Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Pwani

Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa amesema ujenzi wa miundombinu ya barabara nchini unafanyika kwa umakini na viwango vya ubora chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Waziri Bashungwa ameyasema hayo leo Septemba 20, 2023 mbele ya wananchi wa Ikwiriri mkoani Pwani ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa mikoa ya Kusini.

“Sisi kazi yetu ni kutekeleza yale ambayo Mhe. Rais ametuagiza, kwenye maelekezo uliyotupatia ya utiaji saini mikataba mbalimbali ambayo inakaribia trilioni 2 hata TARURA watakuwepo kuonesha namna Serikali yako ilivyojipanga katika ujenzi wa barabara”, amesema Mhe. Bashungwa.

Katika hatua nyingine Waziri Bashungwa amesema Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameagiza upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Barabara ya Mabasi yaendayo haraka kutoka Mbagala – Vikindu ufanyike haraka ili utaratibu wa kuanza ujenzi uanze mara moja.

“Mhe. Rais BRT kutoka Mbagala rangi tatu hadi vikindu umetuelekeza usanifu ufanyike haraka ili barabara hiyo na njia nne ije  mpaka Vikindu ili wananchi wa mkoa wa hapa Pwani na Rufiji waweze kuingia Dar es Salaam kwa wepesi na kutoka kwa wepesi”- amesema Mhe. Bashungwa.

Naye Mbunge wa Rufiji ambaye pia ni  Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohammed Mchengerwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia kutoa kiasi cha Shilingi Bilioni 75 kuanza ujenzi wa barabara ya Nyamwage – Utete yenye urefu wa kilometa 37 na tayari wakandarasi wanaendelea na ujenzi wa barabara hiyo.

“Naomba nichukue nafasi hii kukushukuru Mhe. Rais kwa kuridhia kujenga barabara ya Ikwiriri- Mkongo kwa kiwango cha lami na tayari mkandarasi yupo site amekwishaanza kujenga daraja la mbambe na barabara itakayotoka mbambe kuja hapa Ikwiriri mjini”- ameongeza Mhe. Mchengerwa.