).

Michoro ya mipango miji namba MMC/MISC/62/0104 wa mwaka 2004 na mchoro namba MMC/MISC/136/108 wa mwaka 2008 ikaidhinishwa na Wizara na kubadili matumizi yale ya awali ya Corridor hiyo na ikapimwa upya kama maelekezo ya wizara yalivyokuwa. Wizara kwa ramani ya upimaji zenye usajili namba 39784 ya mwaka 2004, namba 60925 ya mwaka 2009 na 62414 wa mwaka 2010, iliidhinisha upimaji huo na viwanja 90 vilipimwa na kugawiwa kwa wananchi wakiwamo wale 65 waliovunjiwa nyumba mwaka 1995.

Wananchi waliopo Block JJJ Pasua, walipewa taarifa za kupewa viwanja, barua ya toleo (letter of offer), hati za umiliki na kujenga nyumba kwa kufuata taratibu zote ikiwamo michoro kupitishwa na Halmashauri na kupatiwa kibali au Building Permit. Tunalipa kodi zote za Serikali ambazo ni Land Rent na Property Tax kwa wenye majengo.

Katika barua ya toleo, Halmashauri ilitupa masharti ya kujenga na kukamilisha ujenzi ndani ya miezi 36 na wale walioshindwa, waliandikiwa barua za kusudio la kunywang’anywa viwanja. Wengi wetu tulilazimika kukopa fedha kwenye mabeki na taasisi nyingine za fedha ikiwamo SACCOS ili kukamilisha ujenzi ndani ya muda huo wa miezi 36.

Lakini kwa mshangao mkubwa, tarehe 14.09.2017, maofisa na mawakala wa RAHCO wakatuwekea alama X, nyumba zetu wakitutaka kubomoa nyumba zetu tulizozijenga kwa tabu bila FIDIA kwa maelezo kuwa tumevamia eneo la Reli.

Tunamshukuru RC Kilimanjaro Anna Mghwira na kamati yake ya ulinzi na Usalama kwa kuingilia suala hili. Hata hivyo, pamoja na RC kuunda tume yake, lakini ipo “Minong’ono” kuwa wajumbe kutoka RAHCO walikataa Halmashauri isiingize ramani, michoro na vielelezo vingine muhimu kuthibitisha uhalali wa ugawaji huo kama viambatanisho.

Mheshimiwa Rais, tangu tuwekewe alama ‘X’ na kutakiwa kuondoka pasipo kulipwa fidia, tunaishi kwa hofu na tumeathirika kiakili na kisaikolojia tukijiuliza kosa letu sisi kama wananchi masikini ni lipi wakati ugawaji huu ulifanywa na mamlaka halali ya Serikali baada ya kupata baraka za Wizara yenye dhamana. Tunajiuliza tumekosea wapi hatupati majibu.

Tunafahamu na sheria ziko wazi kuwa pale ambapo kuna makosa yaliyotendwa na watumishi wa Serikali au taasisi yoyote, Serikali hiyo au taasisi ndio inayobeba dhamana ya madhara yote yaliyojitokeza. Sisi hatukuvamia eneo bali tulipelekwa hapo na Halmashauri.

Tunakuomba na kukusihi sana Mheshimiwa Rais, utumie mamlaka uliyonayo kusimamia jambo hili ili haki itendeke katika mgogoro huu kwa vile sisi kama watanzania masikini, hatukuvamia eneo hilo bali tulipewa na mamlaka halali ya ugawaji ardhi.

Mheshimiwa Rais, tunafahamu, kutoka mahali tupopewa na Halmashauri tukajenga nyumba hizi ni kilometa 1.5 kufika stesheni kuu ya Moshi. Bado treni inaweza ikaingia stesheni na kuondoka kwenda Arusha kwa kupitia reli ya Arusha kama dhamira itakuwa ni hiyo.

Kwa uelewa mdogo tulio nao, hata kama basi lengo halikuwa kuhudumia viwanda pekee bali treni ambayo haitaki kuingia stesheni iweze kupita hapo na kuunga na ile ya Arusha, bado pangeweza kutafutwa eneo ambalo halijajengwa na kuichepusha.

Mgogoro huu kwa sura yake ulivyo, ni kati ya Halmashauri na RAHCO, lakini umewaingiza wananchi wasio na hatia katika matatizo makubwa, katika mahangaiko makubwa ya kiakili na kisaikolojia ambayo ni wewe peke yako unaweza kutusaidia.

Kuvunja nyumba hizi za wananchi masikini wakiwamo wastaafu walioitumikia nchi hii kwa uaminifu mkubwa, kungeweza kuepukwa kama mapendekezo tuliyoyasema hapo juu yatazingatiwa. Tunaamini hili liko ndani ya uwezo wako.

Pia kama itakupendeza, unaweza kuwaita watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na RAHCO ili kujua nani ni mkweli ili hata pale utakapoamua kufanya maamuzi kama baba, uwe umepata picha kamili ni nani anayestahili kuadhibiwa.

Tuliwasilisha pia malalamiko ya mgogoro huu kwa viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ngazi ya mkoa Kilimanjaro ambao walituahidi kulifikisha suala hili kwa katibu mkuu wa CCM mheshimiwa Abdulrahaman Kinana ili alilete kwako.

Mheshimiwa Rais, tunapenda tukuthibitishie, sisi hatupingi maendeleo. Kama Serikali na RAHCO wanalihitaji eneo hili kwa maslahi ya umma, basi watupe fidia kwa mujibu wa sheria na pia kutupa muda maalum wa kuondoka kama suala la kubaki eneo hilo litashindikana.

Pamoja na barua hii, Tunaambatanisha baadhi ya nyaraka ambazo ni pamoja na taarifa ya kupewa kiwanja, letter of offer, title deed, building permit na nyaraka za ulipaji wa kodi mbalimbali za Serikali ili uweze kujiridhisha. Hatutaweza kuzifungasha nyaraka za kila mmoja wetu, lakini hizi baadhi zinawakilisha sampuli ya nyaraka hizo.

Tunatanguliza shukrani zetu za dhati kwako wewe binafsi kwa namna mnavyosimamia haki za watanzania tukiamini utalisimamia jambo hili ili haki iweze kutendeka kama ambavyo siku zote umesimama upande wa wanyonge.

Tunakusihi na kukuomba sana, wewe ni baba wa wote, libebe hili tatizo la wanao. Hata kama itaonekana ni lazima tuondoke licha ya kwamba hatukuvamia eneo hili, tunakuomba utuonee huruma ili tulipwe fidia na kupewa muda maalum wa kuondoka.

Pamoja na barua hii, tunaambatanisha nyaraka zote muhimu tangu mwanzo wa kupewa viwanja, hati miliki, vibali vya ujenzi na uthibitisho wa malipo ya kodi na taarifa maalumu ya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kuhusiana na ugawaji wa eneo hilo ili kukuthibitishia kuwa hatukuvamia eneo hilo bali tuliingizwa hapo na Halmashauri.

Mungu akubariki sana,

Wamiliki wa Viwanja

Block JJJ Section V

S.L.P 1115

MOSHI

You may also like